Bravo serikali utekelezaji katazo la mifuko ya plastiki

23May 2019
Mhariri
Nipashe
Bravo serikali utekelezaji katazo la mifuko ya plastiki

UTEKELEZAJI wa katazo la serikali dhidi ya matumizi ya mifuko ya plastiki, kwa lengo la kudhibiti uharibifu wa mazingira ulikuwa umeibua wasiwasi na hofu kubwa katika jamii.

Makundi ambayo yalikuwa yameingiwa na hofu kubwa kwamba yangeathirika zaidi ni watumiaji na wauzaji wa mifuko hiyo; kwamba wangekutana na bughudha ikiwamo vipigo kutoka kwa watendaji na mgambo.

 

Serikali ilishatangaza kwamba mwisho wa matumizi ya mifuko hiyo ni Juni mosi mwaka huu, na kutangaza kanuni ambazo zinaainisha adhabu zikiwamo faini kwa watakaokiuka katazo hilo kwa kuiagiza kutoka nje, kuisafirisha, kuiuza na kuitumia.

Licha ya kuwapo hofu ya kibano hicho, pia kulikuwapo na wasiwasi kuhusiana na upatikanaji wa mifuko mbadala. Hata hivyo, serikali imekuwa ikisisitiza kwamba tayari mifumo mbadala mbalimbali itakuwapo na itapatikana kwa urahisi.

Hata hivyo, jana serikali ilitoa maelezo yenye ufafanuzi wa kina kuhusu utekelezaji wa katazo hilo utakavyokuwa, huku ikiwatoa wasiwasi wananchi kuwa hakutakuwapo na matumizi ya nguvu kama walivyokuwa wakihofia.

 

Kimsingi, maelezo yaliyotolewa na viongozi wa serikali wenye dhamana jana yameondoa hofu na wasiwasi uliokuwapo katika jamii kuhusiana na  utekelezaji wa katazo hilo.

Serikali  iliwataka watendaji na watumishi wa mkoa wa Dar es Salaam, kutotumia nguvu kuwapiga virungu wananchi watakaokutwa na mifuko ya plastiki kuanzia Juni Mosi, mwaka huu.

Aidha, amepiga marufuku watendaji watakaosimamia kazi hiyo kutoingia kwenye maduka, ofisi na kwenye magari ya watu kutafuta mizigo ya mifuko ya plastiki.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira), January Makamba, ndiye aliyetoa  angalizo hilo jana, wakati akizungumza na watendaji wa mkoa wa Dar es Salaam, wakiwamo wakuu wa wilaya, makatibu tawala, wakurugenzi, madiwani, wenyeviti na watendaji wa kata na mitaa, wasimamizi wa masoko, maofisa afya, mazingira na biashara kujadili utekelezaji wa marufuku ya mifuko ya plastiki.

 

Makamba alisema kuwa katika utekelezaji wa sheria hiyo mpya inayoanza, serikali hatutegemei kuona watu wanaendelea kubeba mifuko.

 

Makamba aliongeza kuwa pia hategemei kuona kinamama wanapigwa virungu na mgambo kisa wamebeba mifuko na wala haitegemei kuona watu kuporwa mali zao.

Alieleza katika utekelezaji wa sheria hiyo, watendaji watakaosimamia kazi hiyo hawapaswi kuingia kwenye ofisi, maduka na kufungua magari ya watu kutafuta mizigo ya mifuko ya plastiki.

Alisema katika utekelezaji wa jambo hilo, mwananchi ambaye atakutwa amebeba au mfanyabiashara anayeuza mifuko ya plastiki ndiye atawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

 

Hatua ya serikali kutoa ufafanuzi huo ni ya kupongeza kwa kuwa sasa wananchi hawatakuwa tena na hofu ya kubughudhiwa, na kwa kuzingatia kuwa mpango huo utaenda sambamba na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu udhibiti wa matumizi ya mifuko hiyo.

 

Ushauri wetu ni kuwa watendaji wazingatie maelekezo hayo ili kuondoa uwezekano wa kusababisha usumbufu usio wa lazima, kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia utekelezaji wa baadhi ya operesheni hususan mgambo wanapokuwa wakisimamia usafi katika maeneo ya miji.

 

Ni matarajio yetu kuwa mamlaka husika kama Ofisi ya Makamu wa Makamu wa Rais (Mazingira), Tamisemi na Baraza la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (Nemc) zitafuatilia kwa ukaribu kuhakikisha hakuna mkanganyiko wala uonevu kwa wananchi.

Habari Kubwa