Mtokee kimyakimya

16Apr 2017
Mary Geofrey
Nipashe Jumapili
Mtokee kimyakimya

KATIKA maisha yetu ya kila siku, hakuna binadamu anayependa kuona akishindwa katika mambo mbalimbali anayofanya au anayotaka kufanya.

Katika suala la uhusiano, mwanamke anapanga kumpata mume anayemfaa, na wanamume hivyo hivyo anataka kumpata yule anayemtamani.

Leo tunaangalia mbinu ambazo mwanaume anaweza kuzitumia kupata mwanamke anayempenda ili awe mke mwema.

MAMBO YA KUFANYA
Pale unapokutana na mwanamke anayekushtua moyo na uanatamani kuwa mke wako, kwanza hakikisha unaondoa papara ya kuomba namba ya simu. Epuka kuonekana una shida ya kumuhitaji kimapenzi.

Jiwekee mipaka ya kuonyesha unataka urafiki pekee, yaani lafiki wa kuchati nae tu kwenye mitandao na kumsaidia mambo ya maendeleo.

Endapo akikupatia namba, usimtafute siku hiyo hiyo, subiri hata wiki moja halafu mpigie. Siku hiyo msalimie tu na hapa uangalie na muda ambao unadhani mtu anakuwa huru.

Usipige simu asubuhi sana au mchana au usiku sana, jaribu kutumia muda unaohakikisha hawezi kukuambia yupo bize na shughuli zake.

Hakikisha kila siku unamtumia ujumbe mfupi wa maneno, ikiwezekana mara tatu asubuhi, mchana na jioni na wenye uchache wa maneno.

Epuka kuzungumza au kumtumia ujumbe wenye maneno ya mitaani ambayo itampa picha mbaya ya kuwa wewe ni mtu ambaye hujiheshimu.

Kuna maneno kama’ oya umeshindaje’, ‘vipi mwana’ ni maneno ambayo yanakutambulisha huna heshima na hujitambui.

Jenga urafiki naye wa kudumu kiasi kwamba awe anakukumbuka mara kwa mara na pale ukisahau kumsalimia yeye akumbuke.

Ukiona hajibu ujumbe wako naweza kumtumia muda wa maongezi lakini siyo kila siku, ni mara moja moja na yeye ataanza kukuona unamjali.

Muombe utoke nawe ‘out’ na akikubali basi mpeleke sehemu tulivu na si kwenda baa ambako kuna miziki na msongamano wa watu.

Mkiwa eneo la utulivu zungumza naye zaidi mambo ya maisha na changamoto zake, epuka kuzungumzia mambo ya mapenzi wala mpenzi wako wa zamani.

Mkimaliza mpe nafasi ya kuondoka huku ukimtakia heri nyingi, hakika atakumisi na kuyawaza yale mliyoyazungumza na utakuwa umejiongezea nafasi kuwa mwanaume bora.

Baada ya urafiki wa kama miezi miwili hivi, hapo sasa mtamkie wazi wazi kwamba unampenda tangu muda mrefu. Mwambie kwa heshima na unyenyekevu ili ajione kama ndege tausi.
Na mbinu hizi zinaweza kukufanikisha kwa asilimia 100 kumpata mwanamke ambaye anajiheshimu na anayejitambua.

Ukiona wewe unafuata mbinu hizi, lakini yeye tayari amesema maneno mengi ya mapenzi na kukusukuma useme jambo hilo, huyo muangalie sana kwani hakufai.

Habari Kubwa