MJUE SHEMSA HAKIM KHAMIS: Dereva teksi mwanamke pekee Zanzibar

21Apr 2017
Rahma Suleiman
Nipashe
MJUE SHEMSA HAKIM KHAMIS: Dereva teksi mwanamke pekee Zanzibar

MARA nyingi mtu anaposikia kuna Umoja wa Madereva wa Teksi, wazo linalomjia mara moja kichwani ni kwamba wanachama wake wote ni wanaume.

Dereva teksi Shemsa Hakim Khamis, mkazi wa Chanjaani Kisiwani Pemba.

Lakini kwa Zanzibar, Jumuiya ya Madereva waTeksi - Pemba yenye wanachama 40, mmoja wao ni mwanamke, ambaye kwa muda wa miezi sita sasa amekuwa akifanya kazi hiyo ya kuendesha teksi.

Huyo ni Shemsa Hakim Khamis, mkazi wa Chanjaani Kisiwani Pemba, ambaye kituo chake cha kusubiri abiria ni ni Kiwanja cha Ndege cha Karume, eneo la Chakechake. Shemsa (40), ambaye haiba yake ni mrefu kiasi na mwenye mwili wa wastani, vazi lake kuu ni ama baibui au dera akiwa amwejifunga mtandio kichwani, anasema anaifurahia kazi hiyo, licha ya kuwa wakati anaanza biashara hii walikuwa wakimshangaa.

“Siku ya kwanza watu walinishangaa na hata baadhi ya majirani na ndugu wa familia, walikuwa wakimlaumu mume wangu, kwanini ameniruhusu kufanya kazi hii wakati tayari mimi na mume wangu tulikushakubaliana,” anaeleza Shemsa.

“Kwa kweli namshukuru mume wangu, kwa sababu wapo baadhi ya wanawake hapa kisiwani Pemba wanataka kufanya kazi, lakini wanakatazwa na waume zao na huishia kuwa mama wa nyumbani, kila kitu asuburi kuletewa na mume,” anaeleza dereva huyo.

Anasema kuwa watu wengi walikuwa wanaomuona katika anachokiita ‘amekengeuka’ kwa kuacha kufanya majukumu ya familia, wakiamini kazi hiyo hutakiwa kufanywa na wanaume.

Zanzibar kunakadiriwa kuwepo zaidi ya wanawake 50 wanaoendesha magari yao binafsi, lakini kwa udereva wa teksi, Shemsa amekuwa wa kwanza.

Dereva huyu wa kike, anafanya biashara ya kusafirisha wageni (abiria) katika maeneo mbalimbali ndani ya Pemba, jambo ambalo limekuwa kivutio kikubwa kwa wageni wanaofika kisiwani humo na wanapohitaji usafiri.

ALIVYOANZA

Mama huyo anasema alijiunga na kazi hiyo ya udereva wa teksi baada ya dereva aliyemuajiri kuendesha gari yake aina ya Toyota –Noah, kushindwa kuwasilisha fedha alizokuwa akizipata kutoka kwenye biashara hiyo ya gari.

“Mwanzoni nilimuajiri kijana mmoja na nikampa gari hii, lakini tangu alipoanza kazi muda wa miezi minne, hakuniletea hata shilingi moja, wakati siyo makubaliano yetu,” anasimulia.

Anasema, mbali na hilo alikuwa halitunzi gari katika namna inavyotakiwa, hata kuna wakati ilimlazimu kufanya matengenezo makubwa yaliyomgharimu fedha zaidi ya shilingi milioni moja. “Kila siku gari imekuwa ikifanya kazi, lakini mapato hayaonekani.

Nkimuuliza mbona fedha huniletei? ananiambia ‘biashara ngumu’ hakuna wateja jambo ambalo sikuridhika nalo,” anasimulia Shemsa.

Mama huyo anasema tangu aanze kazi hiyo mwaka jana, tayari ameshajizolea umaarufu mkubwa kisiwani Pemba na kuwa kivutio kwa wageni, kwani katika safari zao wasafirishwe naye.

Shemsa anasema kuwa kazi hiyo ya udereva hakuisomea chuoni, bali alifundishwa na mjomba wake na hatimaye kutimiza vigezo vilivyompatia leseni ya udereva, ingawaje anakiri mwanzo wa kujifunza kazi hiyo ilikuwa ngumu kwake.

