Mafanikio haya ni ya kujivunia, Hivyo jitihada zaidi ziongezwe

26Nov 2017
Mhariri
Nipashe Jumapili
Mafanikio haya ni ya kujivunia, Hivyo jitihada zaidi ziongezwe

TANZANAIA kwa mara ya kwanza imeandika historia katika tiba baada ya kufanikiwa kupandikiza figo kwa mgonjwa, hivyo kuleta matumaini ya matibabu hayo kufanyika nchini badala ya nje ya nchi kama ilivyozoeleka.

Rekodi hiyo ya kipekee iliwekwa wiki hii katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam kutokana na msichana wa miaka 27 kupandikizwa figo na hali yake imeelezwa kuwa inaendelea vizuri huku akiwa chini ya uangalizi wa madaktari.

Mafanikio hayo katika upandikizaji figo, ambao umekuwa ikifanyika nje ya nchi kwa miaka nenda rudi, yameleta nuru kama ilivyo kwenye matibabu ya moyo kutokana na wagonjwa wengi kutibiwa magonjwa makubwa ya moyo ikiwamo upasuaji kupitia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyoko Muhimbili.

Hatua hiyo ya kupandikiza figo kupitia wataalamu wazalendo kwa kushitrikiana na wenzao kutoka nje, itawezesha wagonjwa wengi kupata huduma hiyo nchini lakini pia kuokoa mamilioni ya shilingi yaliyokuwa yakitumika kusafirisha wagonjwa nje ya nchi.

Akitangaza mafanikio hayo juzi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema kuanzishwa kwa mpango huo wa matibabu nchini, kutaokoa Sh. bilioni 2.8 zilizokuwa zikitumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu kila mwaka.

Waziri Ummy alisema kupitia matibabu hayo nchini, serikali itatumia Sh. milioni 735 takriban chini ya asilimia 25 ya gharama zilizokuwa zikitumika nje kusafirisha wagonjwa wa aina hiyo na badala yake fedha zitakazobaki zitapelekwa kwenye matibabu mengine pamoja na kuimarisha matibabu ya figo katika hospitali za hapa nchini.

Mafanikio hayo ya kupandikiza figo nchini ni makubwa na ya kujivunia kwa nchi kwa sababu yanaiweka sasa Tanzania katika ramani ya dunia hususan kwenye ubora na viwango vya matibabu ya magonjwa makubwa kama moyo na figo.

Pamoja na mafanikio hayo, jukumu kubwa lililo mbele ya wataalamu hao ni kuongeza jitihada zaidi katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa wa figo ili kuongeza sifa zaidi kwa nchi na kupaa katika viwango vya juu kwenye utoaji wa huduma za afya.

Aidha, ili kupunguza matatizo ya maradhi ya figo kwa Watanzania, jambo lingine linalopaswa kufanyika kwenye hospitali ya Muhimbili na nyinginezo ni kutoa elimu juu ya kubadili tabia kwa wananchi ili kujikinga na uwezekani wa kupatwa na ugonjwa huo.

Miongoni mwa mambo ambayo yanapaswa kutolewa katika elimu hiyo ni juu ya jamii kupunguza unywaji pombe kupita kiasi ambao ni kisababishi kikubwa cha maradhi ya figo. Hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa katika mapambano dhidi ya maradhi hayo kwani wahenga walisema kinga ni bora kuliko tiba.

Jitihada na mafanikio yaliyofikiwa katika matibabu hayo yanapaswa kuungwa mkono na wadau wote wa sekta ya afya ikiwamo idara ya tiba ya figo Muhimbili kuwezeshwa zana za kazi na watalaamu kupewa ujuzi zaidi ili kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Habari Kubwa