Taharuki kijijini mlipuko wa Ukimwi kwa watoto

23May 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Taharuki kijijini mlipuko wa Ukimwi kwa watoto
  • Mkoa wenye zahanati feki 500

NI hali ya aina yake, kijiji kimoja nchini hapa kimekumbwa na mlipuko wa virusi vya HIV vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi.

Watoto wakipatiwa huduma ya kuangaliwa afya, mkoani Sindh. PICHA: BBC.

Sindh, Pakistan

 

Hiyo ilianza na kuibuka dalili zilizojitokeza tangu miezi mitatu iliyopita, kijijini Ratto Dero, Kusini mwa nchi katika mazingira yanayotafsiriwa yenye utata.

Hadi sasa hatua zimeshaanza kuchukuliwa na daktari mmoja amekamatwa kuhusishwa na mlipuko huo ambayo waathirika wakuu ni watoto.

Inaelezwa kuwa, wazazi walijaa katika hospitali kulalamika watoto wao wanapatwa na homa za kila mara, hali inayotawaliwa na kuwapo mfululizo wa matukio hayo, kila baada ya muda.

Ili kubaini undani wa tatizo, serikali iliagiza watoto hao wafanyiwe uchunguzi wa kina kiafya na matokeo ya uchunguzi yalithibitisha kuwa wameambukizwa virusi vya HIV pasipo kujulikana chanzo kilivyo.

"Kufikia Aprili 24, watoto 15 waligunduliwa kuwa na virusi vya HIV, japo wazazi wao hawakuwa na virusi hivyo," daktari mmoja anasema.

Kutokana matokeo hayo, zaidi ya watu 607 wengi wao ni watoto kiwango cha asilimia 75, wamekutwa na virusi vya HIV baada ya fununu ya mlipuko wa ugonjwa huo, uliyozifanya familia kwenda katika kambi maalum iliyoazishwa na hospitali ya serikali ya mji huo, katika Mkoa wa Sindh.

Mshangao unaotawala ni kwamba, huo si mlipuko wa kwanza kutokea mahali hapo, bali imekuwa mara kadhaa katika miaka tofauti, ikiwamo kijijini hapo, mwaka 2016 watu 1,521 walikutwa na virusi hivyo.

Takwimu zilizopatikana wakati huo, kwa sehemu kubwa walioambukizwa ni wanaume na ilihusishwa na biashara ya ngono, hasa ya jinsia moja katika mkusanyiko ya kibiashara.

Wakati huo, msako mkali ulifanywa dhidi ya makundi hayo na ukahaba ulikemewa, lakini haukutoweka.

Katika maeneo ya vijijini nchini Pakistan, watu wengi hutafuta huduma za afya kutoka kwa wahudumu wasio rasmi na wanaodaiwa hawajahitimu, kwa sababu inasadikiwa hospitalini huduma ni ya gharama kubwa.

Dk. Fatima Mir, anafanya kazi katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan, anaamini, mlipuko wa kwanza mwaka 2015 hadi 2016, ulichangiwa na udhaifu katika sekta ya afya.

"Kuna njia tatu tu ambayo mtoto anaweza kuambukizwa virusi," anaelezea na kuongeza:"Huenda ikawa kupitia maziwa ya mama anayenyonyesha akiwa na virusi hivyo, kupitia utoaji damu, au kupitia vifaa vya matibabu kama vile sindano."

Anasema, mikasa mingi ya kuambukizwa  watoto inaashiria uwezekano mkubwa wagonjwa kadhaa walitibiwa katika kliniki za vijijini, kutumia sindano moja

Mtuhumiwa Dk. Muzaffar Ghangro, alikamatwa kwa kushukiwa anaeneza maambukizi ya Ukimwi kwa kutumia sindano moja, kuhudumia wagonjwa kadhaa katika kliniki yake, madai ambayo amekanusha

Inaelezwa katika mkoa husika kuna jumla ya kliniki 500 ambazo hazitimiza masharti yaliyowekwa na zimefungwa kote mkoani humo.

Pia, serikali mkoani Sindh, ambako kuna athari ya maambukizi, wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha mlipuko huo.

Habari Kubwa