Anasema tayari ameshapata mafanikio mengi kutokana na kazi hiyo, ikiwamo fedha za kuendesha maisha ya familia yake na matumizi mengine, akijiondaa katika kumtegemea mume wake.

 “Kwa kweli kazi ya udereva wa teksi ni kazi kama kazi zingine na wala haimbagui mwanamke wala mwanaume, lakini kutokana na mifumo dume jamii, inadhani kuwa hii ni kazi ya wanaume pekee,”anasema Shemsa.

CHANGAMOTO

Mama huyo anasema kuna wakati anakumbana na changamoto, ikizingatia biashara ya teksi ni ya msimu na kuna kipindi wageni wanaotumia teksi huwa wachache, hali inayofanya biashara yao kudorora.  “Kama hivi sasa, muda mrefu nipo hapa stendi nasubiri wateja, kwa sababu siyo msimu wa wageni wengi.

Lakini, msimu wa wageni hasa kipindi cha utalii, biashara huwa nzuri, napokea wateja mpaka wengine nawagawia madereva wezangu,” anaelezea mama huyo.

Anadokeza dhamira yake kwamba anakusudia kununua gari nyingine nzuri, ili kuwavutia wateja na kuongeza kipato, kwani anasema njia hiyo ndiyo utamsaidia kumkomboa kiuchumi.

Shemsa ambaye elimu yake ni ya sekondari kidato cha pili, anasimulia kuwa mbali na udereva, pia anapika vyakula mbalimbali vya biashara. Ushauri wake kwa kinamama wenzake ni kwamba waache kuchagua kazi kwa madai kuwa wanawake hawawezi kuzifanya jambo analosema siyo kweli.

Ili kupanua wigo na kuinufaika na mapato ya kujitosheleza, mama huyo pia anajihusisha na kupika vyakula mbalimbali zikiwamo chapati, keki, vileja ambavyo hutumia, sana visiwani Zanzibar na maandazi, ambapo  soko lake zaidi lipo katika hoteli na migahawa iliyomo  kisiwani humo.

Anasema ni biashara inayomuingizia kiasi kikubwa cha fedha zaidi, kuliko hata anachokipata katika biashara ya teksi.

Biashara ya teksi anasema ni nzuri na kuna wakati kwa wiki moja inamuingizia maslahi ya wiki ikiwa katika kiwango mara mbili ua kima cha chini cha mshahara wa Zanzibar, inagawje kuna wakati inakuwa ngumu kwa kuambulia wastani wa Sh. 30,000 kwa wiki .

Mafanikio haya makubwa anasema yamepatikana pia kutokana na ushirikiano  mzuri  anaopata siyo tu kutoka kwa maderava wenzake bali pia kutoka kwa wateja ,jamii na hata familia yake akiwamo mume wake ambaye amekuwa akimuunga mkono.

 “Kwa kweli namshukuru mume wangu kwa sababu wapo baadhi ya wanawake hapa kisiwani Pemba wanataka kufanya kazi lakini wanakatazwa na waume zao na huishia kuwa mama wa nyumbani kila kitu anasubiri kuletewa na mumewe.”anasema.

FAMILIA JE?

Licha ya kufanya kazi hiyo, Shemsa hutenga muda wa majukumu yake kuhudumia familia yake na kuhakikisha kabla ya kwenda kazini, anakuwa ameshafanya usafi wa nyumba na huduma nyingine za kifamilia.

Anasema hilo linawezekana, kwa sababu katika kazi ya udereva  wa teksi wamepangiana zamu, ambayo   kila dereva anatakiwa kufanya kazi siku mbili na nyinginezo anapumzika, jambo linalompa muda wa kuhudumia familia yake.

WENZAKE ‘WAMPA TANO’

Saidi Abdallah, dereva wa teksi kisiwani humo, anasema kazi ya udereva wa teksi ni sawa na nyingine, hivyo anapongeza juhudi za mwanamke huyo, huku wakisifu uendeshaji wake kuwa ni mzuri ametulia na ana nidhamu ya kutosha katika taaluma hiyo.

Rai ya dereva Abdallah, ni kwamba aendelee kulinda heshima yake na kufanya kazi kwa bidii, kwani wateja wengi hasa wanawake wamekuwa wakimhitaji kwa ajili ya safari zao.

