Ummy ahimiza wanawake Singida kutumia fursa zilizopo za kiuchumi

22Apr 2017
Jumbe Ismaily
Nipashe
Ummy ahimiza wanawake Singida kutumia fursa zilizopo za kiuchumi

TAREHE 08, Machi ya kila mwaka serikali ya Tanzania huungana na nchi zingine duniani kuadhimisha siku ya wanawake duniani,ambayo chimbuko lake ilikuwa ni sehemu ya mapambano ya kujenga ujamaa.

Wanawake wajasiriamali mkoani Singida wakiwa kwenye uzinduzi wa Jukwaa la Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi: PICHA: MTANDAO

Na maadhimisho ya kwanza ya siku ya wanawake duniani yalifanyika mwaka 1910 nchini Ujerumani, baada ya kupitishwa kwa Azimio la Chama cha Kijamaa Amerika.
 
Nchi zote za Ulaya Magharibi na Amerika ziliadhimisha siku hii kwa pamoja mara ya kwanza mwaka 1977, baada ya Umoja wa Mataifa (UN), kuomba wanachama wake kuitangaza Machi 08, kuwa siku ya UN ya Haki za Wanawake na Amani.

Na tangu wakati huo, siku ya wanawake duniani imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka Machi 08.
 
Mkutano wa Beijing nchini China mwaka 1995 ni matokeo ya uamuzi huo wa UN.
 
Maadhimisho haya ni fursa ya kipekee kwa wanawake kupata mwanga, fursa za kubadilishana uzoefu, kutathmini na kuihabarisha jamii kuhusu hatua zilizofikiwa na vikwazo vilivyopo katika kufikia maazimio ya utekelezaji wa malengo ya mkutano wa Beijing, uliofanyika miaka 23 iliyopita.
 
Katika Makala hii Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anazitaja sababu za kuhitimishwa kwa siku hii pamoja na changamoto zilizopo kwa wanawake.
 
Ummy anasema maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani huandaliwa kwa lengo la kutambua na kuenzi mchango wa mwanamke katika jamii na pia kutoa fursa kwa wadau mbalimbali wa masuala ya maendeleo, kutafakari kwa kina umuhimu na nafasi ya mwanamke katika kutekeleza shughuli za kuleta maendeleo.

Wadau hawa ni pamoja na Mashirika yasiyo ya kiserikali,vyama vya siasa, sekta binafsi, wabia wa maendeleo na jamii nzima.

“Kauli mbiu ya Siku ya Wanawake duniani ya mwaka huu ni ‘Tanzania ya Viwanda:Wanawake ni msingi wa mabadiliko ya kiuchumi,” anasema Waziri huyo.
 
Anafafanua, kauli mbiu hii inahimiza jamii kuona umuhimu wa wanawake katika kufikia lengo la serikali la kuwa nchi ya Viwanda.
 
Aidha kauli mbiu hiyo inawakumbusha juu ya umuhimu wa kuhakikisha wanawake wanashiriki na kunufaika na shughuli za kiuchumi hapa nchini, hususani katika kipindi hiki ambacho nchi yetu inajipanga kufikia uchumi wa kati kwa kuwekeza katika viwanda.
 
“Nimefahamishwa kuwa Mkoa wa Singida una jumla ya watu 1,381,750 ,kati yao wanawake ni 714,653 sawa na asilimia 51.7 na wanaume ni 699,541 sawa na asilimia 48.3. Na kwa matokeo ya mwaka 2016 yanaonyesha kwamba wanawake wako 766,184 na wanaume ni 749,982”.anafafanua.
 
Ummy anaweka bayana kuwa, mwaka 2012, Manispaa ya Singida ilikuwa na wakazi 150,379 na miongoni mwao wanawake walikuwa 76,895 na wanaume 73,484.
 
Takwimu hizo zinaonyesha kwamba wanawake ni wengi katika kila nyanja na ni wazalishaji na wanunuzi wa bidhaa zinazozalishwa na viwanda.

MKAZO

Hivyo Mwalimu anasema kuwa katika kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu na kunufaika ipasavyo na uchumi wa viwanda ni muhimu masuala ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, elimu na mafunzo, ushiriki katika uongozi na maamuzi, kupiga vita mila na desturi zenye madhara yakatiliwa mkazo.
 
Aidha anafafanua kuwa,baada ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ya mwaka huu, ni vizuri kutafakari hatua ambazo zimechukuliwa na serikali, wadau mbalimbali na mtu mmoja mmoja pamoja na changamoto zinazojitokeza na namna ya kuzikabili kuhusiana na ustawi wa wanawake.
 
