Simba inavyojipigia Ndanda

01Jan 2018
Adam Fungamwango
Nipashe
Simba inavyojipigia Ndanda

KWA mara nyingine tena, Simba imepata ushindi wa saba mfululizo dhidi ya Ndanda FC.

Mabao mawili yaliyofungwa na straika John Bocco yaliiwezesha timu hiyo kuendeleza ubabe wake dhidi ya Ndanda yenye maskani yake mjini Mtwara.

Jumamosi iliyopita, Simba ilishinda mabao 2-0, ikiwa ni mechi ya  saba mfululizo tangu timu hiyo ipande daraja na kuanza kucheza Ligi Kuu msimu wa 2014/15, lakini ikiwa ni mechi ya nne kushinda mfululizo kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Hii ina maana timu hiyo haijawahi kutoka hata sare na Simba.

Mwandishi wa makala haya amekusanya mechi zote za Ligi Kuu  ambazo timu hizo zimekutana nyumbani na ugenini.

1. Ndanda 0-2 Simba-2014/15 (Nangwanda)Hii ndiyo mechi ya kwanza kwa timu hizo kucheza tangu Ndanda  ilipoanza kucheza Ligi Kuu. Ilichezwa Nangwanda Sijaona Januari  17, 2015. Simba ilishinda mabao 2-0 msimu huo wa 2014/15.Yalikuwa ni mabao ya Mganda, Danny Sserunkuma na Elius  Maguri.

2. Simba 3-0 Ndanda-2014/15 (U/Taifa)Mechi ya mzunguko wa pili msimu huo huo, ilichezwa kwenye  Uwanja wa Taifa Aprili 25 na Simba kuichakaza Ndanda kwa mabao 3-0. Wafungaji walikuwa ni Jonas Mkude, Ramadhani Singano na Said Ndemla.

3. Ndanda 0-1 Simba-2015/16 (Nangwanda)Msimu uliofuata wa 2015/16 Simba ilikwenda tena Mtwara kwenye  Uwanja wa Nangwanda Sijaona. Safari hii ilitoa kipigo cha bao 1-0  mfungaji akiwa ni Ibrahim Ajibu ambaye kwa sasa amehamia klabu ya Yanga, mechi ikichezwa Januari Mosi 2016.

4. Simba 3-0 Ndanda-2015/16 (U/Taifa)Kwenye Uwanja wa Taifa, Simba iliitandika Ndanda mabao 3-0  kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa msimu wa 2015/16, mechi  ikichezwa Machi 10, 2016.

Wafungaji kwenye mechi hiyo walikuwa ni Mwinyi Kazimoto na  Hamisi Kiiza aliyefunga mara mbili kwenye mechi hiyo.

5. Simba 3-0 Ndanda-2016/17 (U/Taifa)Msimu wa 2016/17, Simba ilianzia nyumbani na ilikuwa mechi ya  ufunguzi Agosti 20, 2016 dhidi ya Ndanda.

Kama kawaida, Simba ilipata ushindi wa mabao 3-1, yaliyowekwa wavuni na Laudit Mavugo, Fredrick Blagnon na Shiza Kichuya, huku bao la kufutia machozi la wageni likifungwa na Omari Mponda.

6. Ndanda 0-2 Simba-2016/17 (Nangwanda)Hadithi iliendelea kuwa ni ile ile. Ndanda ilikubali kipigo cha mabao  2-0 nyumbani dhidi ya Simba Desemba 18, 2016 kwenye mechi ya  mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita.

Mzamiru Yassin na Mohamed Ibrahim ndiyo waliofunga mabao kwenye mechi hiyo.

7. Simba 2-0 Ndanda-2017/18 (Nangwanda)Msimu huu Simba imeanzia ugenini dhidi ya Ndanda. Lakini kama  kawaida imepata ushindi wa mabao 2-0 Jumamosi iliyopita.

Bocco alifunga mabao yote mawili dakika ya 52 na 56 na kuifanya timu ya Simba kuendelea na rekodi yake safi dhidi ya Wanakuchele hao.

 

Habari Kubwa