Rwanda yazindua operesheni kupambana na umaskini

21Apr 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Rwanda yazindua operesheni kupambana na umaskini

SHIRIKA la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), limezindua mradi mpya nchini Rwanda, unaolenga kuongeza kasi ya vita dhidi ya umaskini miongoni mwa familia duni katika wilaya nne za nchi hiyo.

Mradi huo ulizinduliwa juzi, jijini Kigali nchini humo.

Mradi utajielekeza kwenye uhusiano madhubuti na thabiti ya mipango ya ulinzi wa kijamii na kilimo, ili kuhakikisha suala la kuwatoa watu kwenye hali ya umaskini ni endelevu, msisitizo ukiwa katika dhana nzima ya kuboresha lishe kwa manufaa ya kiafya.

Ni mradi wa miezi 18 ukiwa na thamani ya Faranga za Rwanda (Rwf) milioni 286, sawa na shilingi za Tanzania, shilingi milioni 780.

Utazinufaisha familia zenye uhitaji katika wilaya nne za majimbo mawili ya nchi hiyo, ambazo ni Rubavu na Nyabihu kutoka jimbo la Magharibi na Rulindo na Gakenke katika jimbo la Kaskazini.

Kimsingi mradi huo utatoa msaada wa kiufundi kwenye mfuko wa serikali wa ufadhili.

Utafanya hivyo kwa kutoa fungu la kima cha chini kuwawezesha wananchi waondokane na umaskini kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi,zikiwamo za kuwapatia msaada wa mifugo.

Wanufaika watapatiwa mbuzi watatu au kondoo watatu au kuku au nguruwe mwenye thamani ya Faranga ya Rwanda (Rwf) 80,000.

Kwa mujibu wa Vyombo vya Wakala wa Utawala wa Kimaendeleo vya Ndani (LODA), mpango huo wa maendeleo wa miaka mitatu unafanya kazi kwenye sekta 30, ikiwa ni sekta moja katika kila wilaya zilizochaguliwa.

Mpango ni kwa kaya duni 19,889 zinufaike na hatua hiyo, huku kiasi cha Faranga za Rwanda (Rwf) bilioni tatu zikitumika kununulia mifugo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo jijini Kigali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Serikali za Mitaa na Masuala ya Jamii, Odette Uwamariya, alisema mradi huo utaenezwa nchi nzima iwapo mpango wa majaribio utakuwa na mafanikio.

Uwamariya alisema mradi huo unahitajika kwa kuwa utasaidia kuboresha mshikamano kati ya mauala ya ulinzi wa jamii na kilimo.

Asilimia 70 ya wananchi wa Rwanda wanategemea kilimo na ndiyo wanaofanya sehemu kubwa ya wale wanaosaidiwa chini ya mpango huu wa ulinzi wa jamii.

Uwamariya alitanabaisha kwamba, kuhusanisha ulinzi wa jamii na kilimo kutatoa mchango mkubwa kwa wananchi kuongeza kasi ya kujinasua na umaskini.

 “Kuuhusisha mradi huu wa programu ya ulinzi wa jamii na kilimo kutasaidia hasa kushughulikia suala la utapiamlo. Huu ni mradi saidizi ambao utakuwa chachu kwetu kufikiria miradi mingine itakayosaidia kuwanyanyua kwa haraka watu wetu kutoka kwenye dimbwi la umaskini,” alisema.

Kwa mujibu wa Utafiti wa Afya ya Idadi ya Watu, takribani asilimia 38 ya watoto chini ya miaka mitano wamedumaa nchini humo.

Rwanda inatafuta kudhibiti suala la udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano hadi chini ya asilimia 18, ifikapo mwaka 2018.

Uwamariya alisema wanufaika wa mradi huu watasaidiwa fursa ya kupata mbegu bora na mbolea pamoja na mafunzo ya kitaalamu ya kilimo.

FAO YANENA
FAO inasema kwamba, kuongeza kasi ya kuufuta umaskini na kuhakikisha panakuwapo na usalama wa chakula na lisjhe, kunahitaji ujumuishi wa wahusika wote ikiwa ni pamoja na suala la jinsia, vijana na maskini wenyewe.

Mwakilishi wa FAO nchini humo, Attaher Maiga, alisema Wizara ya Serikali za Mitaa iko kwenye mchakato wa kuwaorodhesha walengwa wa mfuko huo katika wilaya nne zilizochaguliwa.

 “Tunataka kuendeleza kilimo kinachozingatia lishe kwa maana kuwa mafunzo yatatolewa ili kwamba hata maofisa ugani wanaowasaidia wakulima kwenye mradi huu, wawe na mtazamo wa lishe wakati wanapokutana na wakulima,” alisema.

Naibu Meya wa Wilaya ya Rubavu, anayeshughulikia masuala ya kijamii, Marie Grace Uwampayizina, alisema mradi huo utakapotekelezwa kwa ukamilifu, unaweza kuwa moja ya njia zenye tija za kusaidia kunyanyua wengi kutoka katika lindi la umaskini.

“Mradi huu utakuwa unaongeza thamani kwa walengwa kwa kuwa utawasaidia kuongeza mavuno ya kilimo na mifugo,” alisema.

Takwimu kutoka LODA zinaonyesha kwamba, kati ya mwaka 2009 na 2016, zaidi ya Faranga za nchi hiyo bilioni 43.4 zilitumika kusaidia moja kwa moja kaya 338,970, wakati zaidi ya Faranga bilioni 38.9, zilitumika kuwalipa wafanyakazi 704,307 wa kazi za umma.

Aidha, zaidi ya kaya 250,000 zilipatiwa ng’ombe kupitia programu ya Girinka dhidi ya lengo la kuzifikia kaya 350,000 zinazolengwa kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Takwimu nchini humo zinaonyesha kwamba, umaskini ulishuka kutoka asilimia 60 mwaka 2000, mpaka asilimia 39 mwaka 2013/2014, kama zinavyobainishwa na Utafiti Jumuishi wa Hali ya Kaya (EICV), huku programu ya ulinzi wa jamii ikitoa mchango mkubwa.

Chini ya Visheni 2020, Rwanda inalenga kupunguza umaskini hadi asilimia 20 na ule umaskini wa kutupwa hadi asilimia zero, kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 16.

Makala imetafsriwa kutoka gazeti la The New Times la Rwanda.

Habari Kubwa