Agizo la udhibiti fedha za kigeni litekelezwe kwa maendeleo ya nchi 

31Dec 2017
Mhariri
Nipashe Jumapili
Agizo la udhibiti fedha za kigeni litekelezwe kwa maendeleo ya nchi 

HATIMAYE serikali imekata mzizi wa fitina juu ya kilio cha muda mrefu cha matumizi ya fedha za kigeni, hususan dola ya Kimarekani, katika ununuzi wa huduma na bidhaa kwenye soko la ndani baada ya kupiga marufuku kuanzia kesho. 

Kwa miaka mingi kumekuwa na kilio cha matumizi ya dola katika ununuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali kwenye soko la ndani kama vile kwenye maduka, hoteli,  ving’amuzi na ada za masoko kwenye baadhi ya shule na vyuo. 

Hata baadhi ya wabunge katika mjadala wa bajeti ya serikali mwaka 2006, waliwahi kuhoji juu ya matumizi hayo ikiwamo katika upangishaji nyuma mijini hususan Dar es Salaam, huku aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, akiahidi kulifuatilia na kuahidi serikali kutoa tamko.

Baada ya kilio hicho cha muda mrefu, hatimaye serikali imekunjua makucha yake kwa kupiga marufuku matumizi ya sarafu za kigeni kwenye miamala mbalimbali ikiwamo huduma katika baadhi ya hoteli. Licha ya kupiga marufuku, serikali imesema wale watakaokiuka agizo hilo, watachukuliwa hatua kali za kisheria. 

Akitoa tamko hilo juzi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisisitiza kuwa kuanzia Januari, Mosi (kesho), ni marufuku kwa mkazi yeyote wa Tanzania kulazimishwa kulipia bidhaa au huduma yoyote nchini kwa fedha za kigeni ikiwamo dola ya Marekani. 

Licha ya kupiga marufuku hiyo, Waziri Mpango aliagiza Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka agizo hilo halali la serikali.

Kwa hakika hilo limedhihirisha kuwa serikali imedhamiria kusimamia sheria, kanuni na taratibu juu ya udhibiti wa matumizi ya fedha ikiwamo utakatishaji fedha.

Kadhalika suala hilo lilikuwa kero miongoni mwa baadhi ya wananchi kwa kuwa walikuwa wakilazimika kubadilisha fedha na hata kupata hasara, kulingana na hali ya soko la fedha.

Kutokana na uamuzi uliofikiwa, serikali inapaswa kupongezwa kwa sababu hatua hiyo haikuwa na athari kwa wananchi pekee bali hata kwa uchumi wa nchi kwa sababu ilikuwa ikidhoofisha sarafu ya nchi dhidi ya zile za nje.

Pia sarafu ya Tanzania (Shilingi) ilifikia hatua ya kudharauliwa hata baadhi ya watu, wakiwamo viongozi waandamizi serikalini, walidiriki kuita ‘fedha za madafu’. 

Kwa ujumla, suala hilo , kwa watu ambao wametembea katika nchi mbalimbali walikuwa wakiona ni la ajabu kwa sababu hakuna nchi ambayo inaruhusu matumizi ya sarafu tofauti na zile za nchi husika katika miamala mbalimbali.

Nchini Msumbuji kwa mfano, hakuna mtu anayeruhusiwa kutumia sarafu nyingine zaidi ya nchi hiyo (Meticais) katika miamala yoyote ile. Mtu kutoka nje ya nchi anapotaka kufanya muamala wowote, akionyesha sarafu ya nje anaambiwa aende kwenye duka la kubadilishia fedha ili apate fedha za nchi hiyo kwa matumizi mbalimbali. 

Ni imani kwamba utekelezaji wa agizo hilo utasaidia kudhibiti pia matumizi holela ya fedha za kigeni ambayo pia huchangia utakatishaji wa fedha haramu. Pia hatua hiyo itasaidia kuimarika kwa Shilingi ya Kitanzania ambayo imekuwa ikiyumba mara kwa mara na hatimaye kuathiri uchumi wa nchi.

Kwa upande mmoja, serikali imeshatoa msimamo wake hivyo kinachotakiwa ni utekelezaji wa agizo hilo.       

Habari Kubwa