Hongera Taifa Stars, imalizeni na Rwanda

10Jul 2017
Mhariri
Nipashe
Hongera Taifa Stars, imalizeni na Rwanda

TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', imerejea nchini usiku wa kuamkia jana ikitokea Afrika Kusini kushiriki michuano ya Kombe la Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa) kama wageni waalikwa wa michuano hiyo.

Tofauti na miaka mingine ya nyuma ambapo Taifa Stars imekuwa ikienda kushiriki tu michuano ya kimataifa na kurejea mikono mitupu, safari hii imerudi na kitu mkononi.

Tunasema imerudi na kitu mkononi kutoka na kumaliza michuano hiyo kwa kushika nafasi ya tatu na kuwa miongoni mwa timu nne zilizofanikiwa kutwaa zawadi kutoka kwa waandaaji wa mashindano hayo.

Timu hiyo inayonolewa na kocha mzawa, Salum Mayanga, imezawadiwa kiasi cha Dola za Marekani 10,000 ambazo ni zaidi ya Sh. milioni 22.

Nipashe tunawapongeza wachezaji pamoja na benchi zima la ufundi kwa mafanikio waliyoyapata kwenye michuano hiyo iliyomalizika jana nchini Afrika Kusini.

Kama alivyonukuliwa kocha Mayanga akisema haikuwa kazi rahisi kwa timu yake kufikia hatua hiyo, na sisi tunaamini hivyo, kutokana na namna vijana hao walivyopambana kwa uwezo wao na kufanikiwa kuzishangaza timu nyingine ambazo ndizo zenye michuano hiyo zikiwamo Afrika Kusini, Angola na Malawi.

Lakini pia Taifa Stars bado inakabiliwa na michezo mingine ya kimataifa ya kusaka nafasi ya kushiriki katika michuano ya Afrika kwa Wachezaji Wanaocheza Ligi za Ndani (Chan).

Nipashe tunaamini ushiriki wa Taifa Stars kwenye michuano ya Cosafa, na nafasi ya tatu waliyoishika ni chachu kwa vijana wetu kuibuka na ushindi kwenye mchezo wao wa Julai 15, mwaka huu wa kuwania kufuzu michuano ya CHAN dhidi ya Rwanda.

Tunaamini kocha Mayanga ameona upungufu na udhaifu katika kikosi chake wakati wakishiriki michuano ya Cosafa, hivyo katika siku hizi chache zilizobaki kabla ya mechi hiyo ataafanya marekebisho na kukiandaa vema.

Haitafurahisha kwa wadau wa soka, mashabiki na Watanzania wengine kuona timu hii iliyotoka kufanya vizuri kwenye michuano ya Cosafa ikipoteza mchezo wa nyumbani dhidi ya Rwanda.

Sisi tukiwa kama wadau namba moja wa soka tunaimani kubwa na Taifa Stars, na tunaamini inaweza kuibuka na ushindi kama tu itajipanga na kuingia uwanjani kwa nia moja tu ya kushinda.

Kama ni maandalizi ya kina, tunaamini wameyapata katika ushiriki wao kwenye michuano ya Cosafa ambayo imemalizika wiki moja tu kabla ya mchezo dhidi ya Rwanda.

Hivyo Mayanga hatokuwa na kazi kubwa ya kufanya katika maandalizi haya ya wiki moja kabla ya kuelekea kwenye mchezo huu wa kuwania tiketi ya kushiriki Chan.

Nipashe tunaitakia kila la heri Taifa Stars kuelekea kwenye mchezo dhidi ya Rwanda na tunaamini ina lengo na uwezo wa kufanya vizuri.

Habari Kubwa