Kukatika umeme itafutiwe dawa isiathiri vitambulisho

28Dec 2017
Mhariri
Nipashe
Kukatika umeme itafutiwe dawa isiathiri vitambulisho

KUKATIKA ovyo kwa umeme kumekuwa kukilalamikiwa sana na wananchi mkoani Mtwara kwamba kunawakwamisha kufanya shughuli zao za maendeleo.

Hali hiyo ilishazungumziwa mara kwa mara na viongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na serikali akiwamo Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, ambaye alisema tatizo la umeme mkoani humo lilisababishwa na uchakavu wa mashine na kuahidi kuwa lingeshughulikiwa na kumalizwa ndani ya siku kadhaa.

 

Licha ya kupita siku kadhaa baada ya Waziri huyo kutoa maelekezo kwa Tanesco kulishughulikia na kulimaliza tatizo hilo kwa kufunga mashine mpya, changamoto hiyo imeendelea katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo na kuathiri shughuli mbalimbali za wananchi, zikiwamo za kujipatia kipato pamoja na huduma mbalimbali.

Kutokana na hali hiyo, ipo haja kwa serikali kulifanyia tathmini ya kina suala la umeme mkoani humo na kupanga mkakati ambao utawezesha kulipatia ufumbuzi wa kudumu, hivyo kuwaondolea wananchi kero na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kujipatia kipato na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

 

Pamoja na kero ya umeme kuathiri sekta kadhaa, lakini huduma ya usajili wa wananchi kwa ajili ya kupewa vitambulisho vya taifa imeathirika na kuzua malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi wa mkoa huo.

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), imethibitisha hilo kwa kueleza kuwa wananchi wamelalamikia umeme kukatika kwa muda mrefu wakati zoezi hilo likiendelea licha ya wananchi wengi kujitokeza kusajiliwa.

Nida imesema kwamba changamoto ya umeme kukatika kwa muda mrefu katika vituo vya usajili, kulisababisha mashine zinazotumika kushindwa kufanya kazi.

Mwananchi mmoja alisema changamoto kubwa ni kukatika kwa umeme, hivyo kusababisha wananchi wasubiri muda mrefu kiasi cha kukatisha tamaa na kuhoji kuwa kwa usajili huo ni zoezi la kiserikali, kwa nini Serikali isisaidie umeme kutokatwa kwenye vituo.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Nida, Rose Mdami, alithibitisha changamoto ya umeme ni kubwa katika vituo vingi vya usajili, ingawa alisema kwa kushirikiana na uongozi wa Wilaya wameshachukua hatua za kutafuta majenereta ili kazi ziendelee kama kawaida.

 

Kuna haja kubwa ya kufanyika maandalizi ya kutosha pale serikali inapopanga kutekeleza mipango muhimu kwa taifa kama ya usajili wa vitambulisho vya taifa na ikiwezekana ziwapo huduma za dharura kama umeme katika maeneo ambayo hakuna umeme wa uhakika.

 

Tunashauri kuwa, kwa kuwa wananchi wanajitokeza kwa hiyari yao kwa wingi katika zoezi hilo muhimu kwa Taifa letu, ni vyema serikali ikachukua hatua za makusudi kuhakikisha umeme unakuwapo ili shughuli ya usajili ifanyika bila usumbufu wowote kwa wananchi na watoa huduma hiyo.

 

Bila ya kuchukuliwa hatua, upo uwezekano wa wananchi kukata tamaa wakaacha kushiriki kwa kuona wanapoteza muda wao vituoni, hivyo zoezi hilo likakwama na kusababisha hasara kubwa kwa taifa ikiwamo ya fedha ya walipakodi na muda.

Pale inaposhindikana kuwapo huduma ya uhakika ya umeme, basi ni vizuri zoezi kama hilo kusitishwa eneo husika kwa ajili ya kufanya maandalizi ili lirejee baada ya maandalizi hayo kukamilika.

 

Ni matumaini yetu kuwa mamlaka zote zinazohusika zitachukua hatua zinazostakili ili zoezi hilo lifanikiwe bila kuendelea kuwasababishia wananchi usumbufu.

 

Aidha, tunaamini kuwa Nida itaendelea kujitahidi kuchukua hatua ili kufanikisha zoezi hilo kama ilivyosema kuwa inaendelea kuharakisha inapata majenereta, ili kuamsha mashine ambazo zimeshindwa kufanya kazi ili wananchi wasisubiri muda mrefu vituoni.

Habari Kubwa