PROFESA LIPUMBA Mwanasiasa aliyetingisha siasa za upinzani 2016

11Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
PROFESA LIPUMBA Mwanasiasa aliyetingisha siasa za upinzani 2016

MWAKA 2016 umeondoka na makandokando mengi ya kisiasa na utabaki kuwa wenye historia ya kipekee kutokana na matukio makubwa ya kisiasa yaliyotokea.

Yapo matukio mengi ya kisiasa ya kukumbukwa mwaka jana lakini kwenye makala hii tutaangazia sinema ya ‘Mwenyekiti wa CUF’, Profesa Ibharim Lipumba tu.

Mwanasiasa huyu alisababisha mtikisiko wa aina yake kwenye Chama cha Wananchi (CUF), mwaka jana baada ya kujiuzulu Agosti mwaka 2015 na kurejea tena kwenye nafasi yake.

Agosti 5 mwaka juzi, mwanasiasa huyo aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuwaambia kuwa anaachia nafasi yake ya Mwenyekiti kutokana na sababu mbalimbali.

Moja ya sababu alizozitoa ni kwamba amekerwa na namna ambavyo Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), imeshindwa kusimamia masuala waliyokubaliana kwenye umoja huo.

Lipumba alidai kuwa nafsi yake inamsuta kuona watu waliokuwa wanaipinga Rasimu ya Katiba ya Joseph Warioba wanakaribishwa kwenye Ukawa.

Hapo Lipumba alikuwa akimlenga aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Ukawa, Edward Lowassa, ambaye wakati huo ndiyo alikuwa ametokea CCM na kujiunga na Chadema.

Katika hatua za awali za mikutano ya Ukawa kumkaribisha Lowassa, Lipumba alihusishwa na mikanda mbalimbali ya video inathibitisha hilo. Hivyo hatua ya Lipumba kukana kushiriki katika mchakato wa kumkaribisha Lowassa ilikuwa kituko.

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa yeye atabaki kuwa mwanachama wa kawaida wa chama hicho na mshauri wa masuala ya uchumi na masuala ya maendeleo.

Kujiuzulu kwa Profesa Lipumba kulisababisha taharuki kubwa kwenye Ukawa, hasa ikizingatiwa kuwa wapinzani walikuwa wameungana kuing’oa CCM madarakani.

Chama chake nacho kilitaharuki kuona kiongozi wao anawakimbia wakati wa mapambano muda ambao bado walikuwa wakihitaji awavushe kwenye wimbi la Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Profesa Lipumba alionekana kama nahodha ambaye anajitosa baharini baada ya meli kupata dhoruba akiwaacha abiria wake bila kujua cha kufanya ili wajiokoe.

Lakini yote kwa yote, pamoja na kuacha mshangao mkubwa kwa hatua yake ya kujiuzulu wakati Uchaguzi Mkuu unakaribia, Profesa Lipumba aliwastaajabisha Watanzania na pengine dunia pale aliposema anarudi kwenye nafasi yake.

Kuna usemi kwamba ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni, Profesa Lipumba alitoa kali ya mwaka pale alipoibuka mwaka jana na kudai kuwa anatengua barua ya kujiuzulu na anarudi kukiongoza chama hicho.

Hatua yake hiyo ilisababisha mzozo unaoendelea ndani ya chama hicho ambao bado unaendelea hadi sasa.

Baada ya kutangaza kurejea kwenye nafasi yake, Profesa Lipumba alifika katika ofisi za chama hicho zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam huku akiandamana na umati wa wafuasi wake.

Wafuasi wa Profesa Lipumba walianza kukusanyika katika ofisi hizo kuanzia asubuhi ya siku hiyo baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ikimtambua mwanasiasa huyo kama Mwenyekiti halali wa chama hicho kwa mujibu wa Katiba ya chama.

Ilipotimu saa saba mchana siku hiyo, Profesa Lipumba alifika katika eneo zilipo ofisi hizo akiwa na kundi la wafuasi wake waliokuwa wakicheza kwa ustadi ngoma ya mdundiko, lakini walikumbana na kizuizi cha kuingia ndani kutokana na geti kuu kuwa limefungwa.

Zuio hilo halikudumu kwa muda mrefu ambapo baadaye baadhi ya wafuasi wa kiongozi huyo waliamua kuruka ukuta ili kuingia ndani kumfungulia geti kumwezesha kuingia ndani hali iliyosababisha mtafaruku baina ya wanaomuunga mkono na wasiomuunga mkono.

Wakati mtafaruku huo ukiendelea polisi walikuwepo mapema ili kudhibiti usalama katika eneo hilo na walikuwa wakishuhudia wakiwa ndani ya magari matatu yaliyokuwa yamesimama kando ya geti, wakiwatazama wafuasi hao wakitumia nguvu ili kuingia ndani ya ofisi hizo.

Lipumba alipofanikiwa kuingia ofisini, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kurejea kwake kunatokana na uamuzi uliotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, huku akieleza hatua mbalimbali alizochukua tangu alipoandika barua ya kujiuzulu, barua ya kutengua uamuzi wake na yaliyotokea katika vikao mbalimbali vya chama hicho, ambazo kimsingi zinamfanya kuwa na sifa ya kuendelea kuwa Mwenyekiti halali kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho.

