Madereva waongeze uangalifu barabarani

09May 2017
Mhariri
Nipashe
Madereva waongeze uangalifu barabarani

TAIFA limepata msiba mkubwa wa wanafunzi 33, walimu wawili na dereva wa Shule ya Awali na Msingi ya Lucky Vincent jijini Arusha.

Watu hao wakiwamo wanafunzi wa darasa la saba, walifariki dunia eneo la Malera wilayani Karatu, baada ya basi la shule walilokuwa wakisafiria kutoka shuleni kwao kwa Mrombo jijini Arusha kwenda Shule ya Tumaini Junior ya Mjini Karatu kufanya mtihani wa ujirani mwema, kupata hitilafu ya breki kisha kuserereka na kutumbukia kwenye korongo.

Taarifa zinaeleza kuwa wakati ajali hiyo ikitokea, mvua ilikuwa ikinyesha katika miteremko ya milima eneo la Malera Kata ya Rhotia.

Sababu nyingine inayotajwa kuchangia ajali hiyo ni kuwapo kwa ukungu pamoja na dereva kutokuwa na uelewa wa barabara hiyo.

Ni ajali ambayo imeitikisa nchi yetu kutokana na kupoteza idadi kubwa ya watoto ambao walikuwa tegemeo la nchi katika miaka ya baadaye. Kimsingi, tumepoteza viongozi, wataalamu na nguvu kazi ya baadaye.

Tunaungana na Watanzania wenzetu kutoa pole nyingi kwa familia za watu hao na kuwaomba wawe watulivu na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuwapoteza wapendwa wao. Pia tunatoa pole kwa uongozi, wanafunzi na jumuiya nzima ya shule ya Lucky Vincent kutokana na msiba huo mkubwa.

Watanzania wengi jana walizungumza mambo mengi kuhusiana na msiba huo wakionyesha kusikitishwa pamoja na mambo mengine, kupoteza watoto hao ambao walikuwa tegemeo kubwa kwa nchi katika siku za usoni.

Salamu mbalimbali wakati wa maombolezo ya kitaifa na shughuli ya kuaga miili ya marehemu katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha zilidhihirisha jinsi tukio hilo lilivyoitikisa nchi.

Watu wengi walishauri madereva kuwa waangalifu na kuongeza umakini wawapo barabarani pamoja na kuitaka serikali kuongeza kasi ya kudhibiti ajali za barabarani.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliyemwakilisha Rais John Magufuli kuongoza shughuli hiyo, alisisitiza madereva kuongeza umakini wawapo barabarani.

Makamu wa Rais alisema baadhi ya vyanzo vikuu vinavyochangia ajali za barabarani ni matumizi ya vilevi pamoja na dawa za kulevya. Samia alisema serikali kwa upande wake imekuwa ikichukua hatua kadhaa za kudhibiti ajali za barabarani, ikiwamo ya kuweka alama.

Sisi tunakubaliana kwa asilimia 100 na ushauri wa kuwataka madereva kuongeza uangalifu na umakini wanapokuwa barabarani kwa kuwa wanakuwa na dhamana ya kubeba roho za watu.

Matumizi ya vilevi, kutokufunga mikanda, mwendokasi, madereva wa pikipiki na abiria wao kutovaa kofia ngumu na pamoja na matumizi ya simu dereva akiendesha ni mambo ambayo yamekuwa yakitajwa kuwa vyanzo vikuu vya ajali za barabarani.

Tunaishauri serikali kuongeza umakini katika udhibiti wa ajali kwa kuhakikisha kuwa Jeshi la Polisi linayafanyia ukaguzi wa kina na wa kila wakati magari yote, kwa kuwa ubovu wa magari nao umekuwa ukichangia ajali nyingi.

Janga la ajali ya shule ya Lucky Vincent linapaswa kuwa fundisho kwa Watanzania kwamba madereva wawe waangalifu na makini zaidi kwa kuwa ndivyo vitakavyosaidia kuepusha ajali.

Kadhalika, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani hakinabudi kuongeza elimu kwa umma kuhusu usalama barabarani hususani kwa madereva, badala ya kujikita tu katika kuwatoza faini madereva wanaokwenda kinyuma cha sheria za usalama barabarani.

Habari Kubwa