Utamu wa mechi za ufunguzi Ligi Kuu

17Jul 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Utamu wa mechi za ufunguzi Ligi Kuu

ZILE nyakati za mashabiki kukaa roho juu, kila mwishoni mwa wiki, zitaanza tena Agosti 26, mwaka huu baada ya Bodi ya Ligi kutangaza kuwa ndiyo siku ya kufungua pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu 2017/18.

Jumla ya timu 16 zitaanza safari ndefu, mithili ya mbio za marathon kutafuta mfalme mwingine wa soka la Tanzania kwa msimu mpya.

Mara nyingi mechi za mwanzo huwa ngumu kwa sababu kwanza timu huwa hazifahamiani vizuri, ama zinakuwa na makocha wapya na mifumo mipya.

Timu nyingi zinakuwa na wachezaji wapya waliojiunga, hivyo kuongeza nguvu na chachu kwenye timu.
Timu ngeni nazo pia huwa zinakuwa na nguvu, hata kama baadaye zitakuja 'kutepeta'.

Lakini kila timu inataka kupata ushindi kwenye mechi za mwanzo, kwa maana hiyo, macho na masikio ya mashabiki ambao muda mrefu hawajapata uhondo huo, yataelekezwa kwenye mechi za ufunguzi.

1. Ndanda vs Azam
Mechi hii itapigwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona. Itaikutanisha timu mwenyeji ya Ndanda, iliyoponea chupuchupu kushuka daraja msimu uliopita dhidi ya Azam iliyokamata nafasi ya nne.

Azam itabidi iende kwa tahadhari kubwa Mtwara kwani mara ya mwisho kucheza kwenye uwanja huo dhidi ya Ndanda Ligi Kuu msimu uliopita ilichapwa mabao 2-1, Septemba 24, mwaka jana.

2. Mwadui vs Singida
Mwadui itakuwa na wakati mgumu japo, itakuwa nyumbani, Uwanja wa Mwadui Complex dhidi ya timu iliyopanda daraja, Singida United.

Pamoja na kwamba Singida itakuwa inacheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu, pia ikiwa ugenini, lakini usajili wake ndiyo unaibeba na kuonekana ni timu iliyokamilika.

Imefanya usajili wa 'kufa mtu' ikiwa na wachezaji wa kimataifa kutoka Zimbabwe, Uganda na Rwanda, pia ikiwa na wachezaji wa Kibongo wengi wao ambao ni wazoefu kwenye Ligi Kuu.

3. Mtibwa vs Stand
Itakuwa ni mechi ngumu kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.

Mechi kati ya timu hizi mbili kwenye uwanja wa Manungu mara nyingi huwa na matukio ya kushangaza.

Msimu uliopita, Oktoba 22 mwaka jana, timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3, mechi ya kufunga nikufunge, Kelvin Sabato ambaye kwa sasa yupo Majimaji, akifunga 'hat-trick.'

Msimu wa 2015/16, mechi kati ya timu hizo mbili, Januari 30, 2016 haikwisha kutokana na mvua kubwa, ikabidi irudiwe kesho yake.

4. Simba vs Ruvu
Moja ya mechi yenye mvuto zaidi siku hiyo, itakuwa kati ya Simba dhidi ya Ruvu Shooting. Nina uhakika kuwa itaangaliwa kwa sababu mbili. Kwanza Simba ni timu yenye mashabiki wengi ndani na nje ya nchi, hivyo watataka kuingalia timu yao hata kama itakuwa dhaifu vipi.

Pili ni kuangalia 'vifaa' vipya vya timu hiyo vilivyosajiliwa, akiwamo Emmanuel Okwi wanafanya nini, pia mashabiki wengi watakuwa wanaangalia viwango vyao.

5. Kagera vs Mbao
Mechi itachezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba. Itakuwa ni kisasi cha mechi ya msimu uliopita Mei 13 mwaka huu, kwenye uwanja huo Mbao ilipokubali kipigo cha mabao 2-1.

Mbao itakwenda ugenini kivingine ikiwa imeondeokewa na wachezaji wake wengi waliotia fora kwenye ligi iliyopita, huku Kagera Sugar, timu isiyotabirika ikitaka kuanza vema nyumbani.

6. Njombe vs Prisons
Timu mpya ya Njombe Mji ndiyo timu pekee iliyopanda daraja iliyopata bahati ya kuanzia nyumbani. Haitotaka kuwaangusha mashabiki wake ambao watajazana kwa wingi kushuhudia Ligi Kuu kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, itakuwa inacheza na timu zoefu na ngumu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

7. Mbeya vs Majimaji
Majimaji itakwenda ugenini Uwanja wa Sokoine kucheza na Mbeya City.
Itakuwa na kumbukumbu ya kuchapwa mabao 3-2, Oktoba 29, mwaka jana, hivyo itakwenda kwa tahadhari.

Hata hivyo, kama itakuwa imefanya usajili mzuri inaweza kupata matokeo, kwani pamoja na uzuri ilionao, Mbeya City imepoteza ubora ule iliyokuwa nao ilipopanda Ligi Kuu.

8. Yanga vs Lipuli

Hii ndiyo mechi pekee itakayochezwa Jumapili ya Agosti 27, mwaka huu.

Lipuli imepata bahati mbaya, kupambana na mabingwa watetezi, Yanga tena ugenini Uwanja wa Taifa ambao ni nadra sana timu hiyo kupoteza.

Lakini kama timu hiyo itataka kuwathibitishia mashabiki wa soka Tanzania kuwa Lipuli ile iliyokuwa ikitikisa katikati ya miaka ya '90, basi iivimbie kwa kutoka sare, au kuifunga. Kila mtu atageuza macho kuitazama. Yanga itakuwa nyumbani, ikiwa na vifaa vyake vyote ilivyosajili.

Habari Kubwa