Wafugaji walia mateso yamezidi kipimo

19Nov 2017
Mary Geofrey
Nipashe Jumapili
Wafugaji walia mateso yamezidi kipimo

WAKAZI wa tarafa ya Loliondo, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, wanaeleza machungu na adha walizopata kufuatia kuwapo kwa mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 27 kati ya wakulima na wafugaji.

Mgogoro huo ambao ulihusisha jamii ya wafugaji na wahifadhi katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, umesababisha wananchi kubomolewa nyumba na maboma yao zaidi ya 500 na hivyo kusababisha baadhi yao kukosa mahala pa kuishi.

Agizo la kuwaondoa wananchi wanaoishi katika hifadhi hiyo, lilitolewa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, na kusababisha wanavijiji kuchomewa nyumba na maboma yao.

Mifugo 700 ilikufa kwa kukosa malisho na wanyama wengine zaidi ya 2,000 waliuzwa bila kufuata taratibu na kaya zaidi ya 500 zilipoteza makazi, watu 20 walipoteza maisha na 10 walishikiliwa kwa makosa mbalimbali.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala, mara baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli, Oktoba mwaka huu kuiongoza wizara hiyo, aliamua kuanza kushughulika na mgogoro huo kwa kufanya ziara na kuzungumza na wafugaji.

Oktoba 27, mwaka huu, Dk. Kigwangala alisitisha uchomaji wa maboma na nyumba za wafugaji na kuagiza kuwa, wasubiri ripoti ya tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuchunguza mgogoro huo chini ya Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo.

Mara baada ya Dk. Kigwangala kuagiza wafugaji hao wasiondolewe katika pori hilo, wafugaji wanadai wanachokumbana nacho ni kukamatiwa mifugo yao.

Mifugo yaswagiwa hifadhini

Nikiwa katika kijiji cha Kitaalo nazungumza na wafugaji ambao wanaeleza masikitiko yao juu ya kile walichokiita uonevu wa hali ya juu unaofanywa na Askari kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Yohana Toroge anasema ng’ombe wake walikamatwa eneo la kijiji lililo umbali wa kilometa 15 kabla ya kuingia hifadhini na askari hao waliwaswaga kuwaingiza Serengeti na kudaiwa kuwa walikutwa kwenye hifadhi.

“Mifugo yetu inakamatwa katika eneo la kijiji halafu wanaanza kuiswaga kuiingiza hifadhini ili kutafuta ushaidi wa kutushtaki,” analalamika Toroge.

Mfugaji huyu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kartalo anasema, Dk. Kigwangala aliagiza unyanyasaji wa kuchomewa nyumba, kupigwa na mifugo yao kuteswa visitishwe lakini ukatili huo unaendelezwa.

“Lengo lao baada ya kuona Waziri amezuia tusifanyiwe ukatili na mifugo iruhusiwe kunywa maji wanafanya hivyo ili kutuchonganisha naye kwa sababu wanakamata mifugo yetu kwa makusudi na kuiingiza ndani ya hifadhi,” anasema.

Thomas Kairungi anasema, serikali inapaswa kuliangalia jambo hilo kwa undani kwa sababu wanayofanyiwa yana lengo la kuwaangamiza wafugaji ili hali wao ni watunzaji wa mazingira.

“Wanataka kutufilisi kwa sababu wanakamata ng’ombe zetu zikiwa malishoni na kuanza kuziswaga, wakishazifikisha hifadhini wanatutaka tukazikomboe na tukichelewa wanazipiga mnada,” anasema.

Anasema Waziri Kigwangala anasitisha kazi hiyo kusibiri ripoti ya tume na kabla ya kutoa suluhu ya kudumu kuhusu tatizo hilo watu wenye lengo la kuuendeleza mgogoro huo ndiyo wanaanzisha na kutekeleza vitendo vya kihalifu.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ngorongoro, Ndirangu Senge, anasema ng’ombe wake na wa wafugaji wengine zadi ya 1,000 waliswagwa umbali wa kilometa saba na kuingizwa Serengeti.

“Ng’ombe wangu walikuwa malishoni kama ilivyokawaida lakini askari wa wanyapori wakawakamata na kuwaswaga hadi kuwaingiza hifadhini ili kudai kuwa tunakiuka agizo la Waziri la kutoingiza mifugo hifadhini,” anasema.

Anasema baada ya kuona hivyo aliamua kwenda kuulizia ng’ombe wao na walitakiwa kulipa Sh. 7,000,000 kuwakomboa.

Damian Rango wa Kijiji cha Ngorebeth, anadai alilazimika kukimbia umbali wa kilometa 10 kukwepa kukamatwa na askari wa hifadhi walioingia ndani ya kijiji kwa ajili ya kukamata mifugo yao na kuwachukulia hatua.

“Hatuna amani kwenye nchi yetu, Waziri alishaagiza mifugo isikamatwe lakini tunachofanyiwa ni kuteswa bila sababu ndani ya kijiji,” anasema Rango.

Kadhalika, anasema, awali wakati wa operesheni ya kuwafukuza na kuwaondoa katika kijiji hicho kabla ya kuzuiliwa na Dk. Kigwangala, ng’ombe wake walichomwa moto.

Anasema serikali pekee ndiyo inayoweza kuwasaidia na kuwatoa katika mateso ya mgogoro huo ambao una maslahi ya watu wachache lakini una mateso makali kwa wananchi wengi wa Tanzania.

VIBALI VYA MAJOSHO
Wakazi hao pia wanatumia fursa hiyo kumuomba Waziri Kigwangala ambaye ameruhusu mifugo yao ipelekwe kunywa maji katika maeneo waliyokuwa wakitumia siku za awali, kuwapatia vibali maalum.

“Tunaomba vibali kwa sababu tumeona hawa askari wa hifadhi wakija na kukuta ng’ombe wakinywa maji eneo tunalotumia kuwanyweshea ambalo ni kilometa chache kuingia hifadhini wanawaswaga na matokeo yake wanasingizia tumeingia hifadhini,” anasema Patrina Kubwani.

Kubwani anasema, kama watakuwa na kibali itakuwa rahisi kuliko kutumia kauli ya Waziri pekee ambayo wakati wowote inaweza kutenguliwa, kama ambavyo wanasingiziwa kuingiza mifugo hifadhini.

“Kama tukipata kibali tutakuwa huru na mifugo yetu itakunywa maji kwa amani katika eneo hilo lilitengwa kwa ajili ya shughuli hii,” anasema.

Anaeleza zaidi kuwa, wanalazimika kwenda kunywesha maji mifugo yao eneo hilo kwa sababu hawajazoea kukaa karibu na vyanzo vya maji.

SERIKALI YAJIPANGA
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro, Silom Eliachim, anasema wanahakikisha wananchi na mifugo haingii ndani ya hifadhi hiyo.

Anasema wameweka mikakati ya kukabiliana na changamoto za wafungaji kusingiziwa kuingiza mifugo hifadhi hiyo na wanaojiita wahifadhi wenye lengo la kuendeleza mgogoro huo kwa maslahi yao binafsi.

Eliachim anasema mbali na mipango hiyo pia wanaendeleza utamaduni wa kutunza maeneo hayo yote ya hifadhi kwa maslahi binafsi na ya taifa kwa ujumla.

“Tunamuomba Waziri Kigwangala, asirudi nyuma katika kazi hii aliyoanza kuifanya, tupo nyuma yake na tunamuhakikishia hakuna mifugo iliyoingizwa hifadhini kama inavyodaiwa,”anasema.

Habari Kubwa