Ripoti za ukaguzi CAG ziadabishe halmashauri

11Jul 2017
Mhariri
Nipashe
Ripoti za ukaguzi CAG ziadabishe halmashauri

HATUA aliyoichukua Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, ya kuwasimamisha viongozi sita wa idara mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Lindi kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali, ni ya kuungwa mkono.

Zambi alitangaza kuwasimamisha kazi watumishi hao kwa ajili ya kupisha uchunguzi dhidi yao, baada ya kubainishwa na ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kwa mujibu wa Zambi, baadhi ya mambo yaliyosababisha kuchukuliwa uamuzi huo ni pamoja na madai ya watumishi hao kushindwa kutekeleza ipasavyo majukumu yao na kusababisha utata ambao uliibua hoja mbalimbali kutoka kwa CAG kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.

Waliosimamishwa kazi ni wakuu wa idara za sheria, ukaguzi wa ndani, hazina, mhandisi ujenzi, ushirika na ugavi.

Zambi aliwaambia madiwani kuwa wakuu hao wa idara walishindwa kujibu hoja 36 zilizoibuliwa na CAG yakiwamo madai ya muda mrefu ya Shilingi milioni 669.67, kutokusimamia ipasavyo makusanyo ya mapato zikiwamo Shilingi milioni 127.85 zinazotokana na madeni kutoka vyama mbalimbali vya ununuzi wa mazao wilayani humo.

Mengine yaliyoibuliwa ni utaratibu wa ulipaji wa madeni kwa wakati, upimaji ardhi, ununuzi wa dawa bila kuwa na fomu ya maombi ya kufanya hivyo, kufanya malipo kwa mzabuni bila kumkata kodi ya zuio na kufanya mikataba ya miradi ya ujenzi bila kuwasilishwa kwa mkaguzi.

Ziko hoja nyingi za CAG zilizokosa majibu kutoka kwa viongozi hao wa idara, hali iliyomfanya Zambi kumwagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo kuunda kamati ya kuchunguza tuhuma dhidi ya watumishi hao na watakaobainika kuhusika kwa namna moja au nyingine, wachukuliwe hatua zinazostahili.

Matukio ya aina hii ambayo yanaisababishia serikali hasara yamekuwa ya kawaida, kutokana na kila mwaka kubainishwa na CAG katika ripoti yake ya ukaguzi, lakini ripoti hiyo haijatumiwa ipasavyo na mamlaka kadhaa za maamuzi kwa ajili ya kudhibiti vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma.

Kibaya zaidi ni kuwa matukio haya yameshamiri katika halmashauri zetu, hivyo kuendelea kukwaza jitihada za kuwaletea wananchi wengi maendeleo.

Kinachosikitisha zaidi ni kuona halmashauri zetu zikikosa mapato yake kwa uzembe au hujuma za baadhi ya watendaji huku zikikabiliwa na changamoto ya kutokuwa na vyanzo vya kutosha vya mapato.

Kwa hatua hii, tunampongeza sana Zambi kwa kuchukua hatua hiyo baada ya kubaini jinsi wakuu wa idara wa halmashauri hiyo walivyoshindwa kujibu hoja za CAG baada ya kupata shaka wakati wa ukaguzi wake.

Ni jambo lililo wazi kuwa madudu hayo yapo katika halmashauri nyingi na yamekosa majibu sahihi ya hoja za CAG. Tunawashauri wakuu wote wa mikoa na wilaya kutumia muda wao wa kutosha kusoma ripoti za CAG na kuchukua hatua dhidi ya watendaji wa halmashauri ambazo ukaguzi wa hesabu zao utakuwa na utata.

Watumishi na viongozi wa idara watakaoguswa na tuhuma za kufanya madudu hayo wachunguzwe na kamati na hata Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)na wakibainika wachukuliwe hatua, ikiwamo kufikishwa kortini.

Hili ndilo litakalokuwa sulihisho la matukio ya wizi, ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi ambayo yamekuwa yakijirudia kila uchao katika halmashauri zetu.

Tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu kama kibano kitaelekezwa kwenye wizara, wakala, idara, mashirika na kuziacha halmashauri, ambazo zimekuwa zikiitwa ‘mchwa’ anayetafuna fedha za umma.

Habari Kubwa