Neema ya korosho sasa iende kwa mazao mengine

03Jan 2018
Mhariri
Nipashe
Neema ya korosho sasa iende kwa mazao mengine

NI hakika kuwa zao la korosho mwaka 2017, halikuwa na mpinzani kibei na kibiashara. Kinachozidi kulifanya kuwa zao lenye tija zaidi ni malipo ya Sh. trilioni 1.1 yaliyolipwa kwa wakulima wa mikoa minne maarufu kwa kilimo hicho.

Katika msimu wa kilimo wa 2017/2018 wakulima wa Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma, waliuza kilo 285,828,205 zenye thamani ya Sh. 1,082,200,383,581 katika mnada wa mwisho uliofanyika Desemba 21, 2017 na mingine  inaendelea kwa msimu wa 2017/2018.

 

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho (CBT), Hassan Jarufu, alibainisha hayo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu uzalishaji na mauzo ya zao la korosho nchini hadi kufikia mwisho wa mwaka 2017.

 

Ni habari njema ambazo wakulima wa mazao mengine ya biashara na chakula wangependa kuzisikia zikigusa kile wanachozalisha iwe chai, kahawa, mahindi, vitunguu, pamba, mkonge au karafuu.

 

Kwa korosho utafiti unaofanyika kwenye Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele mkoani Mtwara umeibua mafanikio kwenye mbegu bora zenye ukinzani na magonjwa, ukame na zinazozaa kwa wingi.

 

Jitihada zinazofanyika kwenye korosho zifikishwe kwenye mazao mengine. Mathalani, mahindi kuna mbegu zenye ukinzani na ukame na wadudu waharibifu ambazo pia huzaa sana. Lakini tatizo linakuwa kwenye mbegu na pembejeo kutowafikia wakulima kwa wakati.

 

Aidha, maofisa ugani kukosekana vijijni nayo ni changamoto inayowapata wakulima. Unaweza kushangaa kuwa miche ya mahindi inapotobolewa na wadudu wakulima bado wanajaza mchanga au majivu badala ya kunyunyizia dawa za kuua vivamizi? Wakulima kuendelea kutumia udongo huo kutibu mahindi ni udhihirisho kuwa maofisa ugani hawapatikani ama hawatimizi wajibu.

 

Mwishoni mwa wiki Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alizindua kampeni ya kitaifa ya upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 kwa msimu wa 2017/2018 mjini Ruangwa, mkoani Lindi, wenye kaulimbiu“Korosho ni dhahabu ya kijani, tuitunze, itutunze”.

 

Kama ilivyo kwa korosho ambazo miaka hiyo zilikuwa zinauzwa Sh. 300,500  mpaka 800 kwa kilo safari hii zimefikia Sh. 3,995 kwa kilo. Ongezeko hilo na jitihada hizo ziende pamoja na kuboresha mazao mengine kama mahindi, maharage, viazi mviringo, mpunga na mboga kama ilivyo nyanya na vitunguu.

 

Kuna umuhimu wa kufanyika tafiti zaidi kupata mbegu, ili angalau kila mkoa uwezeshe familia kulima mahindi na mpunga na kujipatia chakula cha kutosha. Lakini pia kujengewa uwezo wa kuyauza kwenye vyama vya ushirika, kuyasindika na kusafirisha unga nje ya nchi kukuza uchumi.

 

 Katika    “Korosho ni dhahabu ya kijani, tuitunze, itutunze” mikoa mingi itahusika kuilima,  hivyo basi mkazo zaidi kwenye mazao mengine ni muhimu ili tija itokane na kilimo cha mazao mengine mengi  ya chakula na ya biashara.

 

Taifa lina taasisi za kilimo za mazao mengi kama Maruku mkoani Kagera, Lyamungo Kilimanjaro, Ukiliguru Mwanza, Mlingano Tanga, Tengeru na Seliani Arusha pamoja na Mikocheni Dar es Salaam zije na mikakati na kuibua mbegu bora na za kisasa za mazao zinayoyatafiti na kuzisambaza kwa wakulima kama ilivyo kwa korosho ambayo sasa imefanyiwa majaribio katika mikoa mingi na huenda ikapandwa nchi nzima.

 

Upandaji wa korosho unahusisha kila kijiji, hivyo tunasisitiza kushauri utaratibu huo uende kwa mazao mengi hasa hayo yenye soko kama mahindi, maharage na vitunguu ambayo katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki  yenye soko la watu zaidi ya milioni 100 ni wazi mkulima wa Tanzania ana fursa ya kubadilisha na kuinua maisha yake na ya taifa.

 

Kutokana na kuona faida na fursa nyingi katika korosho, Waziri Mkuu Majaliwa anawataka vijana wanaioishi kwenye mikoa ambayo zao la korosho linastawi wachangamkie kilimo cha zao hilo.

 

 

 

 

 

Habari Kubwa