Mnunuzi, mlaji wanalindwaje kisheria?

17Feb 2017
Denis Maringo
Nipashe
Mnunuzi, mlaji wanalindwaje kisheria?

MAANA halisi ya biashara, iwe kwa msomi ama yule asiyewahi kutia mguu darasani ni mabadilishano ya fedha kwa bidhaa au huduma fulani.

Mauziano ya bidhaa ama huduma ni jambo linalofanyika kila wakati, takribani kila mahali.

Utaratibu huu watu ndani ya jamii wanalazimika kutegemeana kwa sababu ya uhitaji kwa vile mtu fulani anacho kitu ambacho mwingine hana (na huyu aliyenacho hana kitu ambacho huyu mwingine anacho).

Mazingira hayo, huzaa mahusiano ya kibiashara ambayo wanazuoni wa masuala ya historia na biashara wanatujuza kuwa ulianza zamani za kale (maelfu ya miaka iliyopita) hata kabla ya kugunduliwa kwa sarafu na fedha.

Awali biashara ilifanyika kwa utaratibu wa ubadilishanaji wa bidhaa kwa bidhaa (maarufu kama barter system). Kupitia mfumo huu wa kiuchumi, mkulima angeweza kumpa mfugaji debe la nafaka naye akampatia maziwa, ng'ombe na kadhalika.

Hata sasa matumizi ya fedha yametawala kama daraja la ubadilishanaji wa huduma na bidhaa. Kuna watu hutokea wakaafikiana tu na kuridhiana kwa mmoja kupokea kitu badala ya fedha baada ya kumtendea mwenzake jambo fulani lenye manufaa.

Nadharia hii hujulikana pia kisheria na kwa lugha ya kilatini kama quid pro quo, yaani hakuna chenye manufaa kitokacho bure pasipo kingine kuingia. Nadharia hii imejumuishwa pia katika vifungu vya sheria yetu ya mikataba.

Ni mara ngapi (mathalani wewe mwenyewe) umewahi kuhudumiwa kwa kiwango kisichokidhi matarajio yako? Ama ni mara ngapi umewahi kuingia 'mkenge' kwa kuuziwa bidhaa duni na zisizokidhi kiwango kinachokubalika?

Jiulize pia, unakumbuka nyakati fulani umewahi kutapeliwa ama kuona mwenzako 'akiingizwa mjini' kwa kuuziwa mali ambayo ni tofauti kabisa na vile alivyoonyeshwa ama kutangaziwa?

Basi kama hujawahi kutapeliwa au kupoteza fedha zako kwa bidhaa duni ama mbovu basi una bahati sana. Lakini ukweli ni kwamba kila uchao, maelfu ya watu wanatapeliwa.

Na tatizo hili liko dunia nzima, lakini kwa Tanzania limekithiri, mijini na vijijini. Tuangalie sasa Sheria zikoje katika mambo kama haya.

B. SHERIA ZA KUMLINDA MLAJI; MNUNUAJI BIDHAA/HUDUMA

Tanzania, kama ilivyo nchi nyingine yoyote, ina sheria nyingi, kila mojawapo ikilenga kufanikisha lengo fulani la kitaifa.

Ndiyo maana zipo sheria mahsusi za kupambana na uhalifu, kulinda rasilimali za taifa, kusimamia makusanyo, mapato na matummizi ya fedha za umma, masuala ya kiafya, na kadhalika.

Katika masuala ya kibiashara, zipo sheria nyingi pia-nyingine zikilenga kuinua ustawi wa kibiashara, mathalani sheria ya kampuni, benki na bima, masuala ya zabuni, ushirikiano baina ya serikali na Sekta Binafsi (PPPs) na hata kuwalinda watu wanaofilisika.

Kwa upande wa mlaji (wananchi wanaotoa fedha zao ili wanunue bidhaa ama huduma fuluni) zipo sheria mahsusi zinazowalinda pia, na hiki hasa ndicho kiini cha mada yetu leo katika safu yetu hii. Kwa ujumla wake sheria hizi hujulikana kimombo kama ‘consumer protection laws’ (Sheria za kumlinda mlaji).

Nikuombe tu kuwa neno 'mlaji hapa' kwa kadri litumikavyo kisheria halimaanishi mtumiaji wa bidhaa ziingiazo mdomoni kama vyakula, vimung'unywa kama pipi na bazoka (Chewing gums), vinywaji na kadhalika.

badala yake unapaswa ulichukulia kwa tafsiri yenye maana pana zaidi inayojumuisha takribani kila aina ya bidhaa ama huduma ambayo wewe na mimi huzilipia ama kuzitumia kila siku.

Ndiyo kusema basi, sheria za kulinda 'mlaji' zinanuia kulinda fedha, afya na hata heshima ya wanunuzi wa bidhaa za vyakula sokoni, madawa, nguo madukani, vifaa vya elektroniki na digitali kama simu, seti za runinga, redio, kamera, na kadhalika.

Yule anayenunua gari, bodaboda, vipuri, matairi, kalamu, na kadhalika naye ni 'mlaji' kwa matumizi ya neno hili katika sheria hizi. Na sheria za kumlinda mali haziishia katika bidhaa zinazoonekana kwa macho tu.

