Safari bado ndefu usafiri wa majini

12Jan 2017
Mhariri
Nipashe
Safari bado ndefu usafiri wa majini

WATOTO watano wa familia moja walikufa maji baada ya boti ya MV Burudan iliyokuwa imebeba watu nane wa familia hiyo na wengine zaidi ya 30 kuzama kwenye Bahari ya Hindi na kusababisha vifo vya watu 12 juzi.

Ajali hiyo ilitokea alfajiri baada ya boti hiyo kupigwa na mawimbi makali na kuzama, wakati ikitoka eneo la Sahare Kasera jijini Tanga kwenda Pemba.

Nahodha wa boti hiyo, Badru Saidi alifariki dunia kwenye ajali hiyo iliyotonesha kidonda cha ajali za usafiri wa majini nchini, kubwa zaidi ikiwa ile ya Mv Bukoba iliyotokea Ziwa Victoria, jijini Mwanza karibu miaka 21 iliyopita na kuua watu 1,000.

Mbali na ajali ya Mv Victoria, tukio lingine kubwa linalofanana na mkasa huo ni kuzama kwa meli ya MV Skagit ikiwa na abiria 250 katika bahari ya Chumbe, Zanzibar Julai 18, 2012.

Pamekuwa na matukio mengine mengi yaliyochukua uhai wa Watanzania wenzetu katika Bahari ya Hindi na Ziwa Tanganyika tangu kutokea kwa ajali ya Mv Bukoba na kuzama kwa MV Burudan juzi, Nipashe tunakumbusha, na kujiuliza ajali hizi, nyingi zikiwa ni za kizembe, zitaendelea mpaka lini?

Kimsingi, Nipashe tunaona, kama mamlaka inayohusika na usafiri wa majini, SUMATRA, na wanachi kwa ujumla wangetafakari kwa makini ajali ya Mv Bukoba, matukio ya watu kupoteza maisha kwenye maji yalipaswa kuwa ya nadra sana nchini.

Lakini kwa sababu wananchi wapo tayari kuweka roho zao rehani, na kwa sababu SUMATRA haijapanuka kiasi cha kutosha kusimamia kila chombo cha usafiri wa majini, pengine, ndiyo maaana juzi tumepoteza Watanzania wengine 12 katika mazingira ambayo tunathubutu kusema ni ya uzembe.

Tumepoteza Watanzania wengine 12 katika mazingira ambayo tunathubutu kusema ni ya uzembe, kwa sababu kwanza taarifa zilizopo ni kuwa MV Burudan haikuwa na leseni ya kubeba abiria bali mizigo.

Aidha, tumepoteza Watanzania wengine 12 katika mazingira ambayo tunathubutu Nipashe kusema ni ya uzembe, kwa sababu boti hiyo haikuwa na vifaa vya uokoaji sanjari na kuwa na mawasiliano ya uhakika na rada ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kutokana na dhoruba baharini.

Na tumepoteza Watanzania wengine 12 katika mazingira ambayo tunathubutu kusema ni ya uzembe, kwa sababu abiria zaidi ya 30 hao waliopanda MV Burudan usiku wa kuelekea maafa hayo walitakiwa kujua kuwa wanaingia kwenye chombo kisicho salama.

Abiria zaidi ya 30 hao waliopanda MV Burudan usiku wa kuelekea maafa walitakiwa kujua kuwa wanaingia kwenye chombo kisicho salama, Nipashe tunasema, kwa sababu bandari yenyewe iliyotumika ni bubu na baadhi ya manusura wameeleza kulazimika kutumia usafiri hatarishi kwa sababu hakuna chombo cha uhakika kinachohudumia kati ya Tanga na Pemba.

Lakini wasafiri wa majini wanapaswa kujua kuwa hakuna adha ambayo utatuzi wake una thamani ya uhai wa binadamu, kiasi cha kuwa radhi kutumia usafiri kama wa MV Burudan.

Aidha, wamiliki na manahodha wa vyombo vya majini ni lazima wafahamu kuwa kutokea tu kwa ajali majini hakumaanishi kupotea kwa uhai wa hata mtu mmoja endapo masharti ya usalama wa usafiri huo yatakuwa yamezingatiwa.

Alisema kati ya watu 12 waliyopoteza maisha kutokana na ajali hiyo, sita ni watoto na kwamba miili ya marehemu hao yote ipo katika Hospitali ya Rufani ya Bombo ili itambuliwe na kuchukuliwa na ndugu zao.

Aliongeza kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba kati ya watu 30 na 35 na kwamba Polisi inawasiliana na mamlaka inayosimamia vyombo vya usafiri wa majini na nchi kavu, ikiwemo SUMATRA, ili kubaini idadi halisi ya abiria ambao walikuwa kwenye boti hiyo.

Kamanda Wakulyamba alisema bado hawajabaini chanzo cha ajali hiyo ingawa mashuhuda walidai chombo hicho kilipigwa na mawimbi makali eneo la nyuma na hivyo kupoteza mwelekeo na kuzama.

Alitoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya majini kuhakikisha wanakuwa na vifaa vya uokoaji sanjari na kuwa na mawasiliano ya uhakika na rada ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kutokana na dhoruba baharini.