Pamoja na kutetewa na Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Jaji Francis Mutungi, Chama cha CUF kilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kikisema kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya mwaka 1992 haimpi mamlaka wala uwezo wowote Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa ushauri, msimamo au mwongozo kwa vyama vya siasa kuhusiana na maamuzi ya vikao vya chama.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui ilisema katika taarifa ya chama hicho kuwa, “Chama kimepokea kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kile kinachoitwa “Msimamo na Ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu Mgogoro wa Uongozi wa Kitaifa wa Chama cha Civic United Front (CUF)” ambao uliwasilishwa Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni. Chama hakikuomba ushauri kwa Msajili na hivyo tunamwambia ushauri wake abaki nao mwenyewe,” alisema Mazrui wakati huo.

Alisema chama hicho kinawataka wanachama wake na wananchi wote kutambua kwamba Msajili hana uwezo kisheria wa kusikiliza mashauri yanayohusiana na malalamiko dhidi ya maamuzi ya vikao vya vyama vya siasa na kuyatolea uamuzi na kwamba uwezo huo ni wa Mahakama pekee.
Hoja 11 zilizotolewa na Msajili wa Vyama ndizo zilimrejesha Profesa Ibrahim Lipumba kwenye uongozi.

Viongozi wengine waliorudi ofisini kwa huruma ya Msajili wa Vyama ni mwaka jana baada ya kusimamishwa na Baraza Kuu la Uongozi la CUF, katika kikao chake cha Agosti 30, mwaka huu ni Naibu Katibu Mkuu Bara Magdalena Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua na Naibu Mkurugenzi wa Habari Taifa, Abdul Kambaya.

Wengine ni Mbunge wa Mtwara, Maftaha Nachuma, wajumbe wa Baraza Kuu Taifa, Masudi Omari Mhina, Thomas Malima, Ashura Mustafa na Kapasha Kapasha. Pia Musa Haji Kombo, Habibu Mnyaa na Haroub Shamis ambao wataendelea kuhesabika kama wanachama halali wa chama hicho.

Katika barua yake kwa viongozi wa CUF, Msajili alieleza kuwa amefikia msimamo wake huo baada ya kupata nafasi ya kusikiliza pande zote zinazosigana katika mgogoro huo wa uongozi ndani ya chama hicho.

Uamuzi huo ulipingwa na wadau mbalimbali

Uamuzi wa Profesa Lipumba, kurejea ndani ya chama hicho, ulipingwa kila kona huku kigogo mmoja wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), akiweka wazi msimamo wa umoja huo wa kutomuamini Lipumba kwa sababu ana maamuzi ya kitoto.

Aidha, Chama cha CHADEMA kilisisitiza kuwa, hakitamuamini Profesa Lipumba kurejea kwenye umoja huo, kwa sababu hakuna alichokifanya katika kipindi chote akiwa kiongozi wa CUF.

Kauli hiyo ilitolewa na Profesa Jumbe Safari, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu ombi la Profesa Lipumba, kutaka arejeshwe kwenye nafasi yake ya uenyekiti ndani ya CUF.

Profesa Safari alisema hawezi kumwamini Lipumba kwa kuwa sababu alizozitoa awali za kujiengua hazijabadilika.

“UKAWA imeisaidia CUF, hivyo mimi simuamini. Sababu zake zilizomuondosha hazijabadilika, kwani UKAWA bado ipo na Edward Lowassa anaweza kugombea tena urais. Je, atatoka tena? Huo ni utoto,” alisema Profesa Safari.

Aliongeza kuwa UKAWA imeisadia CUF na sio Lipumba, kwa sababu wakati akiwa mwenyekiti, hakuna lolote alilolifanya, hivyo hawezi kuaminika.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Banna, alisema Lipumba alijiuzulu uongozi na sio uanachama,
hivyo kwa kutaka kurejea kwenye nafasi yake, anapaswa kuwaridhisha Watanzania kwa kueleza kama sababu alizozitaja wakati anajiuzulu zipo au hazipo.

Alisema endapo Lipumba atazitaja sababu hizo, wananchi watamwelewa, lakini akishindwa kufanya hivyo, watahoji kwa sababu kiongozi anapaswa kuwa na msimamo na chama chake hata kama kikiwa kinapitia mitafaruku mbalimbali.

“Kiongozi anapaswa kuwa mwaminifu kwenye chama chake katika mazingira ya mitafaruku au raha, hivyo ndivyo inaonyesha namna viongozi wa vyama vya siasa nchini wasivyozingatia misingi ya demokrasia,” alisema Profesa Banna.

Msomi huyo alisema Profesa Lipumba hakuzaliwa kuongoza CUF milele, amekuwa kwenye nafasi ya uenyekiti kwa muda mrefu, hivyo alihoji iwapo chama hicho kimekosa watu wenye uwezo wa kikiongoza.

Alibainisha kuwa kama angekuwa ametimiza wajibu wake kama kiongozi, angekwishawaandaa watu kukiongoza, lakini tatizo la baadhi ya viongozi wa kisiasa hawana demokrasia ya ukweli.

“Viongozi wetu wana uimra, wanaweza kugombania demokrasia nje, lakini kwa ndani, taasisi zao zinakosa demokrasia ya kweli,” alisema mhadhiri huyo.

Habari Kubwa