Mtatiro: Ipo siku tutashinda mgogoro wa CUF

03Jan 2018
Sabato Kasika
Nipashe
Mtatiro: Ipo siku tutashinda mgogoro wa CUF

KWA muda mrefu sasa Chama cha Wananchi (CUF) kimekuwa katika mgogoro wa kiuongozi, ambao haijulikani lini utaisha baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu nafasi yake ya uenyekiti wa taifa na kisha kuamua kurejea tena katika nafasi hiyo.

Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Julius Mtatiro.

Hatua ya Prof. Lipumba kurejea katika nafasi hiyo ilisababisha kuwapo mgogoro na kuibuka kwa makundi mawili ndani ya chama hicho yanayopingana likiwamo linalounga mkono hatua yake hiyo na lingine kumpinga na hivyo kuifanya CUF kupasuka katikati.

 

Kundi linalomuunga mkono halitaki chama kuwa ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na lile linalompinga ambalo linaongozwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad liko katika umoja huo.

 

Julius Mtatiro, Kaimu Mwenyekiti wa CUF yuko upande wa Katibu Mkuu Hamad na pia ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii nchini, ambaye anaamini kwamba ipo siku upande wao utaibuka na ushindi.

 

“Mgogoro wa kiuongozi unaoendelea katika chama hiki lengo lake kubwa ni kuua nguvu ya Ukawa, ambayo imechangia kuifanya CUF iwe na wabunge na madiwani wengi tofauti na miaka ya nyuma na mimi siwezi kukubali hilo litimie,” anasema na kuongeza:

 

“Niseme kuwa pamoja na vita hii vinavyoendelea nina uhakika ipo siku CUF ya upande wetu itaibuka na ushindi, kwani tuna wabunge, madiwani wengi na wanachama wanaunga harakati za chama hiki ndani ya Ukawa.”

 

Mtatiro anasema vyama vya siasa kuungana huwa vina malengo makubwa zaidi ikiwa ni kupambana na chama tawala katika kuleta mabadiliko kwenye sekta mbalimbali na hasa zaidi katika kukitoa madarakani kwa njia ya kidemokrasia.

 

Kaimu Mwenyekiti huyo anabainisha kwamba mchakato wa Katiba mpya uliwaunganisha viongozi baadhi wa vyama vya upinzani na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao umekwenda mbali zaidi.

 

Anasema Ukawa umekwenda mbali zaidi kwa kutaka kuleta mabadiliko katika nchi baada ya kusimamisha mgombea mmoja wa nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

 

“Mbali na kuweka mgombea mmoja wa nafasi ya urais, vyama pia viliachiana majimbo na kata katika uchaguzi huo na kuifanya CUF kwa mara ya kwanza kuwa na wabunge wengi, madiwani wengi na kuongoza baadhi ya halmashauri nchini.

 

“Mimi si kiongozi wa Ukawa na ni mwanachama muhimu wa Ukawa na ninaamini katika mabadiliko ya kimfumo hapa nchini. Siamini kwamba Ukawa itakufa kama ambavyo baadhi ya wenzetu wamekuwa wakitaka ife,” anasema.

 

Mwanasiasa huyo anafafanua kuwa bila Ukawa, CUF isingefikisha idadi kubwa ya wabunge na madiwani ilionao sasa, hivyo yeye na viongozi wenzake wataendelea kuungana na vyama vinavyounda umoja huo na kuhakikisha wale wanaotumwa kuwadhoofisha wanashindwa.

“Ndani ya Ukawa, CUF ina wabunge 10 wa kuchaguliwa Tanzania Bara, wakati kule Zanzibar wapo 23, viti maalum wapo wabunge 10, jumla yao ni 43, huku madiwani nchi nzima wakiwa ni 306,” anasema.

 

HALMASHAURI

 

Mtatiro anasema kuwa halmashauri zinazoongozwa na CUF kwa ushirikiano na Chadema ni tano na pia CUF inaongoza miji midogo sita nchi nzima na kwamba hayo yote yametokana na kuwa ndani ya Ukawa.

 

“Iwapo tutaamua kutoka ndani ya Ukawa tutarudi kwenye sifuri kama ilivyokuwa miaka ya nyuma na ndivyo baadhi ya wenzetu wanavyotaka na sisi hatuwezi kukubali upuuzi huo kwa sababu lengo letu ni kuongoza nchi,” anasema.

 

Anabainisha kwa kusema kuwa wanaopingana na upande wa Katibu Mkuu ndani ya CUF hawana lengo la kushika dola bali wanatumika tu.

 

Anasema watu hao hawataki Ukawa kwa sababu wanajua kwamba umoja huo ni ushindi ambao wao wasingependa utokee.

 

“Ukawa inapozidi kujiimarisha watu wajue mikakati zaidi ya kuidhoofisha inapangwa, ili kama siyo kusambaratika bado idhoofike na kutokuwa tishio zaidi kwa watawala,” anasema na kuongeza:

 

“Wapo baadhi ya watu waliowahi kufanya utafiti wao baada ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kupata taarifa kutoka vyanzo vyao wanavyovijua wenyewe kwamba CUF ilipata hasara baada ya kuwa ndani ya Ukawa.”

 

Kaimu Mwenyekiti huyo anasema watu hao walidai kwamba ni ukweli usiopingika kuwa kupitia Ukawa, CUF ilipata hasara kubwa kuliko faida kutokana na kukosa ruzuku inayotokana na kura za urais kwa kutokusimamisha mgombea urais.

 

Anabainisha walidai kwamba kura za wabunge zinazotoa viti maalumu waliofaidika ni Chadema kutokana na kushinda viti vingi vya ubunge na udiwani kwa vile wana majimbo 130 kupitia Ukawa.

“Mbali na hilo wakatoa sababu yao nyingine kuwa kugawanyika kwa kura za wabunge na madiwani wa CUF ambao Chadema nao walikuwa na wagombea wao na hata katika majimbo walioshinda CUF kati ya 10 mengine yalikuwa na wagombea wa Chadema likiwamo lile la Mtwara Mjini na mengineyo,” anasema na kuongeza:

 

“Eti kutokana na hasara iliyopatikana mwaka 2015 ni vyema wana CUF kujitafakari na kujiondoa ndani ya Ukawa kukijenga chama kisiasa kwa vile CUF kuwa ndani ya Ukawa ni sawa na kuiua kisiasa na kuipaisha Chadema.”

 

APONDA

 

Mtatiro anaponda utafiti huo na kusema kuwa walioufanya walilenga kuua umoja huo, kwa madai kwamba hakuna mwaka wowote wa uchaguzi ambao CUF ilishafanikiwa kupata wabunge na madiwani wengi kama 2015.

 

Anasema ni wakati muafaka sasa kwa CUF kulinda matunda waliyopata wakiwa ndani ya Ukawa badala ya kubeza kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakifanya kwa lengo la kuunufaisha upande mmoja.

 

“Wale ambao wanataka CUF itoke katika Ukawa wana lengo la kuturudisha kwenye sifuri ambako hatukuwa na wabunge wengi na madiwani wengi kama ilivyo sasa, hivyo tuwapinge kwa nguvu zetu zote na wajue kuwa hatutoki Ukawa,” anasema.

 

Habari Kubwa