Mimba zinazotolewa zinavyoitikisa Sengerema

23May 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mimba zinazotolewa zinavyoitikisa Sengerema
  • Yashika namba mbili nyuma ya malaria

AKIWA na matarajio ya kufika mbali kimaisha, Naomi Pastory (25), mkazi wa Busilasogwa, wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza, ghafla ndoto zake ziliyeyuka kama mshumaa, pale alipopata ujauzito.

Naomi anasimulia jinsi alivyonasa kwenye penzi zito na kijana mmoja mtanashati (hakupenda jina lake liandikwe gazetini), akidokeza mkasa ulivyo: “Niliamini atakuwa mume wangu. Nikiwa na miaka 18 tulianza kujamiiana kwa siri. Nilikuwa darasa la saba,”

 

Anasema miezi mitatu ilipita tangu waanze uhusiano huo, hakuona siku zake na akapatwa na hofu kubwa. Anasmulia: “Mpenzi wangu alikwenda Dar es Salaam kushughulikia mchakato wa kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.”

Anaongeza: “Sikuwa na mawasiliano naye, niliogopa kuwashirikisha wazazi wangu, ni watu wa dini. Baba yangu ni Mchungaji. Mimi ni mtoto wa sita kuzaliwa. Niliogopa kuwaeleza dada zangu, sikutaka taarifa ziwafikie wazazi wakati ule.

“Miezi ilizidi kwenda, niliogopa jamii itanielewaje itakapojulikana nina ujauzito. Wazazi wengi waliwasihi watoto wao kuiga mfano kwangu,” anasimulia na kuongeza, na kwamba aliamua kumshirikisha rafiki yake ambaye walishauriana na mambo mengi.

“Alinitaka nisiwe na wasiwasi, atanifichia siri yangu. Alinishauri tuitoe, alinipeleka kwa mtu nikapatiwa dawa, majani na mizizi ya miti.

“Nilirudi nikazificha nyumbani, kila nilipotaka kuvitumia, nilihisi sauti ya mama yangu ‘ikipita’ kwenye ufahamu wangu, niliwahi kumsikia akisema ‘kutoa mimba ni hatari, mtu anaweza kufa.

“Sentensi ile ilijirudia mara nyingi kwenye ufahamu wangu. Hofu ilizidi kuniandama. Mwisho nikamueleza wazi mama. Hakuamini, akamueleza baba. Walisikitika mno, waliniuliza kwanini nilificha, niliwaeleza nilihofia yule kijana angenikimbia kwa hofu ya kukamatwa.

“Hivyo, hata yeye asingekuwa makini na masomo chuoni. Niliamini atarejea tujenge familia yetu, jamii ilinilaumu, nilinyooshewa kidole kila nilikopita, maisha yangu yalibadilika,” anasema.

Naomi anasema, hayo yalitokea kipindi alikuwa anakaribia kuhitimu darasa la saba. Anasena, kilichomsaidia kutogundulika mapema ni umbile  lake. Tumbo lake halikuwa kubwa mno na akafaikiwa kuhitimu masomo salama.

Hata hivyo, matokeo yake hayakuwa mazuri, hakuendelea na sekondari. Alilea mimba yake, akajifungua mtoto wa kiume.

Anasema, hatimaye kijana yule alirejea kijijini. Siku moja akiwa ameambatana na wazazi wake, walienda kumuona mtoto. Naomi anasimulia ilivyokuwa:

“Walifurahi mtoto amefanana na baba yake. Aliahidi kumtunza. Waliondoka, wakarejea tena kutoa mahari, lakini tangu alipoondoka hadi sasa mtoto ana umri wa miaka saba, hakurejea tena. Nilipata taarifa ameoa mwanamke mwingine,” anasimulia.

 “Wasiwasi wangu mkubwa niliyo nao, kwa kuwa alitoa mahari, kwa mila zetu wakati wowote anaruhusiwa kuja kumchukua mwanawe. Sipo tayari!” anang’aka.

“Kinachonisikitisha zaidi, alinizalisha, akanitelekeza. Nimelea mwenyewe, hajanisaidia chochote. Hapa Sengerema wasichana wengi wanatoa mimba kwa dawa za kienyeji. Hatuna elimu sahihi ya afya ya uzazi, tunaelimishana wenyewe ‘vibarazani.’

