Umuhimu wa usingizi na ulivyo ‘nyeti’ kwenye ubongo wako

12Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Umuhimu wa usingizi na ulivyo ‘nyeti’ kwenye ubongo wako

Makala ya Alhamisi iliyopita nilizungumzia ugonjwa wa Kiharusi au ‘Stroke.’ Leo naangalia umuhimu wa binadamu kupumzisha akili na uhusiano wake na matatizo ya maradhi ya Msongo wa Mawazo.

KWA NINI TUNAPUMZISHA AKILI?

Kupumzisha akili kuna faida nyingi, ila kuu ni mambo yafuatayo:

• Akili ikipumzika, inaupa ubongo nafasi ya kuona au kutafakari mambo katika uhalisia, pia kuufanya ubongo kuweza kuchanganua mambo katika weledi wa hali ya juu sana, kulingana na upeo wake.

• Pia kutokuwa na msongo wa mawazo, maana yake ni kupunguza mwili kutengeneza homoni zinazosababisha moyo kuongeza msukumo wa damu na kuongeza sukari katika damu, ili kuutayarisha mwili kupambana na msongo.

Hivyo basi, ni hatari kwa maisha ya mtu mwenye ugonjwa wa shinikizo la damu na kisukari. Maana yake ni kwamba, mgonjwa au wagonjwa wa shinikizo la damu na kisukari wanatakiwa kuishi katika namna isiyoweza kusababisha msongo wa mawazo.

Pia ieleweke kuwa, kila binadamu anayo mawazo ya kawaida, ambayo hayajafikia kwenye msongo.

• Uwepo wa msongo wa mawazo, unasababisha mwili kupungukiwa kinga. Hivyo, ni muhimu kwa mtu mwenye upungufu wa kinga mwilini kuepuka hali hiyo, kwani kila wakati anapokuwa na msongo wa mawazo, inamfanya kupunguza kinga zake za mwili.

• Kupumzisha akili na hasa kupitia usingizi ni muhimu sana, hasa kwa wanafunzi na wafanyakazi. Akili inapopumzika, inapata nafasi kubwa sana ya kuweka kumbukumbu vyema.

Mwanafunzi anayesoma huku akipata muda mzuri wa kupumzika humfanya alichokisoma kukaa katika ubongo kwa muda mrefu, kuliko yule aliyekuwa anasoma wakati akili imechoka.

Mtu anayesoma na kuthamini muda wa mapumziko, anakuwa na kumbukumbu ya muda mrefu au hata miaka mingi. Wafanyakazi ambao hawapati muda mzuri wa kupumzika, ufanisi wao wa kazi huwa ni mdogo. Mathalan, mfanyakazi anatakiwa kuandika taarifa za kikao ambazo kwa kawaida anatumia saa moja au mbili, anajikuta anatumia siku nzima kufanya kazi hiyo.

• Kupumzisha akili kunasababisha mwili kuwa na furaha. Hivyo basi, mtu mwenye mapumziko mazuri ya akili, ni mwenye furaha na kwa wanaomzunguka, wanakuwa mashuhuda, iwe majumbani na kazini.

NAMNA YA KUPUMZISHA AKILI
Kuna mambo mengi muhimu katika kupumzisha akili. Baadhi ni kama yafuatayo:

• Kuuruhusu ubongo kuona au kutafakari kitu kizuri, ambacho mara nyingi ni kwa ajili ya kukufurahisha tu. Mfano, kwenda kwenye ufukwe wa bahari au ziwani au kando ya mto ukikaa na kuangalia maji, miti, maua, mchanga au miamba kwa jinsi ilivyopendeza, kuona na kusikia sauti za ndege na viumbe hai vingine.

Ni ukweli kuwa sauti ya maji na mawimbi ya bahari, maziwa au mtiririko wa maji mtoni huwa yanaleta mapumziko mazuri sana ya akili.

Ukumbuke kuwa, hivi vyote unavyoviangalia huwa vipo mara nyingi katika uzuri wa maumbo ya dunia, vinakupa pumziko la akili lisilokuwa na kukumbusha fikra nyingine, mfano kuangalia gari zuri sana au nyumba nzuri sana.

Itafurahisha sana akili. Kuna maeneo ya dunia yaliyobahatika kupata sehemu za wanyamapori na kuwa na mbuga za wanyama kama ilivyo hapa nchini Tanzania. Mbuga ya wanyama ni eneo zuri sana la mapumziko ya akili.

Sidhani kama mtu akarudi kutoka mbuga ya wanyama na akawa na fikra ya kuwafuga, bali atakachoondoka nacho ni furaha ya moyo unayoupa ubongo mapumziko na hamu ya kurudi kufanya kazi kwa bidii na weledi.

