Hongera Ajibu, jifunze kwa waliofanikiwa

02Jan 2017
Mhariri
Nipashe
Hongera Ajibu, jifunze kwa waliofanikiwa

INAELEZWA kuwa mshambuliaji wa Simba na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Ibrahim Ajibu amefuzu majaribio yake ya kucheza soka la kulipwa kwenye klabu ya Haras El Hodoud inayoshiriki ligi daraja la pili nchini Misri.

Taarifa zinasema kwa sasa imebaki klabu husika, Simba na El Hodoud kumalizana ili Ajibu akacheze soka la kulipwa Misri.

Kwanza Nipashe inampongeza mchezaji husika kwa hatua aliyofikia lakini pia inaipongeza klabu ya Simba kwa kuendeleza utaratibu wa kuwaruhusu wachezaji wake kujaribu bahati ya kucheza soka nje ya Tanzania.

Wachezaji wanaocheza soka la kulipwa au walioonja radha ya soka la nje ya Tanzania wengi wao wametoka Simba, miongoni mwao yumo Haruna Moshi ‘Boban’ ambaye alipata bahati ya kwenda Sweden, Henry Joseph aliwahi kucheza soka Norway, Mussa Hassan ‘Mgosi’ aliwahi kucheza sokaJamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kwenye orodha hiyo fupi, yupo pia nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta, ambaye alitokea Simba na kwenda kucheza soka kwenye klabu ya TP Mazembe kabla ya kuuzwa kwenda Genk ya Ubelgiji anayochezea mpaka sasa.

Ni jambo jema kwa Simba na pia ni mfano wa kuigwa kwa klabu za hapa nchini kuwapa nafasi wachezaji wao kwenda kujaribu bahati yao nje ya nchi pindi wanapopata nafasi ya kufanya hivyo.

Lakini pamoja na hayo, wapo wachezaji waliopata nafasi ya kwenda nje, lakini wakashindwa kudumu kwenye nchi hizo kwa sababu mbalimbali.

Wapo ambao taifa lilikuwa likiwategemea na pengine wangekuwa mfano kwa wachezaji wangine kufuata nyayo zao, lakini waliishia njiani huku wengine sababu zao za kurudi nchini zikiwa hazifahamiki mpaka sasa.

Nipashe inamkumbusha Ajibu, nafasi kama hizi haziwezi kuja mara mbili, ni vyema akaitumia vizuri kwa kuhakikisha anazidi kusonga mbele badala ya kutorudi nyuma.

Sio mbaya tukamtolea mfano kwa Samatta, ambaye tangu ameondoka Simba mwaka 2011 ajawahi kurudi nyuma na kwa sasa amefika sehemu anacheza ligi ya Europa.

Kamwe Ajibu asijifunze kwa walioshindwa, bali aangalie waliofanikiwa wamefanya nini au wamewezaje kufikia walipofika.

Baadhi ya vitu ambavyo Ajibu anapaswa kuzingatia atakapoenda kuanza maisha mapya Misri kama klabu hizo mbili zitakubaliana, ni kujituma na nidhamu.

Kwenye nchi zilizoendelea kisoka kama Misri hakuna ubabaishaji kama ulivyo nchini, hakuna kutegea mazoezi na wala hawamvumilii mchezaji asiyekuwa na nidhamu.

Hatutegemei kuona Ajibu akirejea kwenye ligi ya nyumbani baada ya muda mfupi, kurudi nyumbani kwa mchezaji ambaye tayari alikuwa amepiga hatua moja mbele ni dalili za kushindwa soka la nje ya Tanzania.

Leo hii licha ya Samatta kucheza soka Ubelgiji, bado anawazo la kwenda mbele zaidi kucheza soka kwenye ligi za juu zaidi kama Uingereza, Ujerumani , Italia au Hispania, kamwe kwa sasa hafikirii kurejea kwenye ligi ya Tanzania bara.

Hivyo ndivyo Ajibu anatakiwa kuwa ili kuongeza idadi ya wachezaji waTanzania wanaocheza soka nje ya nchi.

Kwa kuwa na idadai kubwa ya wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania itasaidia pia kuinua kiwango cha soka letu kama ilivyo kwa nchi za Afrika Magharibi au Afrika Kaskazini.

Tunatumia fursa hii kumpongeza Ajibu kwa kufuzu majaribio yake na kumtakia kila la heri mambo yatakapokamilika na kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Misri kwenye klabu hiyo ya Haras El Hodoud.

Habari Kubwa