BANDARI BUBU
Mashuhuda hao waliendelea kueleza kuwa eneo la Sahare jijini humu, mbali na kutumiwa na wavuvi, limekuwa miongoni mwa bandari bubu ambazo zimekuwa zikipitisha bidhaa haramu nyakati za usiku kutoka visiwani Pemba na maeneo mengine.

Waliiiomba serikali kuhakikisha inawapatia usafiri wa uhakika na wa gharama nafuu ili kuwaepusha kutumia vyombo ambavyo havina usajili wa kusafirisha watu kwenda visiwani Zanzibar.

Mwanamoa Mohamed, mmoja wa watu waliokutwa na gazeti hili eneo la Sahare, alisema sababu kubwa ya watu kusafiri kwa vyombo hivyo visivyo na ithibati ni kutokuwapo kwa vyombo vya uhakika vya usafiri wa Tanga-Pemba zaidi ya ndege.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Bombo, Godlack Mbwilo, alidhibitisha kupokea miili ya watu 12 pamoja na majeruhi 25 ambao wanapatiwa matibabu na kueleza kuwa miongoni mwao walikuwa wanaendelea vizuri huku baadhi wakiwa na hali mbaya kutokana na majeraha waliyopata.

Emanuel Mniga (30), mmoja wa majeruhi hao ambaye ni mkazi wa Morogoro, alisema chombo hicho kilianza safari juzi majira ya saa nne usiku, lakini ilipofika majira ya saa sita usiku, walipata dhoruba ya kupigwa na upepo mkali uliosababisha chombo kianze kuzama.

WATOTO WATANO
Ambialo, mkazi wa Pemba ambaye ni baba mdogo wa watoto watano waliofariki dunia, akizungumza kwa shida baada ya kupata fahamu, alisema maji yaliwashinda nguvu kisha kuzama.

Alisema kuwa wenye ujuzi wa kuogelea, waliogelea kwa muda mrefu hadi majira ya saa 10:15 alfajiri walipookolewa na wavuvi waliokuwa wakivua samaki baharini.

Hata hivyo, Ambialo alishindwa kueleza vizuri jinsi alivyofanikiwa kupamba na maji ya bahari hadi pale walipookolewa kutokana na kushindwa kuzungumza kwa ufasaha.

Lakini, mjomba wake na Ambialo, Masoud Abdallah, alisema kuwa katika boti hiyo mpwa wake huyo alikuwa na wanafamilia wengine saba wakiwamo watoto watano.

Abdallah alisema kuwa kati ya watu wazima watatu wa familia hiyo waliokuwa kwenye boti hiyo, wawili wameokolewa na mwanamke mmoja hajulikani alipo.

ZANZIBAR WATOA TAMKO

Akizungumza na Nipashe visiwani humu jana mchana, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini, ZMA, Abdallah Kombo, alisema boti hiyo imesajiliwa Zanzibar na cheti chake kilikuwa kinafikia ukomo Oktoba mwaka huu, lakini haina leseni ya kusafirisha abiria.

“Taarifa kamili wanazo wenzetu SUMATRA na tayari timu yetu ya ZMA imeshakwenda Tanga kwa ajili ya kupata taarifa zaidi,” alisema Kombo.

Alisema chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana kwa kuwa boti hiyo iliondoka katika bandari isiyo rasmi hivyo hata idadi ya watu waliokuwamo kwenye boti hiyo nayo bado haijajulikana.

Alisema ajali hiyo ni ya kwanza kutokea mwaka huu na kuwataka manahoza na wamiliki wa vyombo vya baharini kuzingatia sheria na masharti waliyopewa.

Hata hivyo, taarifa ambazo Nipashe ilizipata jana jioni, zilieleza kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba abiria na shehena ya bia na chakula cha kuku.

“Boti ilikuwa imesajiliwa na kupewa cheti cha kupakia mzigo, hairuhusiwi kubeba abiria na kutokana na kutumia injini moja na matanga, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika," alisema Kombo.

Alifafanua kuwa boti hiyo ilikuwa na uwezo wa kubeba tani 15.68 za mzigo ikiwa na injini moja ya nyuma lakini akaeleza kusikitishwa na kitendo cha uongozi wa boti hiyo kupakia abiria bila ya kuzingatia usalama wao.

“Taarifa kutoka katika eneo la ajali zimesema boti ilikuwa imepakia masanduku ya bia pamoja na pumba za chakula cha kuku, lakini na abiria walipakiwa kinyume cha masharti ya usajili wa boti yao," alifafanua zaidi Kombo.

Usafiri wa kati ya Pemba na Tanga umekuwa mgumu kutokana na wawekezaji wengi kuimarisha usafiri wa kati ya Pemba, Unguja na Dar es Salaam, uamuzi ambao umewalazimu baadhi ya wananchi wanaosafiriki kutoka Tanga kwenda Zanzibar kutumia majahazi na boti bila ya kuzingatia usalama.

*Imeandikwa na Agnes Michael, TANGA, Mwinyi Sadallah na Rahma Suleiman, ZANZIBAR

Habari Kubwa