Kuongeza muda wa chapa ya mifugo uamuzi sahihi

02Jan 2018
Mhariri
Nipashe
Kuongeza muda wa chapa ya mifugo uamuzi sahihi

CHAPA ya mifugo ni suala lililosababisha malalamiko makubwa kutoka kwa wafugaji mbalimbali tangu lilipotolewa agizo hilo na serikali.

Agizo la serikali la kumtaka kila mfugaji kupiga chapa mifugo yake lilitokana na Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo na 12 ya mwaka 2010 na Kanuni zake za Mwaka 2011 GN 362.

Kwa hiyo malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na baadhi ya wafugaji dhidi ya serikali kuwa utekelezaji wa agizo hilo ni kuwanyanyasa na kuwabagua hayakuwa na mashiko kwa kuwa ni agizo halali linalotokana na sheria ya nchi.

Wafugaji wengi walikuwa wakilalamikia agizo hilo na kutaka lisogezwe mbele kutokana na viongozi na watendaji kadhaa kuonekana kushindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu katika suala zima la kusimamia agizo hilo, ambalo lilikuwa limeweka tarehe ya mwisho la kupiga chapa mifugo kuwa Desemba 31, 2017.

Kimsingi, usimamizi wa utekelezaji wa agizo hilo pamoja na kulalamikiwa na wafugaji wengi, lakini pia ulikuwa wa kusuasua kwa kuwa agizo hilo lilitolewa mwaka mmoja uliopita.

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ndiye aliyetoa agizo hilo kwa wizara ya Mifugo na Uvuvi kupiga chapa mifugo yote nchini Desemba 16, 2016 ukiwa ni utekelezaji wa Sheria ya utambuzi,Usajili na ufuatiliaji wa Mifugo na 12 ya mwaka 2010 na Kanuni zake za Mwaka 2011 GN 362.

Hatua ya serikali kuongeza muda wa upigaji chama kuanzia juzi hadi baada ya siku 30 ni ya kupongeza, kwa kuwa imegundua baada ya kujiridhisha kuwa kuna viongozi kadhaa ndani ya wizara husika walishindwa kuwajibika ipasavyo katika kusimamia zoezi hilo, hivyo likasuasua na kuzua malalamiko kutoka kwa wafugaji.

 

Akizungumza juzi katika zoezi la kuhitimisha upigaji chapa kitaifa katika Kata ya Migato Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, aliongeza siku 30 huku akionyesha kutokuridhishwa na usimamizi wa maofisa waandamizi wa wizara hiyo.

 

Alisema kutokana utekelezaji wa  zoezi hilo kutokuwa la kuridhisha kwani asilimia 38.5 ya ng’ombe milioni 19,219,487 waliotakiwa kupigwa chapa ni ng’ombe  milioni 7,401,661 tu ndio waliopigwa chapa tangu Desemba 14, 2016 Waziri Mkuu alipoielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupiga chapa mifugo yote nchini.

Mbali na kuongeza mwezi mmoja, Waziri Mpina pia alitangaza hatua ya kuwavua nyadhifa viongozi kadhaa wa wizara yake kwa kushindwa kusimamia kikamilifu zoezi hilo.

Alisema maofisa hao walishindwa kusimamia kimamilifu zoezi hilo kwa mujibu wa Sheria ya utambuzi,Usajili na ufuatiliaji wa Mifugo na 12 ya mwaka 2010 na Kanuni zake za Mwaka 2011 GN 362. Wamo pia waliopewa onyo kali kwa kushindwa kusimamia zoezi hilo huku waliovuliwa madaraka akiagiza wachukuliwe hatua kali za kinidhamu.

Kutokana na malalamiko mengi kutoka kwa wakulima kuhusiana na suala zima la upigaji chapa mifugo, tunampongeza waziri Mpina kwa kuona umuhimu wa kuongeza muda baada ya kubaini mapungufu yaliyokuwapo.

Aidha, tunampongeza Mpina kwa ufuatiliaji wake katika sekta ya mifugo ambao umewezesha kubaini utendaji mbovu wa watumishi na watendaji wa umma ambao wamekuwa wakiwakwaza wafugaji na shughuli za ufugaji. Ni ufuatiliaji huo wa karibu uliowezesha kubaini waliozembea katika utekelezaji majukumu yao na kusababisha upigaji chapa kukokamilika kwa wakati uliopangwa.

Ni matarajio yetu kuwa wafugaji wote watachangamkia upigaji chapa mifugo yao ili wakamilishe ndani ya mwezi mmoja ulioongezwa ili serikali ifikie malengo yake ikiwamo kupata kodi stahiki itokanayo na mifugo.

 

 

Habari Kubwa