Faini ya 300,000/- sahihi kwa wanaopandisha nauli

27Dec 2017
Mhariri
Nipashe
Faini ya 300,000/- sahihi kwa wanaopandisha nauli

VITENDO vya upandishaji holela wa nauli za mabasi ya mikoani vimeendelea kusababisha kero, taabu na usumbufu mkubwa kwa abiria katika kipindi cha sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Upandiishaji wa nauli sasa imekuwa tabia ya kila mwaka kinapofika kipindi cha sikukuu hizo.

 

Wanaofanya hivyo ni mawakala wa mabasi waliojazana katika stendi za mabasi nchi nzima ambao wanashirikiana na wafanyakazi wa mabasi hayo yaani madereva na makondakta.

 

Hata hivyo, tunapolizungumzia suala hili ambalo ni changamoto kubwa kwa jamii, hatunabudi pia kuwatupia lawama wamiliki wa mabasi hayo.

 

Bila kuwalalamikia wamiliki tutakuwa tunakwepa kulizungumzia tatizo hili kwa uhalisia wake na tutakuwa tunawalinda, hivyo ufumbuzi wake kutokupatikana.

 

Kimsingi, mmiliki wa basi ndiye mwenye wajibu na jukumu la kufanya maamuzi yote kuhusu uendeshaji na usimamizi wa kampuni yake ya usafirishaji.

 

Kwa kusema hivyo tunamaanisha kuwa hakuna jambo lolote linaloweza kufanyika bila mmiliki wa basi asijue, likiwamo suala zima la upandishaji wa kauli usiozingatia sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa na kusimamiwa na mamlaka mbalimbali za serikali.

 

Mmiliki wa basi ni jukumu lake kila mwisho wa siku kufuatilia na kujua kiasi cha fedha alizozipata iwe hasara au faida. Pale basi lake linapokamatwa na kwa kukiuka sheria na kutozwa faini, lazima apewe taarifa na wafanyakazi wa basi husika.

 

Mifano hii michache inadhihirisha ni jinsi gani wamiliki wa mabasi hawapaswi kuachwa kando dhidi ya malalamiko ya mabasi kupandisha nauli kiholela na kinyume cha sheria kila Desemba wakati wa sikukuu hizo.

Kutokana na hali hiyo pamoja na matukio ya matatizo ya usafiri ukiwamo upandishaji wa nauli kwa mabasi ya mikoani kuanzia wiki iliyopita, wamiliki wa mabasi hawanabudi kubeba lawama hizo na siyo mawakala, makondakta na madereva.

Ni jambo la dhahiri kuwa wamiliki wa mabasi nao wanakuwa na mgawo wao wa fedha zinazopatikana kwenye nchezo mchafu wa kupandisha kauli hizo kwa kushirikiana na mawakala na wafanyakazi wao.

 

Kutokana na hali hiyo, tunashauri kwamba ili kukomesha tabia hiyo ya kuwaibia wananchi, gari lolote litakalobainika limepandisha nauli ninyume cha nauli halali iliyopangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), adhabu ya faini itolewe sambamba na kifungo kwa mmiliki.

 

Kumhukumu kifungo wakala, dereva au kondakta hakuwezi kusaidia kumaliza tatizo hilo, bali mmiliki akienda jela litakuwa funzo kwa wamiliki wote wa mabasi kutekeleza wajibu na majukumu yao kama inavyostahili, ikiwamo kuhakikisha hakuna upandishaji ovyo wa nauli.

Hilo linawezekana kabisa kwa kuwa sheria zipo, isipokuwa hazitekelezwi ipasavyo, hivyo kuwapa wakaidi kiburi na jeuri ya kufanya watakavyo.

 

Wakati wa kilio cha upandishaji kiholela wiki iliyopita, Sumatra mkoani Tanga ilitoa kauli ikiwataka wamiliki wa magari ya abiria mkoani humo kutotumia sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kama kipindi cha kujinufaisha kwa kupandisha nauli.

Mamlaka hiyo ilionya kuwa yeyote atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kutozwa faini ya Sh. 300,000 au kufungwa mwaka mmoja jela.

 

Ofisa Mkuu wa Sumatra Mkoa wa Tanga, Dk. Walukani Luhamba, alisema watawadhibiti kwa kuwachukulia hatua ya kuwafikisha mahakamani wahudumu wa mabasi watakaobainika kutoza wananchi viwango vikubwa vya nauli wakati wa sikukuu kinyume cha maelekezo ya serikali.

Tunaamini kuwa kama wamiliki nao watabanwa, hatua hiyo itakuwa mwarobaini wa tatizo hilo linalosababishwa na tamaa ya fedha ya watu wachache.

 

Habari Kubwa