Ratiba imetoka, isipanguliwe ovyo

15Jul 2017
Mhariri
Nipashe
Ratiba imetoka, isipanguliwe ovyo

SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF), wiki hii imetoa ratiba kamili ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2017/2018.

Ratiba hii imetoka katika kipindi mwafaka ambapo klabu nyingi zitakazoshiriki ligi hii kuwa kwenye maandalizi kabambe kuhakikisha wanakuwa vizuri pindi ligi itakapoanza Agosti 26.

Maandalizi ya timu hiyo yapo katika sehemu mbili, kwanza timu bado zinaendelea na usajili na pia nyingine tayari zimeanza kambi kujiandaa kikamilifu.

Nipashe tunaipongeza TFF kwa kutoa ratiba ya ligi mapema kwa kuwa tunaamini vilabu vitajiandaa huku vikijua mpinzani wake wa kwanza kukutana naye ni nani.

Tayari timu nyingine zimeshafahamu zitaanzia wapi, nyumbani au ugenini katika harakati za kuwania ubingwa msimu.

Pamoja na TFF kufanya hivyo mapema, Nipashe tunatoa wito kwao kujaribu kuepuka yale matukio ya kupangua pangua ovyo ratiba ambao wameipanga wenyewe.

Tunaamini ratiba hii imezingatia ushiriki wa timu ya Taifa kwenye michuano ya kimataifa pamoja na vilabu vya Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la soka Afrika, (CAF).

Upanguaji wa ratiba kila wakati unapunguza msisimko wa ligi yetu na pia inatoa mwanya kwa timu kupanga matokeo au hata kuweka mazingira ya rushwa.

Yapo mambo ambayo yanaweza yakatokea na kupelekea mabadiliko ya ratiba kulingana na umuhimu wa tukio husika, lakini hatutegemei kuona ratiba ikipanguliwa hata kwa sababu ambazo hazina uzito.

Tunaamini TFF wamepanga ratiba hii kwa kufuata kalenda ya matukio ya CAF pamoja na Shirikisho la soka Duniani, FIFA.

Pamoja na ratiba kutolewa na TFF, lakini kwa vilabu ratiba hii sasa iwape msukumo wa kuhakikisha wanaongeza nguvu kwenye maandalizi yao.

Wadau wa soka tunatarajia kuona ligi yenye ushindani zaidi msimu huu ambayo itafanya Tanzania kumpata bingwa ambaye atakuwa na uwezo wa kupambana na timu za nje kwenye michuano ya Kimataifa.

Ubora wa ligi pamoja na mambo mengine pia unategemea ubora wa timu shiriki, na ubora huo unapatikana kwa kusajili vizuri pamoja na kufanya maandalizi ya nguvu kabla ya kuanza kwa msimu.

Kwa zile zilizopanda daraja msimu huu, Lipuli ya Iringa, Njombe Mji pamoja na Singida United zinapaswa kujiandaa kikamilifu zaidi ili kukwepa kurudi zilipotoka kwa maana ya kushuka daraja.

Timu hizi zitakutana na timu ambazo tayari zinauzoefu wa ligi kuu hivyo jambo pekee la kuwafanya kupambana nazo na kubaki kwenye ligi ni maandalizi ya nguvu pamoja na usajili wenye tija.

Nipashe tuaamini timu hizi zimepanda kuongeza ushindani kwenye ligi na zimejipanga kuona zinafanya vizuri.

Habari Kubwa