Jaji Mkuu ameanza majukumu yake vizuri

19Sep 2017
Mhariri
Nipashe
Jaji Mkuu ameanza majukumu yake vizuri

JAJI Mkuu, Prof. Ibrahim Khamis Juma, ameanza utekelezaji wa majukumu yake kwa kusitisha kwa muda likizo kwa majaji kuanzia kati ya Septemba hadi Desemba 15, mwaka huu.

Prof. Juma ambaye aliteuliwa Septemba 10 na kuapishwa Septemba 11, mwaka huu, amechukua uamuzi huo kwa lengo la kutaka majaji wajikite kumaliza mrundikano wa mashauri yaliyoko mahakamani kwa muda mrefu.

Kinachothibitisha kuwa kuna mashauri mengi na ya muda mrefu mahakamani ni takwimu zinaoonyesha kuwa zipo kesi 2,198 ambazo baadhi yake zina umri wa miaka 10.

Jaji Mkuu alieleza uamuzi huo wakati akizungumza na majaji wafawidhi wa kanda zote za Mahakama Kuu nchini jijini Arusha Jumamosi katika mkutano wa kupanga mikakati ya kumaliza mrundikano wa mashauri yenye umri wa kuanzia miaka miwili hadi miaka 10 katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.

Hatua ya Jaji Mkuu ya kusitisha likizo za majaji inaonyesha alivyodhamiria kwa dhati kushughulikia changamoto ya muda mrefu ya mashauri kukaa mahakamani kwa muda mrefu.

Ni changamoto ambayo imekuwa ikiathiri wananchi wengi kwa njia mbalimbali ikiwamo kutumia muda wao mrefu kufuatilia, gharama kubwa na kubwa zaidi ni kucheleweshewa haki.

Kwa hiyo kama Jaji Mkuu ameliona hilo na kuwashawishi majaji wenzake kukubaliana na kusitisha likizo zao kupunguza idadi ya kesi, ni jambo zuri na wanastahili pongezi, kwa kuwa ucheleweshaji wa kesi lilikuwa tatizo linalowakabili na kuwaathiri wananchi wengi hususani maskini.

Jitihada za kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani zilishaanza wakati Jaji Prof. Juma akikaimu nafasi hiyo. Mkutano kama ulioanza Jumamosi hadi jana ulishafanyika na ni mwendelezo wa mkutano Aprili mwaka huu, ambapo majaji walijiwekea mikakati ya kumaliza mrundikano wa mashauri katika Mahakama Kuu.

Kwa kuwa jitihada hizo alizianza kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji Mkuu, ni imani yetu kuwa lengo la mkakati huo litafikiwa na wale wote waliocheleweshewa haki watazipata.

Kunawashauri majaji wote kukubaliana na hatua hiyo kwa ajili ya kumuunga mkono Jaji Mkuu katika kushughulikia kero za wananchi, ingawa pia tunatambua na kuthamini kuwa likizo ya mwaka ni haki yao ya msingi.

Umuhimu wa kupunguza mashauri pamoja na kuyashughulikia kwa wakati mashauri mapya ni la msingi. Ndiyo maana hata Rais Magufuli katika hotuba yake fupi baada ya kumwapisha Jaji Mkuu, alimpatia changamoto ya kupunguza mashauri mahakamani hususani yanayowahusu wananchi wa kawaida.

Bila shaka baada ya majaji kusitisha likizo zao sasa kazi ya kushughulikia mashauri hayo itakuwa imeanza kwa kasi huku tukiamini kuwa bajeti ya kuwawezesha kutekeleza jukumu hilo ipo.

Tunafarijika na kutiwa moyo kusikia watumishi wa mahakama wakihimizwa na Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi kuhusu umuhimu wa matumizi ya Tehama, ambao tunaamini utasaidia katika kutekeleza jukumu hilo kwa tija na ufanisi kwa kuwa mahakama itakuwa imehama kutoka kwenye matumizi ya karatasi.

Tunaamini idadi ya mashauri hayo yaliyoko mahakamani tangu mwaka 2002 itapungua kama majaji wote watatumika katika utekelezaji wa mkakati huo ukiacha watakaokuwa wagonjwa au kufikwa na dharura nyingine.

Tunashauri na kuwahimiza wananchi wote wenye mashauri mahakamani kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu utaratibu utakaowekwa na mahakama katika kushughulikia mashauri hayo, ili wajitokeze na kesi ziamuliwe.

Wasikubali kupoteza fursa hii adimu, ili kuondokana na dhama ya kisheria kuwa haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa.

Habari Kubwa