Hatua zaidi zichukuliwe kudhibiti ajali bodaboda

12Apr 2017
Mhariri
Nipashe
Hatua zaidi zichukuliwe kudhibiti ajali bodaboda

USAFIRI wa pikipiki maarufu kama bodaboda umekuwa ukitajwa kuwa unachangia ajali nyingi za barabarani zinazosababisha vifo na majeruhi.

Ajali hizo zimekuwa zikiongezeka kwa kasi kutokana na usafiri huo kuwa tegemeo kubwa la watu katika maeneo ya mijini na vijijini. Wanaoathirika kwa ajali hizo ni madereva na abiria.

Ongezeko la ajali za bodaboda limekuwa ni changamoto kubwa na mara kadhaa serikali imekuwa ikiwataka vijana waliojiajiri katika usafirishaji wa bodaboda kuzingatia sheria za barabarani.

Juzi serikali ilitoa takwimu za takribani miaka saba ikieleza kuwa kwa kipindi cha Januari 2010 hadi Februari mwaka huu watu 6,529 walikufa kutokana na jumla ya ajali 31,928 za bodaboda. Ajali hizo pia ziliacha majeruhi 30,661.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, alitoa takwimu hizo bungeni alipokuwa akijibu swali la mbunge aliyetaka kujua ni watu wangapi waliopoteza maisha na wangapi walijeruhiwa na ajali za pikipiki kuanzia 2010 hadi mwaka huu.

Mwigulu alisema pikipiki za matairi mawili (bodaboda) na matairi matatu (bajaji) zilianza kutumika kubeba abiria kuanzia mwaka 2008.

Alisema mwaka 2010 serikali ilipitisha kanuni na masharti ya usafirishaji wa pikipiki kwa kuwa wakati ule hakukuwa na utaratibu wowote wa kusimamia biashara ya waendesha pikipiki wanaobeba watu.

Kuhusu mkakati wa kupunguza ajali hizo, Mwigulu aliliambia Bunge kuwa serikali inaendelea kutoa elimu kwa kila mkoa na wilaya kwa idara inayoshughulikia usafiri ili waache kuendesha bodaboda kwa mwendo kasi.

Aidha alisema ajali nyingi za pikipiki husababishwa na waendeshaji wake kutozingatia sheria za usalama barabarani.

Takwimu alizozitaja Mwigulu zinatisha na zinabainisha dhahiri kwamba usafiri wa bodaboda hatari kwa maisha ya Watanzania. Tafsiri yake ni kwamba takribani watu 1,000 wanakufa kila mwaka kutokana na ajali za bodaboda.

Kumekuwapo na jitihada kadhaa ambazo zimekuwa zikifanywa na serikali kudhibiti ajali hizo, lakini hazijasaidia sana kutokana na idadi kubwa ya watu kuendelea kuteketea.

Miongoni mwa hatua hizo zinazotekelezwa na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani ni kuwabana madereva wa bodaboda na abiria wao kuvaa kofia ngumu, kutoa elimu kupitia vyombo vya habari, kuendesha semina za mafunzo na kupeleka askari kutoa elimu kwa waendesha bobaboda katika maeneo wanayofanyia kazi.

Aidha, Jeshi la Polisi limekuwa likizikagua bodaboda kuhakikisha zinazotoa huduma kwa wasafiri ziko katika hali ya usalama.

Hata hivyo, kutokana na takwimu hizi kuonyesha kuwa usafiri wa bodaboda bado ni tishio kwa watu, sisi tunaona kwamba kuna haja kubwa kwa serikali na wadau kuchukua hatua zaidi zitakazosaidia kupunguza janga hili la Taifa.

Ni janga la Taifa kwa sababu watu wanaopoteza maisha yao hususani madereva wa bodaboda ni vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa. Itiliwe maanani pia kwamba bodaboda zinachangia umaskini katika familia kutokana na watu kupata ajali na kupata ulemavu wa maisha, hivyo wanaiowategemea kukosa huduma.

Hilo linathibitishwa na takwimu za Waziri Mwigulu kuwa katika kipindi hicho cha Januari 2010 hadi Februari mwaka huu ajali 31,928 zilijeruhi watu 30,661.

Miongoni mwa hatua tunazoshauri zichukuliwe ni kutungwa kwa sheria itakayowalazimisha waendesha bodaboda wote kuhudhuria mafunzo katika vyuo vya Mamlaka ya Ufundi Stadi (Veta)na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ili wawe na uelewa wa kutosha wa sheria, taratibu na kanuni za usalama barabarani kabla ya kupewa leseni.

Habari Kubwa