Anasema serikali inatambua kwamba wanawake ni msingi wa mabadiliko ya kiuchumi.

Anafafanua kwamba na ndiyo maana katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 hadi 2020/2012) imetoa kipaumbele katika kuwawezesha kiuchumi.

Mwalimu anasisitiza kwamba serikali imekuwa ikichukua hatua za kuwawezesha wanawake kuwa washiriki na wanufaika muhimu wa uchumi wa viwanda.
 
“Nimeambiwa kuwa wanawake wa Mkoa wa Singida mmefanikiwa kujiunga katika vikundi vya kuweka na kukopa ambapo kwa Manispaa ya Singida pekee kuna vikundi 230 vyenye wanachama 2,120 wenye mtaji wa shilingi milioni 150, ninawapongeza  kwa jitihada hizi za kujiletea maendeleo”. anasisitiza.

KILICHOFANYWA NA WIZARA
 
Katika kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu na kunufaika na shughuli za kiuchumi, Mwalimu anasema wizara yake iliwezeshwa kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake mwaka 1993 na Benki ya Wanawake Tanzania mwaka 2007.
 
Anasema kufikia mwaka 2016, Benki ya Wanawake Tanzania imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 9,323,240,000 kwa wajasiriamali 6,267,kati yao wanawake ni 4,596.
 
Anafafanua kwamba kiasi cha mikopo iliyotolewa imeongezeka kutoka shilingi 112,473,600,000 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi 121,796,840,000 mwaka 2016.
 
Aidha, idadi ya wajasiriamali waliopata na kunufaika na mikopo inayotolewa na Benki ya Wanawake Tanzania iliongezeka kutoka wajasiriamali 79,983 mwaka 2015, hadi kufikia wajasiriamali 86,250 mwaka 2016 na kwamba asilimia 73 ya wanufaika wa mikopo hiyo ni wanawake.
 
Katika kuhakikisha wanawake wanajikwamua kiuchumi,Mwalimu anasema wizara yake imeendelea kuhamasisha Halmashauri kuchangia asilimia tano ya mapato yake ya ndani kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake.

Anasema kutokana na uhamasishaji huo, kati ya mwezi Julai na Septemba 2016,Halmashauri 101 zilitoa jumla ya shilingi bilioni 4.1 kwa vikundi vya wanawake na vijana.
 
“Na kwa taarifa nilizonazo katika kipindi hicho Mkoa wa Singida ulichangia kiasi cha shilingi 13,555,000 ambazo zilitolewa kama mikopo kwa vikundi mbalimbali vya kiuchumi,” anasema na kuongeza:
 
“Natumia fursa hii kuzipongeza Halmashauri za Mkalama na Manyoni kwa kuchangia angalau shilingi 5,000,000 kwa kila wilaya na kuonyesha dhamira ya kuwawezesha wanawake kiuchumi, ikilinganishwa na Halmashauri zingine za Mkoa wa Singida.”
 
Hata hivyo, Waziri Ummy anasema kiasi kilichochangiwa na Halmashauri za Mkoa wa Singida ni kidogo ikilinganishwa na kiasi cha shilingi milioni 206 kilichotakiwa kutolewa na Halmashauri zote za Mkoa huo katika kipindi husika, ikiwa ni asilimia tano ya mapato ya ndani.
 
Anaweka wazi kwamba Halmashauri za Manispaa ya Singida, Itigi na Ikungi, hazikuchangia kabisa pamoja na kutenga fedha.
 
“Natoa wito kwa Halmashauri zote nchini ikiwamo Halmashauri za Mkoa wa Singida kuchangia asilimia tano ya mapato yao ya ndani kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake nchini kwa kuwa kushindwa kufanya hivyo ni kukwamisha jitihada za kufikia Tanzania ya Viwanda,” anasisitiza.

JUKWAA LA KIUCHUMI LA WANAWAKE
 
Katika hatua nyingine, Mwalimu anabainisha kwamba, mwaka 2016 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani alizindua Jukwaa la Taifa la Wanawake la Kiuchumi.
 
Anafafanua uanzishwaji wa majukwaa haya kwa ngazi ya Mkoa umeshaanza ambapo Mkoa wa Kigoma umekuwa wa kwanza kuzindua jukwaa hilo na kwamba Mkoa wa Dar-es-Salaam uko katika hatua za mwisho za kufanya hivyo.
 
“Nitoe changamoto kwa wanawake wa Mkoa wa Singida kuwa wa kwanza kuanzisha jukwaa hili la kiuchumi la wanawake kwa Kanda ya Kati na hakika mnaweza kufanya hivyo”anabainisha.

Habari Kubwa