Ni korosho dhahabu mpya iliyotesa mwaka 2017

31Dec 2017
Gaudensia Mngumi
Nipashe Jumapili
Ni korosho dhahabu mpya iliyotesa mwaka 2017

MTWARA na Lindi kucheele. Kumekucha wakulima wanasema mwaka unamalizika kwa kuacha alama kubwa ya kimaendeleo kutokana na bei nzuri ya korosho.

Wakulima wakifurahia neema ya korosho mkoani Mtwara.PICHA: MTANDAO.

Wanapozungumza na Nipashe wanaamini kuwa  zao hili ni dhahabu mpya inayoongezewa thamani na serikali ya Rais John Magufuli.Mwaka huu wakulima wa korosho wanachekelea na kufurahia kazi ya kilimo kuliko wenzao wengi wanaolima mahindi, viazi, vitunguu na nyanya vyakula ambavyo kila siku vinaonekana karibu kwenye kila meza iwe ni ya mkazi wa kijijini au mjini.

 

Watanzania hawa wanaolima korosho wanavyoingia mwaka mpya wa 2018 wana mengi ya kujivunia, anasema Juma Libaba, mkulima wa korosho wa kijiji cha Dodoma wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi.

 

“Miaka mitano iliyopota bei ya zao hili katika mikoa ya kusini ilikuwa chini ya sh. 1,000 kwa kilo, lakini kuanzia msimu huu bei imepaa hadi kukaribia Sh. 4,000 hivyo kuibua hamasa na kuimarisha kwa mambo mengi ya kiuchumi miongoni mwa wananchi. Ongezeko la bei ni kutekeleza ahadi ya Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa, aliyoitoa kabla ya kufungua msimu wa mauzo ya korosho akiahidi kuwa bei ya zao hili ingekuwa ya kuvunja rekodi,” Anasema Libaba.

 

Anafurahia kwa sababu zamani kilo moja ya korosho ilikuwa inauzwa chini ya Sh. 1,000 lakini sasa kilo imepaa na inakaribia Shilingi 4,000 akikumbukwa kuwa ilianza kuongezeka kutoka Sh. 1,200 au 15,000 na leo imefikia Sh. 3,995.

 

Libaba anaingia mwaka mpya akiwa ameshauza tani kadhaa za korosho anasema alikuwa na takribani kilo 1,000. Anafurahia kuwa mwaka 2017 umeacha alama isiyofutika kwa maendeleo ya wakulima wa korosho mikoa ya kusini. Ni mwaka wa ukombozi kwa mkulima wa korosho wa Tanzania.

 

Anafurahi ushiriki wa serikali kwenye kudhibiti hujuma na ujanja katika biashara ya korosho na kuwabana ‘kangomba au chomachoma’ wafanyabiashara ambao waliwahujumu wakulima kwa kununua zao hilo kwa bei za chini japo waliuza kwa gharama kubwa katika soko la kimataifa.

 

Libaba anataka soko liboreshwe zaidi kwani kwa sasa wakulima wanachoshwa na usumbufu unaotokana na vyama vya ushirika akisema:”Wananchi wakifika kwenye ofisi za vyama wanakutana majina yao yamebandikwa kuwa wamelipwa fedha, lakini wakifika benki hakuna fedha ndani ya akaunti zetu hii ni kero.Watulipe haki zetu kwa wakati,” anasisitiza.

 

Wanufaika hawa pamoja na kuona kasoro hizo lakini kinachowafurahisha ni bei ya korosho kuwa ya uhakika ambayo inawafikirisha kujiletea maendeleo.

 

Wakulima muda mwingi wanafikiria mabadiliko kwenye maisha yao, kwa mfano Somoe Lyuba, anasema kufuatia kuuza korosho kwa bei ya kutakata hali ya kiuchumi inabadilika wananchi wanajenga nyumba bora za matofali ya kuchoma, zinazoezekwa kwa mabati na pia kuwekewa umeme tofauti ilivyokuwa hapo awali.

 

Lyuba mkulima na mkazi wa Kijiji cha Mbuyuni kilichoko kata ya Namichiga, anasema akiwa na wanakijiji wenzake sita wameanzisha ujenzi wa nyumba mpya za tofali za kuchoma na kuziezeka kwa bati.

 

“Nimevuna magunia sita ya korosho yenye uzito wa kilo 562 na nimepata zaidi ya Sh. milioni 2.25 ambazo zitaniwezesha kuukaribisha mwaka kwa kukamilisha ujenzi wa nyumba yangu yenye vyumba vitatu vya kulala. Kiasi kingine cha fedha nitamgharamia mwanangu anayekwenda kidato cha kwanza sekondari ya kata ya Mchinga ,” ni kauli za matumaini kutoka kwa Lyuba akisifia mafanikio ya korosho.

 

Ni habari nzuri kwa wakulima wa korosho ambao wanamalizika wakiwa juu kiuchumi. Japo ingekuwa vyema kama kungekuwa na viwanda vya kubangua na kusindika korosho taifa lingenufaika zaidi kwa vile zao hilo limeongezewa thamani na kuzalisha bidhaa mbalimbali.

 

Korosho zinaposindikwa huzalisha mazao kama mbegu za korosho,siagi ya korosho, ganda gumu hutengeneza mafuta ya ngozi ama kemikali zikiwamo viuatilifu ,hutoa mashudu ambayo ni chakula cha mifugo wakati mabibo hutengeneza juisi na jamu.

 

Viwanda vinavyosindika na kuzalisha bidhaa za korosho vinapatikana mataifa ya jirani kama Msumbiji lakini nchi zenye uchumi mkubwa za Indonesia na Brazili nako zao hilo huongezwa thamani ili kupata manufaa makubwa zaidi kiuchumi.

 

Sasa inapoanza 2018 wakulima wengine kama wa kahawa, mahindi na pamba nao wanahitaji kucheka kama wanavyofanya wenzao wa Mtwara na Lindi. Mahindi ni chakula kinacholika Afrika nzima na kina soko kuanzia Kongo hadi Sudan Kusini.

 

Mathalani, mtandao wa taarifa za bei wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), unataja bei ya mahindi katika soko la kimataifa kuwa ni takribani Sh. 300 kwa kilo. Bei ya kahawa nayo ni karibu Sh. 6,000 kwa kilo karibu (dolla 2.7).

 

Tunapoingia 2018 mkono wa serikali uonekane kwenye mazao mengine ili wakulima wanufaike na kuwa na maisha bora kama inavyotokea kwa wenzao wa Ruvuma, Lindi na Mtwara.

 

Wakulima wengi wa Tanzania wanufaike na bei kubwa za mazao yao kwa kuwa kikombe cha kahawa katika hoteli za kimataifa ni ghali kuliko bei wanayopewa wanapouza kilo moja ya kahawa ghafi kwa wafanyabiashara hii ni kwa mkulima aliyeko mkoani Kilimanjaro, Bukoba  ama Arusha.

 

Habari Kubwa