Nchi zinazotia fora ndoa za utotoni na mkakati wa kuzitokomeza

18May 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Nchi zinazotia fora ndoa za utotoni na mkakati wa kuzitokomeza

NDOA za utotoni ni tatizo kubwa sehemu mbalimbali duniani. Ingawa serikali, mashirika na taasisi mbalimbali zinazojali haki za watoto zimepaza sauti kukemea jambo hilo, lakini bado jamii nyingi zimefumbia macho.

Kwingine zimewekwa sheria kali kudhibiti ndoa hizi, lakini bado halijaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu, hasa pale linapofanyika kwa siri maeneo ya vijijini. Hapa kwetu Tanzania sheria inakataza binti kuolewa chini ya miaka 18 akichukuliwa kuwa bado ni mtoto.

Zipo nchi zingine duniani ambako jamii zake kuozesha watoto wadogo ambao hujikuta wakifikishwa katika hafla za harusi, siyo kwa matakwa yao bali ya watu wengine. Watoto hawa wanajikuta katika maisha mengine ya ndoa wangali wadogo bila wao kuridhia na pia wasijue hatima yao.

Katika hali inayoonyesha ukatili wa hali ya juu dhidi ya watoto, baadhi hufungishwa ndoa pasina wao kujua au hufungishwa ndoa kwa nguvu. Hii ni hatari sana hasa ikizingatiwa kwamba kuwaozesha watoto wadogo huwa na madhara kadhaa ya kimwili kama vile, kutokuwa tayari kushika mimba katika umri mdogo na vile vile matatizo ya kisaikolojia kutokana na kulazimishwa kufunga ndoa. Pia maumbile ya watoto hao yanakuwa hayako tayari kubeba mimba.

Moja ya ripoti ya Tume Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa hivi karibuni ilielezwa kuwa, kila siku duniani mabinti 39 huozwa bila kuridhia wala kupewa haki ya kuchagua mume.

Iwapo hali kama hii itaendelea, inatabiriwa kuwa ifikapo mwaka 2020, kutakuwa na wasichana milioni 142 walioozeshwa kabla ya kufika umri wa miaka 18.

Hebu sikia ushuhuda huu;- Elina ni binti kutoka nchi ya Malawi ambaye alilazimishwa kufunga ndoa akiwa na umri wa miaka 15 na alikuwa na haya ya kusema;- "Nilipata matatizo mengi baada ya kuolewa. Nilikuwa mtoto mdogo na sikujua ni vipi niwe mke. Kipindi kibaya zaidi kilikuwa wakati nilipopata ujauzito. Hii ni kwa sababu mbali na kumshughulikia mume nililazimika kufanya kazi zote za ndani ya nyumba na pia shambani."

Zipo sababu mbalimbali za ndoa za mapema na hilo hutegemea aina ya jamii. Ukimbizi, umasikini, mila na desturi na kutafuta usalama wa mabinti ni kati ya sababu za ndoa za mapema.

Kuna familia nyingi ambazo huwa zimetumbukia katika dimbwi la umaskini na hivyo ili kukidhi gharama za maisha huamua kuwaoza mabinti zao wakiwa wangali watoto. Katika baadhi ya jamii, wazazi huwa na dhana kuwa iwapo hawataafiki kuwaoza mabinti zao wakiwa watoto, basi hawatapata fursa ya kuolewa katika siku za baadaye.

Katika baadhi ya jamii, hata kama kuna shule za watoto wa kike, lakini kiwango duni cha masomo na ukosefu wa walimu hupelekea wazazi kuona masomo kuwa yanachukua gharama za bure na kuwapotezea watoto wakati.

Lakini kwa upande mwingine baadhi ya familia hupinga watoto wao kwenda shuleni kwa sababu huwatumia mabinti zao kuwa watumishi wa kazi za ndani kwa matajiri ili wakidhi pato lao kwa njia hiyo.

Katika baadhi ya jamii za nchi kama Sudan Kusini, mchumba hufahamisha familia ya binti kuhusu utajiri wake ambapo hujumuisha pesa, dhahabu na mifugo kama vile ng'ombe.

Kwa mfano, Ayen, binti Msudani Kusini anasema hivi: "Mume wangu alimlipa baba yangu mahari ya ng'ombe 75 ili anioe. Hatukuwa tunajuana hata kidogo kabla ya kufungishwa ndoa wala hatukujadili suala hilo wala sikuwa nikijua lolote kuhusu ndoa. Wakati nilipomfahamisha baba yangu kuwa sitaki kuolewa , alisema lazima niolewe kwani anahitaji ng'ombe."

Uchunguzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch umebaini kuwa, katika nchi za Afghanistan, Bangladesh, Malawi, Nepal, Sudan
Kusini, Tanzania, Yemen na Zimbabwe kuna kesi nyingi za ndoa za watoto ambapo watoto waathirika hupata matatizo ya muda mrefu. Uchunguzi huo umebaini kuwa ndoa hizo za mapema hupelekea watoto wengi kupokonywa haki zao kama wanadamu.

Ndoa za watoto ni tatizo sugu kote duniani. Kati ya madhara ya kuozwa mapema mabinti ni kuhatarisha afya, kupata mimba mapema, kuteswa na kupigwa katika ndoa, kuathirika kisaikolojia na kadhalika.

Isitoshe, uchunguzi kote duniani umebaini kuwa, kuna hatari kubwa ya kupoteza maisha watoto ambao huzaa wakiwa na umri wa kati ya miaka 10-14. Aidha madhara mengine ya kuozwa mabinti mapema ni kunyimwa haki ya kuendelea na masomo. Katika nchi kama vile Bangladesh, imebainika kuwa wasichana ambao wanapata fursa za kusoma huwa hawana hamu ya kuolewa wakiwa watoto.

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu, Human Rights Watch limetangaza kuwa, pamoja na kuwa kumepatikana maendeleo katika hali ya wanawake duniani katika siku za hivi karibuni, lakini tatizo la wasichana wadogo kuolewa mapema bado lipo.

Bangladesh ni nchi ya Bara la Asia ambayo ni ya nne duniani kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wasichana wanaoolewa wakiwa wadogo. Kabla ya Bangladesh, nchi zilizo na idadi kubwa zaidi ya watoto wa kike wanaoolewa wakiwa watoto duniani ni Niger, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Chad.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto (UNICEF), katika muda wa mwaka 2005-2013, asilimia 29 ya mabinti wa Bangladesh waliolewa kabla hawajafikia umri wa miaka 15 huku wengine asilimia 65 wakiozwa kabla ya kufikia umri wa miaka 18.

Hapa Tanzania, kwa mujibu wa ripoti ya Unicef ya mwaka jana, mabinti wawili kati ya watano wanaolewa kabla ya umri wa miaka 18. Na asilimia 27 ya mabinti wenye umri kati ya miaka 15 hadi 19 tayari wameshakuwa mama au wajawazito wa mimba ya mtoto wa kwanza.

Zimetajwa sababu kadhaa za kuolewa watoto wa kike Wabangladeshi. Kati ya sababu hizo ni ubaguzi wa kijinsia, wasiwasi wa kijamii pamoja na mila na desturi za nchi hiyo ya Kusini mwa Asia. Aidha sababu nyingine imetajwa kuwa mahari ya juu wanayotozwa wanaume wanaooa wasichana hao wadogo.

Kadhalika umasikini mkubwa katika familia nyingi huwalazimu wazazi waozesha mabinti zao kama njia ya kuwaokoa kwan kuwa huwa hawawezi kujimudu kuwapa chakula na kuwaelimisha.

Bangladesh pia ni kati ya nchi ambazo hukumbwa na mabalaa mengi ya kimazingira kutokana na mabadiliko ya tabia nchi. Ukweli huu umefanya wananchi wa nchi hiyo kukabiliana na hali ngumu ya kimaisha hasa katika mitaa ya mabanda nchini humo.

Human Rights Watch linasema limezihoji familia za Wabangladeshi waliolazimisha watoto wao kuolewa na umri mdogo sana, huku wakitaja sababu kubwa kuwa ni umaskini.

Mmoja kati ya wazazi hao amenukuliwa akisema: "Mimi nilimuoza binti yangu akiwa bado mtoto kwa sababu nilikuwa na njaa."
Mwezi Novemba mwaka 2014, Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio kuzishurutisha nchi wanachama kupiga marufuku ndoa za watoto wadogo katika nchi zao.

Tatizo la ndoa za watoto wadogo ni gumu sana na limeenea kote duniani. Ni kwa sababu hiyo ndio nchi zote duniani zikaahidi kuangamiza tatizo hilo ifikapo mwaka 2030. Bila shaka ili kufikia lengo hilo, serikali zinapaswa kuchukua hatua imara kwa kuzingatia hali ya kila nchi.

Ingawa katika baadhi ya maeneo duniani imedhihirika kupungua idadi ya ndoa za watoto wadogo, lakini kuna baadhi ya nchi ambapo tatizo hilo limeongezeka.

Kwa hiyo, zikichukuliwa hatua za pamoja na kwa msingi wa sheria za kitaifa na kimataifa, bila shaka kutasaidia kutafutiwa ufumbuzi wa kimsingi tatizo la ndoa za watoto wadogo duniani.

*Imeandaliwa na FLORA WINGIA na msaada wa mashirika.

Habari Kubwa