Anashauri kwamba, pindi anapopata wateja ambao ana wasiwasi nao, ni vyema asiwe tayari kuwachukua kwani watavunjia heshima yake. Abdallah anadokeza kuwa kuna wateja wasio waminifu na wanaweza kutumia kigezo cha jinsia yake kutaka kumdhalilisha.

Katibu wa Jumuiya ya Usafirishaji, Madereva,Utingo na Umiliki wa Magari, Mkoa wa Kusini Pemba, Hafidh Mbaraka Salum, anasema kazi ya udereva wa  teksi imekuwa ngumu kutokana na baadhi ya wahalifu kutumia usafiri huo katika malengo yao yasiyo na mema.

Huku akitoa sifa kemkem kwa dereva Shemsa, Salum anawataka wanawake wengine wajifunze kazi ya udereva, kama somo kutoka kwa mwenzao, ili waweze kujiajiri na kujikwamua kiuchumi, hali inayowaondoa katika lindi la umasikini na hasa ikizingatiwa kuwa, wanawake wengi wana vipato vya chini ikilinganishwa na wanaume.

KINAMAMA WANAHARAKATI

Wanaharakati wa Kutetea Haki Za Wanawake Zanzibar, wanampongeza mwanamke huyo kujiajiri kupitia kazi ya udereva wa teksi na anasema ni maendeleo makubwa kwa Wazanzibari.

Mzuri Issa ni Mratibu wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kwa upande wa Zanzibar , anasema kwa miaka mingi ajira zilibaguliwa na zile zilizoonekana kutokuwa na tija ndizo za wanawake na kinababa ndio wameachiwa za tija, kama vile kazi za nyumbani.

Mratibu huyo anasema, mara nyingi wanawake wanapohitaji au kupata kitega uchumi, huwaachia wanaume afanye kazi na wao wanasubiri kuletewa mapato na mara nyingi wanaishi katika kudhulumiwa.

“Jambo muhimu katika kuimarika kwa wanawake hasa masuala ya mabadiliko, kuna hatua za kumuona mwanamke ameweza kwa kiasi gani hasa katika kujikomboa kiuchumi,” anasema Mzuri.

Anafafanua kuwa, kitendo cha mwanamke kujiajiri katika kazi hiyo ya Shemsa, ni uthubutu na hatua kubwa iliyofikiwa, kitu ambacho hakijazoeleka kwa wanamke wengi, kwani wamekuwa wakipingwa katika jamii.

“Huyu mwanamke ni wa kupongezwa, kwani ameweza kuvuka vikwazo vya kuimarika kwa mwanamke kiuchumi, lakini pia nampa pongezi mume wake kwa kutomnyima fursa ya kujiajiri, kwani baadhi ya wanaume wamekuwa wakiwanyima fursa wanawake kufanya kazi,”anasema.

Mzuri anaongeza kuwa mwanamke huyo anapaswa kupewa hadhi ya ‘Mama Shujaa’ ili apate moyo wa kutomrudisha nyuma katika kazi yake hiyo aliyojiajiri na kufungua mlango wa wanawake wengine kufuata nyayo zake.

WAZIRI AFUNGUKA

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, ambae naye ni mwanamke, Riziki Pembe Juma, anasema kuwa wanawake wengi wana changamoto ya kupata ajira kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ukosefu wa elimu, ikilinganishwa na wenzao wanaume.

Kutokana na hali hiyo, anasema baadhi yao a wanakabiliwa kunawa na rushwa ya ngono hasa pale wanapoomba ajira katika tasisi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali.

 “Mwanamke huyu ambae amejiajiri katika kazi ya udereva wa teksi ni faraja kwa wanawake kumbe wanawake tunaweza kufanya kazi yoyote na sasa wanawake tubadilike ili kuondosha mitazamo potofu kuwa baadhi ya kazi haziwezi kufanywa na wanawake,”anasema Riziki. #

Anaeleza kwamba anachokifanya ni kitu sahihi, hivyo kuendelea nacho na asivunjike moyo na kazi hiyo ambayo inamjengea heshima na kujikwamua na umasikini. Pia anaomba jamii kumuunga mkono kwa kutumia usafiri wake, kwani ni namna ya kuwaunga mkono wanawake wote.

Habari Kubwa