Makocha Simba, Yanga  tatizo mfumo wa ajira 

25Dec 2017
Mhariri
Nipashe
Makocha Simba, Yanga  tatizo mfumo wa ajira 

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara na waliokuwa mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho, Simba, juzi ilitolewa katika mbio zake za kutetea ubingwa huo na timu ya maafande ya Green Warriors.

Simba ilitolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia dakika 90 za mchezo kumalizika wakiwa sare ya bao 1-1, hivyo kutemeshwa  rasmi ubingwa wa michuano hiyo.

Kuong'olewa kwa Simba katika michuano hiyo ambayo msimu uliopita ndiyo iliyowapa tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho barani Afrika msimu huu, si tu kumewakera mashabiki na wanachama wa klabu hiyo, bali hata viongozi kwa ujumla.

Na kutokana na kukerwa na kipigo hicho, ambacho sasa kinaifanya Simba kuhakikisha inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ili msimu ujao ipate nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa, kumewafanya viongozi wa klabu hiyo kushushia hasira zao kwa Kocha Mkuu, Joseph Omog, kwa kumtimua kazi.

Ingawa katika mchezo wa soka kumeibuka msemo wa 'makocha wanaajiriwa ili watimuliwe', Nipashe tunaona bado kuna kasoro nyingi katika utaratibu ama mfumo mzima unaotumika hususan kwa klabu kongwe Simba na Yanga katika kuajiri kocha mkuu na wasaidizi wake.

Tumekuwa tunaona kwenye ligi za wenzetu hususan Ulaya, ambapo kocha mkuu anayepewa majukumu ya kuifundisha timu, huachiwa jukumu la kutafuta wasaidizi wake.

Hilo humsaidia kocha mkuu kuwa na wasaidizi wanaoamini katika falsafa moja na mara zote lazima kocha msaidizi aonyesha utii kwa bosi wake kwa kufuata kile anachoagizwa.

Katika kipindi hiki ambacho ligi ilisimama Simba imecheza michezo miwili ya kirafiki chini ya kocha msaidizi Masoud Djuma kufuatia Omog kuwa mapumzikoni kwao Cameroon.

Katika michezo hiyo Simba ilicheza soka safi la kushambulia kwa kutumia mawinga tofauti na wakati timu ikiwa chini ya Omog ambaye alikuwa akiamini katika kujilinda kwa kutumia viungo wengi katikati huku  mashambulizi yakiwa ni ya kushtukiza.

Hata hivyo, baada ya Omog kurejea na kuiongoza Simba katika mechi hiyo ya Kombe la Shrikisho dhidi ya Green Warriors, alirejea mfumo wake wa kujilinda kwa kutumia viungo wengi.

Kwa mtazamo wa haraka tu, hapo unapata picha kuwa Simba ina makocha wawili wakuu wenye falsafa tofauti.Hivyo, kilichokuwa kikiigharimu Simba ni kuwapo kwa makocha wawili wenye falsafa tofauti na kila mmoja akiwa na siri nzito nyuma ya pazia kuhusu ajira yake.

Sisi tunaamini kufukuzwa kwa Omog hakuwezi kuwa suluhisho kwa Simba na hata ikitokea Yanga nayo ikafanya vibaya na kuamua kumfukuza Kocha Mkuu, Mzambia George Lwandamina, hakuwezi kuponya 'gonjwa' hilo sugu lililodumu katika klabu hizo kwa muda mrefu.

Tunalazimika kuijumuisha Yanga katika hilo, kutokana na ukweli kwamba nayo imekuwa na utaratibu kama wa watani zao wa kutimua makocha kila uchao, na hata ukichunguza tatizo lililopo Simba ni kama la mahasimu wao hao.

Hivyo, ni lazima klabu hizi kubwa zibadili mfumo wao wa kuajiri makocha na kumpa fursa kocha mkuu kuja na msaidizi wake ambaye hata akimwachia timu hawezi kuanza kubadili mfumo pasipo maelekezo ya bosi wake.

Kadhalika, kama Simba itaamua kumpa Masoud mikoba ya Omog, basi itoe fursa kwake kutafuta msaidizi wake na si kama inavyodaiwa kuwa atasaidiwa na Selemani Matola. Kama ndivyo labda iwe kocha huyo raia wa Burundi ndiye aliyependekeza hivyo.

Kufanya vibaya kwa Simba tatizo si Omog pekee, bali chanzo ni mfumo mbaya wa namna kocha mkuu anavyopatikana na wasaidizi wake. Tuwaache makocha kuchagua wasaidizi wao ili kuenenda katika falsafa moja.

Habari Kubwa