Mapumziko mazuri ya akili, ni pale mtu ataona au kusikiliza kitu kipya, ambacho kipo kwa ajili ya kupumzisha akili. Mara nyingi ubongo ukishazoea kwa kurudia mfululizo mpaka unazoea, huwa hali ya mapumziko ya akili inapungua.

Binadamu ameumbwa kwa kuwa na mazoea ya kitu, ndio maana mtu anaweza kushangaa wenye kipato kizuri, hawachoki ama kubadili au kuongeza magari mapya ya kifahari, wakati yule ambaye hana utajiri anahisi ni kupoteza pesa.

Ni moja ya sababu inafanya watu wanawashangaa wanywa pombe wasiochoka kuhama kati ya baa moja na nyingine. Kinachowahamisha ni hali ya kutaka upya, kuona na kusikia mapya huko waendako wanapohama baa.

Pia, ndio maana wanandoa wanaoishi kwa mazoea, wanaona ndoa zao hazina utamu na kwa wanaoishi kwa ubunifu na kutamani kuweka mambo mazuri na mapya, hujiona raha sana.

Dhana ya raha haishii katika uhusiano wake na utajiri wa mali au pesa, raha ni utajiri wa ubunifu na kupenda ulicho nacho. Pia ikumbukwe kuwa, tendo la ndoa ni muhimu sana katika ndoa.

Ni jambo muhimu sana linalopunguza kwa kiwango kikubwa msongo wa mawazo. Ndio maana, baada ya tendo hilo, wahusika hupata usingizi mnono na hasa kama limefanyika katika muda wa mapumziko.

• Jamii yetu imekuwa ikijiuliza, ni kwa nini jamii kama za Wazungu au Waasia, wengi wanatembea Tanzania wakiwa watalii. Wengi wao wanafurahi kupita kiasi, baada ya kutimiza azma hiyo.

• Unafikiri kwa nini wanakuja huku ambako wanajua fika kuwa, kuna hali duni ya kifedha, inayoweza kuathiri miundombinu na usalama wa afya zao? Naomba ufahamu wa kinachowaleta huku ni utajiri wa pesa zao, hivyo wanakuja kutumia, wengine sio matajiri kama wanavyodhaniwa.

Kinachowaleta huku ni nia thabiti ya kutaka kupumzisha akili zao. Wenzetu wengi wao wanafahamu umuhimu wa kupumzisha akili zao.

Kinachowaleta ni kwamba wanafurahishwa na kuzipenda mila na utamaduni na ustaarabu wetu. Kwa mfano, wanakuja Tanzania kwa sababu bado iko katika hatua ya awali ya maendeleo. Kuna ushuhuda mwingi.

Mbuga za wanyamapori, ni eneo zuri sana la kupumzisha akili. Cha ajabu ni kwamba, bado watu wengi wanachukulia kuwa tendo la kwenda kupoteza pesa na muda.

Wengi tumekuwa tukijaribu kulinganisha maisha yetu ya kijiji na uhalisia wa uwepo wa wanyamapori.

Hata hivyo, makazi ya wanyamapori ni tofauti na vijiji. Inawezekana ikawa mtu umezaliwa kijijini na hajawahi kuona wanyama kama tembo, simba au chui katika uhai wako wote, ingawaje viumbe hivyo navyo vinapatikana porini.

Hapo, somo linakuwa tujifunze kutofautisha kati ya umaskini wa kipato na umaskini wa kiutamaduni, mila na desturi na utajiri wa maliasili.

NAFASI YA USINGIZI
Sababu nyingine ni muhimu sana kuwezesha kupata usingizi wa kutosha. Binadamu mtu mzima, kibaiolojia anahitaji saa nane za kulala kwa siku. Upatikanaji usingizi wa kutosha, ni muhimu sana katika kipumzisha mwili na akili.

Utakubaliana nami kuwa, mtu asipopata usingizi vyema, anapoamka asubuhi mwili na akili yake inakuwa imechoka, mithili ya namna anavyojihisi anapoenda kulala.

Kupumzisha akili ni jambo linalomhusu kila binadamu. Na ili mtu aweze kuishi maisha kamilifu, anapaswa kukubali kupumzisha akili yake kila mara na kwa kile ambacho ana uwezo nacho.

Mwisho, kama mtu ana msongo wa mawazo uliosababishwa na mwingine na hana uwezo hata kidogo wa kuweza kubadili hilo, ni vyema ikachukuliwa hatua ya kuonana na mtaalamu wa afya ya akili, amsaide.

L Mwandishi wa makala hii ni daktari wa tiba ya binadamu na mtaalamu bingwa wa saikolojia ya akili, anayeongoza kituo kimoja cha tiba jijini Dar es Salaam na anapatikana kupitia simu namba: +255 762 042669 na anwani ya barua pepe: [email protected]

Habari Kubwa