Mwaka 2018 uwe wa ujenzi wa ramani

30Dec 2017
Elizaberth Zaya
Nipashe
Mwaka 2018 uwe wa ujenzi wa ramani

MAMBO ya sasa yaende na wakati ujenzi ni ramani kwani hii ni dira muhimu kwa mafundi wa nyumba, na wahandisi wa ujezi duniani kote.

Watanzania wengi wamezoea kuchimba na kuweka msingi bila kutafuta ramani, kupima na kufanyakazi kitalaam.

Acha hizo . Anza mwaka na mambo mapya jenga kwa ramani fanya mambo kitalaamu.

 

Ramani ni nguzo na ngao ya maamuzi na utekelezaji katika kufikia lengo kabla na wakati wa ujenzi. Nyumba za makazi na majengo yanayojengwa enzi hizi za sayansi na teknolojia zinazoendelea kuleta mabadiliko duniani kote, zimemechangia kwa kiasi kikubwa mapinduzi ya uhandisi ujenzi wa nyumba za kisasa.

 

Lengo kuu la wahandisi wa  ujenzi ni kuifanya dunia kuwa mahali bora na salama kwa wanadamu na viumbe akiwamo mwanadamu kuwa na makazi pamoja na maisha salama.

 

Mtaalamu wa masuala ya ujenzi, Joseph Nyamihonga anasema nyumba bora na ya kisasa ni nyumba ambayo inakidhi mahitaji yote ya watumiaji pasipokuleta kadhia za aina yoyote na kuwa sehemu salama na yenye hamasa kwa mtumiaji au wakazi husika.

 

Anasema zipo sifa mbalimbali zinazopaswa kuzingatiwa kwenye ramani pale unapokutana na wataalamu wa kuzichora.Mojawapo anasema ni ile ambayo inazingatia au ni rafiki wa mazingira.

 

Anasema ramani bora ya nyumba ambayo ni rafiki wa mazingira inampasa mbunifu majengo kuzingatia usalama wa makazi jirani, aina za udongo, milima, mabonde, watumiaji watoto, walemavu,wazee miundombinu pamoja na kufikiria namna ya kuepusha hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa ujenzi unapofanyika na baada ya ujenzi kukamilika.

 

“Yamkini unaweza kuwa umeipenda ramani ya aina fulani lakini ikawa si rafiki wa mazingira halisi ya kiwanja chako.

 

Ni vema ukapata ushauri wa kimazingira kutoka kwa mtaalamu wa ujenzi kwa sababu kutofanya hivyo kutakusababishia gharama za marekebisho kwa siku zijazo,” anaonya Nyamihonga.

 

Jambo jingine analosema linapaswa kuzingatiwa kwenye ramani ambalo pia wataalam wa ujenzi hulipa kipaumbele ni uwezo wa ramani wa nyumba husika na namna inavyoweza kupambana na hali ya hewa.

 

Taarifa za mamlaka ya hali ya hewa katika kuandaa mpango kazi wa kuhakikisha wanafikia viwango husika vya ubora wa nyumba mahali itakapojengwa ni muhimu sana.

 

“Mabadiliko ya hali ya hewa na viwango fulani kuhusu mvua, joto, baridi, mwelekeo wa upepo na matetemeko ya ardhi ni mambo muhimu sana yanayozingatiwa wakati wa ubunifu na uchoraji wa ramani za nyumba,” anasema Nyamihonga.

 

“Nyumba bora lazima iwe na uwezo wa kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa ili iweze kuhimili kwa muda mrefu na kuwa sehemu salama yenye usawa wa mwili na akili za wakazi na wageni husika, ni muhimu ukamshirikisha mtaalamu wa ujenzi ili akupe msaada zaidi ili ramani ya nyumba yako iwe bora  na yenye uwezo wa kumudu changamoto zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.”

 

Jingine analotaja ni umuhimu wa kuzingatia muonekano wa kuvutia wa ramani ya nyumba unayokusudia kuijenga.

 

Anasema kama ilivyo kwenye utofauti wa kimtazamo kwenye mambo mengine, hata mwonekano wa nyumba huwa na mtazamo tofauti kulingana na haiba ya mtu mmoja na mwingine.

 

Mwonekano wa nyumba hutegemea zaidi  mtazamo wa mwenye nyumba pamoja na mbunifu wa ramani za nyumba ambao unaendana na mazingira inapojengwa nyumba na kwamba uzuri na mvuto wa jengo  unatokana na utashi wa mtu mwenyewe anapenda nini.

 

“Nyumba bora ni lazima iwe na uwezo wa kuvutia na ikushawishi wewe na wengine kuendelea kuitazama na ikutie hamasa zaidi ili uendelee kuishi kwenye nyumba hiyo, kuifanya iwe na mwonekano mahiri  kunahitaji fikra na mtazamo wa wahusika kufikisha mawazo kwa mtaalamu wa mambo ya urembo wa nyumba kwa hali ya umakini na kufanya hivyo kutakusaidia upate ushauri bora ambao utakuwezesha kuipenda nyumba yako siku zote,” anasema Nyamihonga.

 

 

Habari Kubwa