Mkakati viwanda kutoa ajira kwa wananchi uwe endelevu

19May 2017
Mhariri
Nipashe
Mkakati viwanda kutoa ajira kwa wananchi uwe endelevu

SERIKALI imesema kwamba ina mpango wa kuongeza nafasi za ajira kwa wananchi, baada ya kusajiri miradi mikubwa zaidi ya viwanda.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, jana alipokuwa akiwasilisha hotuba ya utekelezaji wa bajeti ya wizara yake kwa mwaka huu wa fedha na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka ujao wa fedha 2017/18.

Waziri Mwijage aliliambia Bunge kuwa serikali imesajili miradi ya viwanda vikubwa 393, ambayo vitatoa ajira 38,862 kwa Watanzania.

Kwa mujibu wa Mwijage, tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani Novemba 5, 2015 hadi Machi, mwaka huu, miradi hiyo ya viwanda vikubwa imesajiliwa nchini ikiwa na jumla ya mtaji wa Dola za Kimarekani bilioni 2.363 (Sh. trilioni 5.198).

Alisema miradi hiyo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji na mingine katika hatua za mwisho za kuanza uzalishaji. Kati ya miradi hiyo, Kituo cha Uwekezaji (TIC) kimesajili miradi 224, Mamlaka ya EPZ (41) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) (128) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) limeratibu uanzishwaji wa viwanda vidogo 1,843.

Kwamba viwanda vilivyoanzishwa katika mwaka huu wa fedha ni vya kuzalisha chuma na bidhaa za chuma ambavyo vitatu viko katika Mkoa wa Pwani vya Kiluwa Steel (Mlandizi - ajira 800), Lodhia Steel (Mkuranga - ajira 300) na Lake Steel and Allied Product (Kibaha - ajira 120). Vimo pia vya saruji ambavyo mbali na viwanda 11 vilivyopo nchini, juhudi zimefanyika kupata wawekezaji zaidi katika sekta hiyo.

Waziri Mwijage alitaja orodha ndefu ya miradi ya viwanda ambayo utekelezaji wake umeanza na mingine kuwa mbioni kuanza, hivyo kudhihirisha kwamba mkakati wa Rais John Magufuli wa kuipeleka nchi yetu katika uchumi wa kati kupitia ujenzi wa viwanda unatekelezwa kama ilivyopangwa.

Hatua ya kusajili miradi mingi ya viwanda ni nzuri na inapaswa kuwa endelevu kupitia utaratibu wa kuwahamasisha wawekezaji wa ndani na wa kutoka nje kujitokeza na kujenga viwanda.

Suala la msingi na la kuzingatia ni kwa serikali kuhakikisha kwamba inafanya jitihada za dhati za kuweka mazingira bora na rafiki ya kuwavutia wawekezaji kujenga viwanda.

Mazingira hayo ni pamoja na kuhakikisha miundombinu kama barabara, reli, viwanja vya ndege inaboreshwa zaidi pamoja na kuwapo kwa umeme wa kutosha na wa uhakika.

Pia, kuwapo kwa malighafi za kutosha ni muhimu kwa kuwa kunavipunguzia viwanda gharama za kuziagiza nje pamoja na muda wa kusubiri zifike nchini.

Tunazipongeza hatua za usajili wa miradi zaidi ya viwanda kwa kuamini kuwa zitasaidia kutengeneza fursa za ajira kwa wananchi wetu na kuwaondolea makali ya umaskini kwa kuzingatia kuwa suala la ajira kwa sasa ni changamoto kubwa nchini.

Vijana wengi wanaohitimu katika vyuo vikuu wanabaki mitaani kutokana na uhaba wa ajira ambao pia unachangiwa na uwezo mdogo wa serikali wa kuajiri.

Ujio wa viwanda zaidi unasaidia kuleta ushindani katika viwanda kwa maana ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa bora, kupungua kwa bei ya bidhaa na serikali kupata mapato yake kutokana na kodi.

Nafasi 38,862 za ajira za moja kwa zitakazopatikana kutokana na jumla ya miradi 393 mikubwa ya viwanda iliyosajiliwa, zinaweza kuwanufaisha watu wengine zaidi ya 200,000 ambao ni wategemezi wao.

Kuna watu wengine pia ambao wanapata ajira zisizo za moja kwa moja katika viwanda hivyo, wakiwamo wa kutoa huduma kama mamalishe na wengine, hivyo inatosha kusema kuwa ni mkakati mzuri na unapaswa kuwa endelevu.

Habari Kubwa