Wachezaji 7 Bongo wanaopendwa zaidi na watoto

20Mar 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Wachezaji 7 Bongo wanaopendwa zaidi na watoto

MOJA ya habari zilizotia fora hivi karibuni ni tukio la mtoto mmoja aliyejulikana kwa jina la Aziz, mkazi wa Dodoma kuonekana kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma akiangalia mechi ya kirafiki kati ya Simba dhidi ya Polisi Dodoma akiwa amevaa fulana kuukuu iliyoandikwa jina la Ibrahim Ajibu mgongoni.

Picha hiyo ilirushwa kwenye mitandao mbalimbali na kuzusha mijadala, lakini ikienda mbali zaidi hadi baadhi ya mashabiki wa Simba kuwaagiza wenzao wa Dodoma kufanya kila njia ili kumpata mtoto huyo.

Mtoto huyo aliyeonyesha mapenzi makubwa kwa mchezaji huyo wa Simba na kuandika jina la mchezaji huyo na namba yake kwa kalamu, alipatikana na baadhi ya mashabiki kuanza kumchangia pesa ili apate jezi halisi ya klabu ya Simba.

Mwenyewe alieleza mapenzi yake kwa Ajibu, na jinsi alivyopata ugumu na changamoto kubwa ya kupata ruhusa na pesa ili kwenda kutazama mechi hiyo iliyoisha kwa Simba kushinda mabao 3-0.

Akafichua kuwa hakuwa peke yake aliyetoroka kwao kwenda kutazama mechi hiyo, bali yupo na rafiki yake Rajabu Omari ambaye naye anajiita Kichuya.

Aziz akadai kuwa hata rafiki yake naye alivaa fulana iliyoandikwa Kichuya kama yeye, ila kwa bahati mbaya hakutolewa kwenye mitandao ya kijamii na magazetini kama yeye.

Akafichua kuwa wao kila mmoja anampenda mchezaji wake na hata wakiwa wachezaji shuleni, yeye huiga uchezaji wa Ajibu na mwenzake wa Kichuya na mpaka sasa hata majina yake halisi yanaanza kupotea kwani watoto wenzao wote wanawaita majina ya wachezaji hao ambao wenyewe wanataka kuwa kama wao hapo baadaye.

Hii ni kuonyesha kuwa kuna baadhi ya wachezaji wanakubalika na kuwa mfano wa watoto watakaokuja kuwa wachezaji wa baadaye.
Mfano Kichuya hafichi kuwa aliyemfanya kupenda kucheza soka na hatimaye ndoto yake kutimia ni Haruna Moshi 'Boban'.

Uchunguzi wa mwandishi wa makala haya, umeonyesha kuwa kuna baadhi ya wachezaji wanaocheza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa wamekuwa vipenzi vya watoto sehemu mbalimbali nchini.

Majina yao yapo midomoni mwa watoto, wakiwa wanacheza mpira, wanaongelea soka au wakiulizwa na watu wazima ni wachezaji gani wanaowapenda Bongo.

Hawa ni baadhi ya wachezaji wanaocheza Bongo ambao wanaonekana ni vipenzi vya watoto.

1. Simon Msuva-Yanga
Ni mmoja wa wachezaji ambao wanapendwa sana na watoto. Kutokana na uchezaji wake, ufungaji magoli, kasi yake na kuibeba mara kwa mara timu ya Yanga, vimemfanya jina lake kutajwa zaidi na watangazaji wa redio na televisheni, pia wanachama na mashabiki wa Yanga.

Hii imefanya kuwavutia hata watoto nao hata wakicheza mpira mitaani, baadhi kujipachika jina hilo.

2. Shiza Kichuya-Simba
Kuibeba Simba kwenye mechi ngumu za Ligi Kuu. Kufunga magoli mechi zote mbili dhidi ya Yanga. Kumemfanya kuwa maarufu zaidi kwenye vyombo vya habari, kitu ambacho kimewafanya watoto nao kuanza kumfuatilia kwenye televisheni na kuvutiwa naye.

Kama tulivyoona kwa mtoto Rajabu, tangu ajiunge na Simba msimu huu akitokea Mtibwa Sugar na kufanya vitu vyake, Kichuya amekuwa ni mmoja wa wachezaji maarufu zaidi si kwenye klabu ya Simba tu, bali Ligi Kuu Tanzania Bara.

3. John Bocco-Azam
Wakati mwingine ukipita mitaani na kukuta watoto wanachezaji mpira, utakutana na mmoja akijiita John Bocco.

Na ukimfutilia, utagundua kuwa yeye ndiye aliyewekwa mbele kama mfungaji wao.

Bocco amekuwa na tabia ya kuzifunga klabu za Simba na Yanga mara kwa mara anapokutana nazo.

Hii imemfanya naye kuwa midomoni mwa watoto na kuonekana kuvutiwa naye.

4. Amissi Tambwe-Yanga
Ni mmoja wa wachezaji ambao ni vipenzi vya watoto mitaani. Ukikutana na makundi hata 10 ya watoto wanaocheza mpira, unaweza kukuta kila kundi lina Tambwe wake.

Hii ni kutokana na mchezaji huyo raia ya Burundi anayecheza soka nchini kuwa mahiri kwa kufunga magoli.

Tangu alipojiunga na Simba mwaka 2013, alikuwa mmoja ya mastraika hatari kabisa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara hadi leo.

Ndiyo maana si ajabu kuona akitajwatajwa na watoto mitaani na kuwa kipenzi chao.

5. Ibrahim Ajibu-Simba
Aina yake ya uchezaji, inawafurahisha sana watoto wanaochipukia kucheza soka. Ajibu bado hadi leo ana mpira ule ambao wachezaji waliokomaa wanauita wa 'kitoto'.

Anapenda kuuchezea mpira anavyotaka, akitaka kuonyesha jinsi mwenyezi Mungu alivyomjalia kipaji. Kanzu, matobo na kunyanyasa mabeki kutokana na staili za chenga zake, ni moja ya mambo yanayowavutia zaidi watoto wanaomtazama kwenye televisheni na kuondokea kumpenda. Ni staili ambayo wao wanalicheza wakiwa shuleni.

6. Donald Ngoma-Yanga
Raia huyu wa Zimbabwe ni mmoja wa wachezaji ambao wanapendwa sana na watoto mitaani.

Aina yake ya uchezaji wa kulazimisha, nguvu na upambanaji, umemfanya kujizolea sifa kwa mashabiki wa soka nchini, kiasi cha kuwa gumzo hata kwa watoto.

Straika huyo mbali na kupendwa na watoto, lakini ndiye mmoja wa wachezaji wachache anayekubalika na mashabiki wa klabu zote, licha ya upinzani wao kwenye soka.

7. Laudit Mavugo-Simba
Ni Mrundi ambaye pia amejizolea ujiko na kupendwa na watoto wadogo. Ukipita kwenye viunga vya jiji la Dar es Salaam, ukikuta mtoto amevaa jezi ya Simba, basi moja ya jina litakuwa ni Mavugo.

Ni straika aliyetua kwa mbwembwe nchini na kuteka hisia za wanasoka nchini, licha ya kwamba awali hakufanya kile kilichotarajiwa.

Hata hivyo, haikuondoa nyota yake ya kupendwa, na sasa anaonekana anaanza kurejea kwenye kiwango ambacho Simba waliamua kumsajili kutoka Vital'O ya Burundi.

Habari Kubwa