WITO WA KAMPENI WAITIKIWA Uongozi masoko Dar watekwa na kinamama

21Apr 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
WITO WA KAMPENI WAITIKIWA Uongozi masoko Dar watekwa na kinamama
  • “Wanufaikaji wa “Mpe Riziki si Matusi” kwa mkoa wa Dar es Salaam ni wilaya mbili za Ilala na Temeke. Siku chache zilizopita, shirika hilo lilifanya ziara maalum katika masoko ya Mchikichini, Kisutu, na Tabata Muslim (Ilala) na Gezaulole’

HIVI sasa ni msimu unaoelekeza dhana kuu katika kinachoitwa “Macho yote kwa kinamama,” kutokana na idadi kubwa ya wanaharakati wanaelekeza nguvu katika kupigania haki za wanawake.

Aisha Juma.

Miongoni mwa haki hizo, ni pamoja na uwepo wa nafasi sawa za uongozi katika jamii na ngazi mbalimbali.

Shirika la Usawa Kwa Maendeleo (Equality for Growth-EfG), linalojishughulisha na kuwawezesha wanawake walioko katika sekta zisizo rasmi, ikiwamo masokoni, limekuwa mstari wa mbele kupigania nafasi za mwanamke kiuchumi na kiutawala.

Kupitia kampeni yake ya miaka mitatu ya “Mpe Riziki Si Matusi” iliyoanza 2015 na inayotarajiwa kumalizika Desemba mwaka huu, liko katika mkakati wa kupinga unyasasaji wa kijinsia, ili kuweka usawa katika kila nyanja.

Wanufaikaji wa “Mpe Riziki si Matusi” kwa mkoa wa Dar es Salaam ni wilaya mbili za Ilala na Temeke. Siku chache zilizopita, shirika hilo lilifanya ziara maalum katika masoko ya Mchikichini, Kisutu, na Tabata Muslim (Ilala) na Gezaulole iliyoko katika Wilaya mpya ya Kigamboni, ambayo zamani ilikuwa sehemu ya Wilaya ya Temeke, lengo ni kupata mrejesho wa kampeni zake.

USHUHUDA

Katika hilo ziara ililenga kupata mrejesho wa kinachotajwa chanya inaohusu kupungua unyanyasaji, kwa zaidi ya asilimia 80 katika maeneo yote.

Wanawake wengi katika masoko hayo walithibitisha kuwa kampeni ziliwawezesha kujitambua na kuanza kupigania haki za kisheria, ikiwamo kuwania nafasi za uongozi wa juu wa soko.

Tabata Muslim, kulionekana kuwa soko la kwanza kuongozwa na mwanamke, Aisha Juma, ambaye anajishughulsha na biashara ya ‘Mama Lishe.’

Aisha anakiri kuwa safari ya uongozi haikuwa rahisi kwake, kutokana na uhalisia kwamba mfumo dume bado ni tatizo lililojichimbia mizizi katika jamii.

“Hata hivyo, sikufa moyo bali changamoto hizo ziliniongezea kujiamini. Kutokana na ukweli kwamba EfG imetufundisha pia masuala ya utawala wa sheria, elimu hiyo naitumia hadi nje ya eneo la soko, hasa kuwasaidia wahanga wa unyanyasaji wa kijinsia na wapi pa kupeleka malalamiko yao,” anasema Mwenyekiti Aisha.

Pendekezo lake ni haja ya kuwapo kampeni za kila mara, jambo litakalosaidia kufutika kwa mfumo dume sokoni, kwani ilikuwa rahisi kwa wagombea wenzake kukubali matokeo ya uchaguzi, kwa sababu wote walikua ni wanufaika wa ‘Mpe Riziki Si Matusi.”

SOKONI MCHIKICHINI

Sokoni Mchikichini kuna vitengo vinne kati ya sita vilivyo katika eneo hilo, ambavyo ni Vyombo vya Ndani, Khanga na Vitenge, Mama lishe, Mitumba, Ushonaji na Vinywaji, vinaongozwa na wanawake.

Wafanyabiashara wanaeleza namna ilivyo ngumu kwa mwanamke kupata hata walau kizimba cha kufanyia biashara, kabla ya kuwapo kampeni, hali inayoendana na kero ya matusi na kejeli, pia kudhulumiwa malipo hasa kwa Mama lishe.