“Sasa hivi katika mahusiano, wasichana wanaona bora kupata Ukimwi kuliko mimba. Wanaume si waaminifu kabisa,” anaeleza Naomi.

Mkasa wodini

Nipashe  ilihamia katika Wodi ya Kimamama katika Hospitali ya Wilaya Sengerema. Hapo katika kitanda kilichoko jirani na mlango wa kutoka wodini, amelazwa kijana, Miriam John (19).

Huyo ana maumivu makali mwilini na anazungumza kwa sauti ya chini, kwamba amelazwa hapo kupatiwa huduma ya kusafisha kizazi.

 “Ni ujauzito wangu wa pili. Ule wa kwanza nao uliharibika,” anasema Miriam, ambaye hata hivyo hakuwa tayari kuweka wazi sababu iliyochangia hali hiyo.

“Daktari hajaniambia sababu. Binafsi sijawahi ama kujaribu au kutoa mimba. Ilitoka nikiwa nyumbani. Nimefikishwa na jamaa zangu hapa hospitalini,” anasema.

Mshauri wa Afya ya Akili, hospitalini hapo, Modesta Masala, anafafanua jambo hilo akisema, kuna kawaida ya wasichana wengi wilayani humo kutoa mimba kwa njia zisizo salama, kaktika usiri mkubwa.

“Hakuna aliye tayari kukiri. Mara nyingi tunawapokea wasichana kati ya umri miaka chini ya 20 hadi 26 kwa tatizo la kuharibika mimba. Tunapowahoji wengi, tunabaini wapo kwenye migogoro na wenza wao.

“Tunadhani pengine ni sababu mojawapo inayowasukuma kuharibu mimba. Binafsi nimewahi kukutana na msichana mmoja akiwa katika harakati za kutoa mimba. Alihofia misimamo ya wazazi, itakuwaje pindi watakapojua ni mjamzito?” anasema Modesta.

Anaendelea: “Nilimshauri asitoe. Alijifungua mtoto akampatia jina langu. Sasa ana mimba ya pili, wengi hufikishwa kwetu wakiwa na hali mbaya.

“Tunakuta wamejaribu kutoa, imeshindikana au imetoka sasa wanahitaji kusafishwa. Japo hawaweki wazi, jukumu letu ni kuokoa maisha, tunafanya kila tunachoweza kuwasaidia.”

Modesta anasema mara kadhaa wameshawakamata wajawazito, wakiwa na mitishamba wodini wakati wakisubiri kujifungua. Anasimulia:

“Kuna za unga (zimesagwa tayari), nyingine ni mizizi, nyingine katika mfumo wa majimaji (akimuonyesha mwandishi wa makala mfano mmojawapo). Wanadai zinasaidia kuongeza uchungu, wajifungue mapema. Tunadhani ndizo zinazotumika pia kutoa mimba.”

Mbinu zinazotumika

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Sengerema (DMO), Peter Mao, anakiri kuwapo changamoto hiyo, akiupa ufafanuzi: “Siwezi kusema kwa kiasi gani. Wengi hawaweki wazi. Tunafahamu wapo wanatumia dawa za asili hudai kupatiwa na waganga wa kienyeji, wengine dawa za hospitali.

“Nimewahi kupata kesi (mkasa) moja ya msichana kutumia kijiti, sijui ni cha aina gani, alijichokonoa, mimba ikatoka.”

Katika hilo mkazi wa Sengerema, Fausta Kimambo, ana ufafanuzi: “Nimepata kushuhudia baadhi ya ndugu zangu wakitoa mimba.  Wanatumia mti wa muhogo, wanauchonga unakuwa na ncha, wanaingiza sehemu za siri na kuchokonoa mpaka mimba inatoka.

“Wengine hukoroga majivu mengi, chai ya rangi yenye majani mengi au spoku za baiskeli. Wapo wanaonunua dawa (anazitaja). Maduka ya dawa muhimu zinauzwa kuanzia 60,000 wanameza nyingi, mimba inaharibika.”

Mtihani  Sengerema

Akizungumza na Nipashe, Mratibu wa Afya Wilaya ya Sengerema, Maria Mgoa, anasema takwimu zinaonyesha zaidi ya mimba 1000 ziliharibika mwaka 2018 wilayani humo na anapngeza: “Lakini haijulikani sababu. Si rahisi kujua, wengi hawaelezi iwapo wametoa mimba au la.”

