Rooney ndani ya mastaa wa5 EPL waliotupia Taifa

17Jul 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Rooney ndani ya mastaa wa5 EPL waliotupia Taifa

AKIWA umbali wa mita 35, straika wa Everton, Wayne Rooney, aliachia shuti kali la juu dakika ya 34, lililokwenda moja kwa moja wavuni na kuipatia timu yake bao la kwanza.

straika wa Everton, Wayne Rooney

Rooney, hakufunga bao hilo kwenye Ligi Kuu ya England au Ligi ya Mabingwa Ulaya. Alilifunga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, wakati timu yake ya Everton ikicheza mechi maalum ya kirafiki kwa udhamini wa Kampuni ya SportPesa dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.

Katika mechi hiyo, ambayo Everton ilishinda mabao 2-1, Rooney pamoja na kuweka rekodi kibao, lakini aliingia pia kwenye rekodi ya kuwa mmoja wa wachezaji wanaocheza au kuwahi kucheza Ligi Kuu ya England, kukanyaga Uwanja wa Taifa nchini Tanzania na kufumania nyavu. Katika makala haya, tunakuletea wachezaji watano akiwamo Rooney mwenyewe waliocheza Uwanja wa Taifa na kucheka na nyavu.

1. Didier Drogba (2010)
Staa wa kwanza anayecheza soka Ligi Kuu ya England kuufungua Uwanja wa Taifa kwa mabao wakati huo bado mpya kabisa, wakati huo Didier Drogba akiwa straika wa Chelsea.

Ilikuwa ni Januari 4, 2010 wakati alipokuja na timu yake ya Taifa ya Ivory Coast na kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Ilikuwa ni dakika ya 37, Drogba alipopachika bao hilo kwa kichwa cha kuchupia mpira, kufuatia krosi ya kiungo Emerse Fae baada ya kumzidi ujanja beki Nadir Haroub 'Cannavaro' ambaye siku hiyo alihakikisha straika huyo hafurukuti.

Kosa dogo tu, lilitosha kumfanya straika huyo aliyekuwa anatisha Ulaya, kufunga bao na kuweka rekodi hiyo.

2. Yaya Toure (2013)
Huyu ni kiungo wa timu ya Manchester City ya England. Naye ni mmoja wa wachezaji waliocheza kwenye Uwanja wa Taifa nchini na kubahatika kufunga bao.

Kwa bahati nzuri, Yaya Toure yeye ameweka rekodi ya kufunga mabao mawili kwenye uwanja huo.

Ilikuwa ni Juni 16, 2013. Alikuja nchini akiwa na timu yake ya Taifa ya Ivory Coast kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Brazil mwaka 2014. Katika mechi hiyo, Ivory Coast iliichapa Taifa Stars mabao 4-2.

Yaya alifunga bao kwa mkwaju wa mpira wa adhabu dakika ya 23, nje kidogo ya eneo la hatari akiupitisha juu ya mstari wa mabeki wa Stars na kumpoteza maboya kipa Juma Kaseja.

Kiungo huyo alifunga bao lingine kwa mkwaju wa penalti dakika ya 43, baada ya Gervinho kuangushwa ndani ya eneo la hatari na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

3. Willfred Bonny (2013)
Kwa sasa anaichezea Manchester City. Lakini wakati anafunga bao Uwanja wa Taifa, alikuwa anaichezea Swansea City inayoshiriki Ligi Kuu England.

Alikuja nchini na timu yake ya Taifa ya Ivory Coast kucheza na Taifa Stars. Ni mechi ile ile iliyochezwa Juni 16, 2013, Stars ikachakazwa mabao 4-2 kusaka tiketi ya fainali za Kombe la Dunia lililofanyika nchini Brazil mwaka 2014 lililohitimishwa kwa Ujerumani kutwaa ufalme.

Bonny yeye alipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Stars kwa kupachika bao la nne dakika ya 88.

4. Mohamed Salah (2016)
Ilikuwa ni mechi ya kusaka tiketi ya michuano ya Afcon mwaka huu iliyofanyika nchini Gabon na Cameroon kutwaa ubingwa.
Mechi hiyo ilichezwa Juni 4, mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Staika Mohamed Salah wa timu ya Taifa ya Misri alitua nchini wakati timu yake ilipocheza na Taifa Stars.

Wakati huo alikuwa akiichezea AS Roma ya Italia kwa mkopo, akitokea Chelsea ya England aliyoichezea tangu 2014 hadi 2015 alipopelekwa kwa mkopo Fiorentina pia ya Italia, kabla ya kupelekwa Roma.

Straika huyo hivi karibuni amejiunga na Liverpool na ataanza kuonekana tena Ligi Kuu ya England mwezi ujao.

Aliisaidi Misri kuifunga Stars mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa na kufuzu Afcon, na kufungwa kwenye fainali mabao 2-1 na Cameroon.

Salah alifunga mabao yote mawili kwenye dakika ya 43 na 58.

5. Wayne Rooney (2017)
Alhamisi ya Julai 13 mwaka huu, nahodha wa timu ya taifa ya England, Wayne Rooney alifunga bao dhidi ya Gor Mahia kwenye Uwanja wa Taifa.

Licha ya kuingia kwenye rekodi ya mastaa waliopachika mabao Taifa, lakini pia lilikuwa la kwanza kwa mchezaji huyo aliyerejea klabu yake ya utotoni, Everton baada ya miaka 13 tangu ahamie Manchester United, akikumbushia kitu alichofanya wakati anajiunga na timu hiyo kwa mara ya kwanza kabisa alipofunga bao lake la kwanza katika mechi ya kwanza dhidi ya Arsenal mwaka 2002, siku tano kabla hajatimiza miaka 17.

Habari Kubwa