Kwa sauti ya pamoja, wafanyabiashara sasa wanakiri kujitokeza kwa wanawake kugombea nafasi za uongozi sokoni, ikiwa sehemu ya kampeni za EfG.

Betty Mtewele, anayeongoza kitengo cha Khanga na Vitenge, anaiomba serikali kuunga mkono juhudi za wadau binafsi katika, kuhakikisha kunakuwapo semina endelevu, kwani zimewajengea uwezo wa kujiamini na uthubutu katika shughuli hizo .

Anasema kabla ya kampeni, wafanyabiashara kwa ujumla walikuwa wakiamini dhana “uongozi ni kazi ya wanaume peke yao.”

Mwanamke huyo anaongeza:“Hata baada ya kampeni, wapo wasiojiamini kugombea, bali hujitokeza kwa wingi kupiga kura. Hata hilo ni jambo jema”

GEZA ULOLE

Sokoni Gezaulole, nako nafasi ya mwanamke katika uongozi wa juu ilizingatiwa baada ya Amina Mussa kushika nafasi ya Naibu Mwenyekiti, huku vitengo vingi sokoni hapo vikiwa chini ya kinamama.

Sambamba na mafanikio hayo, Amina anasema kuna changamoto ya wanawake wengi kushindwa kuhudhuria kampeni za kuwajengea uwezo, kutokana na kampeni hizo kuendeshwa asubuhi, walengwa wengi wakiwa wamebanwa na pilika za biashara.

“Kwa hiyo, napendekeza kampeni ziendeshwe muda wa mchana, wateja wanakuwa wamepungua. Vinginevyo wadau watusaidie kutufungia vipaza sauti wakati wa kampeni, ili kila mfanyabiashara apate mafunzo akiwa katika eneo lake la kazi,” anafafanua Amina.

KISUTU

Maendeleo ya kinamama kung’ara katika uongozi wa soko, Kisutu kuna hali hali tofauti kidogo, kwani Mwenyekiti wa Soko, Tamimu Chande, anasema hadi sasa hakuna mwanamke hata mmoja katika uongozi wa juu sokoni kwake.

Hata hivyo, anadokeza furaha aliyo nayo pamoja na kutofanikiwa katiika hilo, bado kuna ukweli unabaki kwamba kinamama wengi sokoni wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa Soko, unaotarajiwa kufanyika katikati ya mwezi huu.

“Hiyo ni baada ya maudhui ya kampeni kuwakolea. Vilevile, hakuna mfumo dume katika soko hili. Tunazingatia usawa,” anasema Chande.

KUTOKA EfG NA WFT

Mwezeshaji Sheria kutoka EfG, Shaaban Rulimbiye, anasema kuwa mwanzoni mwa kampeni, nafasi ya uongozi kwa wanawake anaitaja ‘ilikuwa karibu na sifuri.”

Anasema jitihada hizo za EfG zilipanda hadi kufikia asilimia 27 ya malengo mwaka jana na ilitarajiwa kufika asilimia 35 ukingoni mwa kampeini hizo, Desemba mwaka huu.

Kwa mujibu wa mwanasheria huyo “Mpe Rizi Si Matusi” inafadhiliwa na Umoja wa Mataifa kupitia asasi ya “UN Trust Fund’ kwa thamani ya Dola za Marekani 300,000, ambayo ni sawa na Sh. milioni 660.

Rulimbye anaongeza kuwa :“Mbali na masoko ya Dar es Salaam, wanufaika wengine wa kampeni hii ni baadhi ya masoko mkoani Tanga na Mwanza. Ni matarajio yetu kuyafikia masoko yote nchini.”

Shirika la Mfuko wa Wanawake Tanzania (Women Fund Tanzania-WFT) nalo limekuwa mstari wa mbele kupigania haki ya ushiriki wa wanawake katika uongozi wa ngazi mbalimbali, likijikita zaidi kutoa ufadhili kwa asasi zinazopigania haki za wanawake na watoto.

Hivi karibuni, WFT kwa kushirikiana na Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania, kuandika kitabu chenye maudhui ya umuhimu wa katiba mpya.

Mwansiasa mkongwe Anna Abdallah, anawataka wanaharakati wote kuachana na tofauti za itikadi za vyama kupaza sauti ya pamoja kuhusu masuala yanayowahusu wanawake.

“Tunaamini katiba mpya itasaidia kutatua changamoto zote zinazowakabili wanawake, hasa za kiuchumi na kisiasa,” anahuyimisha.

Habari Kubwa