Sahihi kuivunja KDA

15Sep 2017
Mhariri
Nipashe
Sahihi kuivunja KDA

RAIS John Magufuli amevunja rasmi Wakala wa Uendelezaji wa Mji wa Kigamboni (KDA) katika Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es
Salaam.

Hatua ya Rais ilitangazwa juzi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, na kuitaka mamlaka hiyo kukabidhi majukumu yote ya upangiliaji na uendelezaji kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni.

Lukuvi alitangaza uamuzi huo kwenye kikao cha pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali, dini na vyama wa Wilaya ya Kigamboni kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Lukuvi alisema kumekuwa na migogoro ya muda mrefu juu ya mamlaka hiyo huku Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile akiiomba serikali kuingilia kati suala hilo, hivyo Rais amesikiliza kilio hicho.

Alisema kuanzia juzi hakuna KDA na kuwa Rais Magufuli ameelekeza masuala yote yaliyokuwa yakifanywa na KDA, ikiwa ni pamoja na uthamini, upangaji, utoaji vibali vya ujenzi yatafanywa na Manispaa ya Kigamboni.

Lukuvi alisema anatoa miezi sita kwa KDA kufungasha virago vyao na kukabidhi nyaraka zote, ikiwa ni pamoja na kuwaelekeza namna ya ufanyaji kazi kwa manispaa hiyo. Kwamba kuanzia juzi hati yoyote itakayotolewa iwe imesainiwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni.

Aliwataka pia kuondoa urasimu na kuhakikisha watu wanapimiwa maeneo yao na kupewa hati ndani ya mwezi mmoja.

Uamuzi huo ulionekana kupokelewa kwa mikono miwili na wakazi wa Kigamboni kupitia mwakilishi wao Dk. Ndugulile aliyemshukuru Rais kwa kusikia kilio cha wananchi wa Kigamboni na kuivunja KDA, huku akiitaka halmashauri hiyo kusimamia vyema jukumu la kuipanga na kuiendeleza Kigamboni.

Kwa muda mrefu kumekuwapo na malalamiko ya wakazi wa Kigamboni ambao walikuwa wakiilalamikia KDA kwamba iliwasababishia usumbufu mkubwa kutokana na kuamriwa kusitisha shughuli zote za uendelezaji wa maeneo yao.

Walilalamikia hatua hiyo kuwa iliwaacha katika umaskini kutokana na usitishaji wa shughuli zao.

Kibaya zaidi walikuwa wakilalamikia kutokulipwa fedha zao za fidia kwa ajili ya kupisha maeneo yao kuruhusu ujenzi wa mji wa kisasa Kigamboni. Suala la ujenzi wa mji mpya lilizua malumbano na mjadala hadi ndani ya Bunge.

Kulikuwapo na malalamiko kuwa baadhi ya watendaji wa wakala huo walikuwa wakishirikiana na wajanja wachache kuwatapeli wananchi maeneo ya pembezoni mwa barabara baada ya kujifanya kubadili barabara ambayo wahusika wengi wakiwa hewa wameshalipwa na serikali mabilioni ya shilingi na kubadili ramani kukwepa maeneo yaliyolipwa ili wajanja wajimilikishe upya pamoja ma kuwa wamelipwa.

Malalamiko mengi ya wananchi wa Kigamboni yalikuwa yanaonyesha kuwa walikuwa wamekosa imani na KDA kutokana na kutenda mambo ambayo ni kinyume cha kuanzishwa kwake.

Serikali ilitangaza kuanzishwa KDA mwaka 2013 kwa ajili ya ujenzi wa mji huo huku kukiwa na malalamiko ya wananchi wa Kigamboni walioongozwa wakiongozwa na Dk. Ndugulile kupinga mradi huo kwa madai ulianzishwa kinyume cha sheria.

Hata hivyo, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, alipongeza na kutetea mpango huo akisema kuanzishwa kwa wakala huo kutaisaidia kusimamia vizuri kupanga mji wa Kigamboni kama inavyotakiwa.

Tibaijuka aliongeza kuwa kuanzishwa kwa KDA, kutaifanya Kigamboni kuwa na mamlaka yake kamili, ikiwamo kuwa na baraza la madiwani ambalo litakuwa na jukumu la kupanga mipango yao.

Hatua iliyochukuliwa na Rais ni sahihi kwa kuwa utata uliokuwapo wa mamlaka halali ya kusimamia mji wa Kigamboni kati ya Manispaa na KDA utakuwa umemalizika, baada ya manispaa hiyo sasa kupewa rasmi mamlaka hiyo.

Habari Kubwa