Jitihada zinahitajika haraka kunusuru mradi bomba la gesi

19Apr 2017
Mhariri
Nipashe
Jitihada zinahitajika haraka kunusuru mradi bomba la gesi

MIONGONI mwa mambo yaliyoelezwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2015/16 iliyowasilishwa bungeni mjini hapa Alhamisi, iliyopita udhaifu katika mradi wa bomba la usafirishaji gesi asilia kati ya Mtwara na Dar es Salaam.

CAG, Prof. Mussa Assad, katika ripoti yake alisema matumizi ya bomba hilo yapo chini ya kiwango na wateja wa gesi asilia hulipa bei inayofanana wakati wapo umbali tofauti.

Udhaifu mwingine ni kutokulipwa kwa ankara za mauzo ya gesi asilia kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwenda Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Pia kuwapo kwa kipengele cha mkataba wa mkopo kisichoridhisha na tofauti ya bei ya gesi kwa wauzaji wa gesi kwa Tanesco.

CAG alisema bomba hilo lilijengwa na kampuni ya Maendeleo ya Petroli na Teknolojia China(CPTDC)kwa gharama ya dola za Kimarekani bilioni 1.283 ambapo kati ya hizo, dola za Kimarekani bilioni 1.225 zilipatikana kama mkopo wa masharti nafuu kutoka benki ya Exim ya China.

Kwamba marejesho ya fedha za mkopo huo yalitegemea kupatikana kwenye mauzo ya gesi asilia baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa bomba na kuanza kutumika kibiashara na kuwa katika mapitio ya mkataba wa mikopo amebaini bomba hilo lilijengwa kabla ya kutafuta wateja.

Alisema mapungufu hayo yanaathiri malipo ya mkopo kwa vile mauzo halisi ya gesi asilia yatakuwa chini ya kiwango cha makadirio ya awali cha futi za ujazo milioni 138.8 kwa siku.

Pamoja na hayo, CAG alisema kwa sasa Tanesco ndiyo mteja pekee wa gesi ambapo anatumia wastani wa futi za ujazo milioni 46.61 kwa siku wakati makubaliano yalikuwa ni kutumia futi za ujazo milioni 80 kwa siku.

Kiwango kinachotumiwa na Tanesco cha asilimia 58 ni kidogo na ni hasara kubwa kwa mradi huo kwa kuwa futi za ujazo milioni 33.39 (asilimia 42) haitumiki, hivyo ni hasara kwa kuwa kama ingeuzwa, basi fedha zingepatikana.

Pamoja na kwamba udhaifu huo umesababisha mradi huo kuingiza mapato, lakini uchunguzi wa CAG umesaidia sana kuligundua hilo kwa kuwa taifa lingeendelea kukosa mapato kutokana tu na baadhi ya wahusika kutokujali.

Swali linabaki kuwa ni kwa nini mradi huo uiuzie gesi Tanesco pekee wakati kuna wahitaji wengine ambao wangeweza kuuziwa na kuingiza mapato?

Itakumbukwa kuwa bomba hilo lilijengwa ili kuwezesha usafirishaji wa gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme, viwandani, kupikia majumbani na kwenye magari.

Suluhisho la changamoto hii tunashauri liwe ni kuongeza idadi ya wateja wa gesi asilia na tunakubaliana kwa asilimia 100 na ushauri wa GAC kwamba jitihada zaidi ziongezwe katika kuhakikisha wateja zaidi wa gesi asilia wanapatikana ili mkopo uweze kulipwa kabla ya marekebisho ya ulipaji ambayo yataongeza gharama kubwa kwa serikali.

Tunatarajia kuwa mamlaka husika zitalipitia suala hilo na kufufua makubaliano yenye maslahi kwa taifa. Tunakubaliana na CAG kwa mapendekezo yake ya kushauri TPDC iwasiliane na Tanesco na Wizara ya Nishati na Madini ili wajadiliane ni namna gani mitambo ya uzalishaji umeme ya Tanesco itaweza kumalizika kwa wakati ili bomba la gesi litumike kwa ufanisi na kulipa mkopo wa bomba hilo kutoka benki ya Exim ya China kwa wakati.

Udhaifu uliobainishwa na uchunguzi wa CAG katika mradi wa bomba la kusafirisha gesi unapaswa kuwa funzo la kuwapo umakini katika utekelezaji ili kuepuka kuliingizia hasara taifa.

Habari Kubwa