Hatua kudhibiti ugonjwa wa himofilia zifanyike haraka

20Apr 2017
Mhariri
Nipashe
Hatua kudhibiti ugonjwa wa himofilia zifanyike haraka

KUNA taarifa za kuwapo nchini kwa ugonjwa mpya wa himofilia huku wataalamu wa afya wakisema kuwa idadi kubwa ya Watanzania wanaugua ugonjwa huo.

Wataalamu hao wamebainisha kuwa Watanzania wapatao 5,400 na kwamba wanaojulikana na kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni 100 pekee.

Himofilia unaelezewa kuwa ni ugonjwa wa damu kukosa uwezo wa kuganda pale mtu anapopata jeraha, kwa kukosa kiwango cha kutosha cha chembechembe za protini zinazotakiwa kugandisha damu na kusababisha damu kuvuja kwa muda mrefu.

Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Damu wa Muhimbili, Dk. Stella Rwezaura, jijini Dar es Salaam juzi kuwa ugonjwa huo uliogundulika mwaka 2009.
Kwa mujibu wa Dk. Rwezaura, takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa katika kila Watanzania 10,000, mmoja anaugua ugonjwa huo ambao kwa asilimia 70 unatokana na kurithi kutoka kwenye vinasaba vya kike na asilimia 30 kwa mabadiliko ya vinasaba.

Kwamba Watanzania wengi hupeleka watoto wao kwenda jando bila kuwapima kama wana ugonjwa wa himofilia au la, na wapo wanaopoteza maisha kwa sababu hiyo, hivyo ni muhimu kuwapima hata kabla ya upasuaji. Tiba huanza kutolewa tangu mtoto anapokuwa na umri wa miaka mitatu na hufundishwa kujichoma sindano maalumu za dawa hizo anapofikisha umri wa miaka nane.

Aina tatu za himofilia zimetajwa kuwa ni himofilia A inayowapata wengi kwa kukosa chembechembe za kugandisha damu au ‘factor’ namba nane na himofilia B ambayo huwapata wagonjwa wachache wenye upungufu wa chembechembe namba tisa na wenye himofilia A na B ambayo mgonjwa huvuja damu kwa muda mrefu kuliko kawaida.

Mgonjwa anaweza kupoteza maisha kwa kuvuja damu nyingi bila matibabu kwa kuwa hakuna chembechembe za kuzuia damu kutoka na kwamba viunganishi vya mwili na wakati mwingine huvimba kutokana na damu kuvujia ndani na baadaye kusababisha ulemavu. Himofilia mbaya zaidi inatajwa kuwa ni ile ambayo damu huvujia kwenye ubongo kwa kuwa ni nadra mgonjwa kupona.

Ni ugonjwa hatari kwa binadamu, ingawa haufahamiki kwa watu wengi licha ya idadi kubwa ya waliougua ugonjwa huo nchini. Udhaifu huu unadhihirishwa na Dk. Rwezaura kwamba wahudumu wengi wa afya hawana uelewa wake.

Changamoto nyingine ni kuwapo na uhaba wa madaktari bingwa wa damu, kutokana na takwimu za mtaalamu huyo kuwa kwa sasa wapo 10 pekee nchi nzima pamoja na taarifa kwamba unatibiwa na Muhimbili tu wakati KCMC na Bugando zinatoa vipimo vya awali.

Vile vile, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za 2008 zinaonyesha tishio kutokana na vifo vya watu milioni 36 duniani vilivyotokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ukiwamo ugonjwa huo na takwimu za Shirika la Himofilia Duniani (WHF) kuwa watu 400,000 wanaishi na himofilia duniani.

Tunaishauri serikali kuchukua hatua za haraka za kukabiliana na ugonjwa huo, hususani kuelimisha umma kuhusu uwapo wake, athari zake na hatua za kujiepusha nao. Serikali isikae kimya wala kuwa mlalamikaji kuhusu ugonjwa huo, bali ichukue hatua hizo.

Tunasema hivyo kwa kuwa katika hotuba yake juzi iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasiyoambukiza, Prof. Magimba, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, hakueleza hatua zinazochukuliwa na serikali kukabiliana himofilia badala yake alisema serikali inatambua kuwa ugonjwa huo ni mkongwe kama maeneo mengine duniani, lakini jamii haina ufahamu wa kutosha na kwamba wengi wa wataalamu wa tiba nao hawana ufahamu wa kutosha pia.

Habari Kubwa