Wasauzi walivyomzuia Rafael kutua Yanga SC

17Jul 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Wasauzi walivyomzuia Rafael kutua Yanga SC

KLABU ya Yanga ilikaribia kabisa kunasa saini ya kiungo wa Mbeya City na timu ya Taifa, Taifa Stars, Rafael Daudi.

Dili hilo lilikuwa likamilike baada ya kurejea kutoka Afrika Kusini kwenye michuano ya Cosafa.

Hata hivyo, mambo yamebadilika. Kungo huyo aliyepiga penalti ya mwisho dhidi ya Lesotho na Taifa Stars kufanikiwa kushika nafasi ya tatu, amepata baadhi ya timu Sauzi ambazo zinahitaji saini yake, baada ya kuwa mmoja wa wachezaji waliofanya vema huko, hivyo kusita kusaini Yanga kwanza.

"Zipo timu nyingi zinanihitaji, Sauzi kuna timu kama tatu hivi, Yanga nayo imo na tulifikia makubaliano kwa asilimia 80," anasema Alfa aliyemaliza ligi akiwa na mabao saba.

Hata hivyo, anasema baada ya mechi ya marudiano dhidi ya Rwanda, itajulikana kama atatua Yanga au atakwenda nchini Afrika Kusini.

"Mambo yote yatakamilika hapo, tutajua nakwenda wapi, kwa sababu kila kitu itakuwa tayari, walioonyesha nia ya kweli watakuwa wameshinda," anasema kiungo huyo.

Mchezaji huyo ambaye kwa sasa amekuwa lulu huku akitajwa kutakiwa na Yanga kuziba pengo la Haruna Niyonzima ambaye taarifa zisizo rasmi zinadai kuwa huenda akajiunga na Simba, mara mkataba wake na Yanga utakapomalizika mwezi huu.

Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, alishatangaza rasmi kuachana na kiungo huyo raia wa Rwanda, baada ya kushindwana naye dau.

Rafael ambaye mashabiki wake wa soka wanamwita Alfa, amekuwa kwenye rada za Yanga baada ya kumkosa Keny Ally aliyejiunga na Singida United.

Hata hivyo, taarifa zinadai kuwa Simba nayo ilikuwa inamwania mchezaji huyo, lakini mwenyewe na washauri wake wakaona si sehemu mwafaka kwenda, kutokana na timu hiyo kusheheni viungo wengi kuliko idara nyingine yoyote tofauti na Yanga.

Alipandishwa kutoka kikosi cha pili cha Mbeya City misimu mitatu iliyopita, huku msimu wake kwa kwanza kucheza ligi 2014/15, ukiwa ndio timu hiyo ilipanda Ligi Kuu.

Kwenye msimu wake wa kwanza alimaliza ligi akiwa na mabao mawili, yote yakiwa ya penalti.

Msimu wa pili, 2015/16, alifunga mara sita, mabao manne yakiwa ya penalti.

Msimu uliopita, kiungo huyo aliipachikia timu yake ya Mbeya City mabao saba, mawili yakiwa ya mikwaju ya penalti. Kwa misimu mitatu, rekodi zinaonyesha kuwa Rafael amecheka na nyavu mara 15.

Kati ya mabao hayo, nane yakiwa ya penalti. Hii inaonyesha kuwa mchezaji huyo ni 'mtaalamu' wa kupiga mikwaju penalti, kwani rekodi zinaonyesha kuwa hakuwahi kukosa hata moja kwenye mechi za Ligi Kuu, pia moja aliyopiga Taifa Stars wakati ikiibuka mshindi wa tatu katika michuano ya Cosafa.

Habari Kubwa