Na wala haziishii katika bidhaa ambavyo ubora ama uduni wake hutokana na utambuzi ufanywao na milango yetu ya kifahamu kama chumvi na sukari uwezavyo kuvilamba kwa ulimi au santuri ya muziki uwezayo kuisikiliza kwa masikio yako, au mkanda wa filamu uwezao kuukodisha na kuutazama nyumbani mwako, na hata mpira wa kiume ambao yule anayeununua atatambua ubora ama kasoro zake za kiafya baada ya kuutumia na hivyo kuwasilisha malalamiko katika mamlaka husika, na hata mahakamani kama madhara yametokea.

Sheria za kumlinda mlaji zinahusika pia na kumlinda mtumiaji wa bidhaa zisizoonekama kwa macho wala kugusika (intangibles).

Tumezoea kuziita 'bidhaa' hizi kwa jina la 'huduma' (kimombo services), tofauti mathalani na kitu kama chungwa ambacho waweza kukushika kwa mikono yako (tangible goods).

Ndani ya kundi hili la huduma, mifano mzuri ni kama huduma ya muda wa maongezi na vifurushi vinavyouzwa na kampuni za simu, huduma za utumaji na upokeaji fedha, huduma za usafiri, huduma za tiba, elimu, mawakili, uhasibu, ushauri wa kitaalamu (Consultancy) na ushauri nasaha (Counselling) na kadhalika.

Mambo mengi katika yote haya hufanyika kibiashara kwa mtu kulipia fedha na kupewa huduma anayoitaka.

Sheria za kumlinda mlaji zinaingia hata huku kwa sababu udanganyifu ama utoaji huduma chini ya viwango ni suala ambalo liko kila mahali hasa ikizingatiwa pia wafanyao shughuli hizi pia ni watu na si malaika.

Kama tulivyodokeza hapo juu. Sheria hizi ziko nyingi, lakini nitazigawa katika makundi mawili makubwa. Mosi, zipo sheria zinazomlinda mlaji kwa uwepo wa vifungu fulani ndani ya sheria inayohusika na wataalamu ama kundi la watoa huduma za aina fulani.

Takribani kila sheria inayotengeneza taratibu za usajili na udhibiti wa wanaaluma, wafanyabiashara ama watoa huduma fulani inakuwa na kipengele ama vipengele vya udhibiti ili kulinda hadhi ya wahusika na wakati huo huo kuilinda jamii inayotegema huduma za kundi hili.

Sheria za usajili wa madaktari, wahandisi, mawakili, walimu, uanzishwaji wa shule binafsi, wahasibu, mawakala, madalali na kadhalika, sheria zote zina vifungu mahsusi kwa udhibiti kwa kukataza mambo fulani yasifanyike ili kwamba anayeyafanya aje kuwajibika ama kupokwa leseni yake anapokiuka ama kumuumiza mlaji (yule anayefuata huduma kwake).

Kundi la pili, ni la uwepo wa sheria mahsusi katika kudhibiti jambo fulani la kibiashara ili kuwalinda walaji, bila kujali nani anatoa huduma hiyo.

Mathalani, Sheria ya Mawakili inamzuia Wakili kutokuwa mkweli ama kumhadaa mteja wake, mathalani katika masula ya fedha na nyaraka. Utaona kuwa sheria hii inawagusa mawakili tu na huwezi kumchukulia hatua mhandisi ama tabibu kwa kutumia sheria hii.

Sasa chukulia sheria yetu kuu inayodhibiti jinai za aina zote. Sheria hii itwayo Kanuni ya Adhabu (Sura ya 16) inatamba makoa mbalimbali na kuyafafanulia adhabu zake.

Itokeapo mwanataaluma fulani akamtapeli mteja wake mamilioni ya fedha, suala hili ni wizi wa kuaminika kwa sababu aliyetoa fedha aliwekewa mazingira ya kuaminiwa kuwa atatoa fedha ali apate huduma fulani na ikawa kinyume.

Basi, vifungu husika katika Kanuni ya Adabu na sheria za aina hii zinazomgusa kila mtu nchini vinaweza kumnasa mtu yeyote ndani ya nchi hii bila kujali kama ni daktari, wakili, mfanyabiashara, dalali, kondakta wa basi, mwalimu, askari na kadhalika.

Hizi ni aina ya sheria zinazomhusu kila mtu, japo inawezekana pia mtu huyu akaadhibiwa na mamlaka husika chini ya sheria nyinginezo, mfano kunyang'anywa leseni ya biashara kama duka ama usafirishaji, utoaji wa tiba za jadi na tiba mbadala, na kadhalika.

Utaona kuwa sheria fulani inaweza kumwadibu mlengwa muuzaji au mtoa huduma, lakini kwa mapana yake zinakuwa zimetungwa ili kumlinda mlaji asitapeliwe ili pia jamii iendelee kudumishiana uaminifu katika mahusiano ya biashara.

Denis Maringo ni mwanasheria aliyeko Dar es Salaam. Mawasiliano: Simu: 0719270067; barua-pepe: [email protected]

Habari Kubwa