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Sengerema, Daktari. St. Marie Jose Voeten, anasema kila mwaka wanapokea wajawazito kati ya 9,000 na 10,000 wanaohudumiwa katika kliniki ya uzazi hospitalini hapo.

Anasema, katika hilo mikasa ya kuharibika mimba inashika nafasi ya pili, kati aina 10 ya wagonjwa waliopokewa na kuhudumiwa hospitalini hapo, mwaka jana.

“Takwimu zinaeleza tulipokea wanawake 850, walioharibikiwa mimba (abortion), malaria iliongoza kwa idadi ya wagonjwa 860,” anabainisha.

Anaongeza: “Matumizi ya dawa za asili yapo kwa kiasi kikubwa, huwa wanazitumia katika kipindi cha ‘mashimba-shimba’ (ufanyaji kazi/ vibarua).

“Japo hatujui moja kwa moja mama amepata ‘abortion’ (utoaji mimba) kwa sababu ya dawa hizo, tunao ushahidi wa mjamzito mmoja pekee ambaye alikiri kutoa mimba kwa dawa za asili, 2018.

 “Elimu ya afya ya uzazi ipo chini mno, hawaelewi athari za matumizi ya dawa hizo. Wengi huchelewa kuja hospitalini, hufika wakati tayari chupa imeshapasuka au wakati mwingine mfuko wa uzazi hupasuka, hasa ikiwa mtoto ana umbo kubwa.

“Wakati mwingine kondo la nyuma hutangulia kutoka kabla ya mtoto. Hivyo hufia tumboni. Ni hatari kubwa, wengi huletwa wakiwa na ‘complications’ matatizo. Kwa mfano, tunakuta mimba imetoka, lakini bado kuna kiungo kimebaki ndani,” anaeleza.

Dk. Marie anataja athari mojawapo ya kutumia dawa za asili za uzazi: “Wapo wanaotokwa damu nyingi, kuna wanaopata kifafa cha mimba, maambukizi kwenye kizazi, hizi ni sababu zinazochangia vifo vya uzazi, Sengerema.”

Hatari ilikojikita

“Wilaya ya Sengerema inachangia vifo vingi vya uzazi mkoani Mwanza, mwaka 2017 vilitokea vifo 33, 2018  vifo 27 na kipindi cha Januari hadi April, 2019 vimetokea vifo saba,” anasemaDk. Marie

Anataja sababu, kwamba wengi huchelewa kuanza kliniki, au hufika katika vituo vya kutoa huduma za kujifungua na takwimu zinaonyesha asilimia 39 pekee, ndiyo wahudhuriaji kliniki.

 “Mtoto anapofia tumboni, hali hiyo huweza kusababisha hitilafu kwenye mfumo wa damu wa mama. Kitaalamu tunaita DIC au hupata tatizo jingine ambalo linafanana na hilo. Mama anapopata tatizo hilo, mara nyingi damu ikianza kutoka huwa haikomi, huwa haigandi kabisa,” anabainisha.

Dk. Marie anasema, katika kukabili changamoto hiyo, Wilaya ya Sengerema, sasa imeanzisha mafunzo maalum kuwaelimisha wakunga na waganga wa jadi athari za utoaji mimba kienyeji.

“Tunafuatilia vifo na kuvijadili kwa kina, ili kuchukua hatua zaidi, tumenunua dawa na vifaa tiba vya kutosha. Tunaelimisha kupitia Radio Sengerema na wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHW), kwenye kaya na mfumo wa rufaa umeimarishwa,” anasema Maria.

Sheria ilikosimamia

Julius Titus, Mshauri wa Kisheria katika shirika lisilo la kiserikali nchini la Pathfinder, anasema hakuna sheria nchini inayoruhusu utoaji mimba.

“Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, vinavyoanzia kifungu cha 150 hadi 152 vinazungumzia adhabu ya mwanamke aliyetoa mimba, aliyemtoa na aliyesaidia kufanikisha utoaji mimba.

“Inatamka, anayetoa (mara nyingi ni daktari) atafungwa miaka 14 jela. Mwanamke anayetolewa, atafungwa miaka saba, aliyesaidia kufanikisha utoaji atafungwa miaka mitatu jela,” anafafanua kuwa  ni vigezo vinavyowafanya wanawake kutafuta huduma hiyo kwa siri.

Waziri Ummy

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anasema utoaji mimba usio salama ni changamoto inayochangia asilimia 18 ya vifo vitokanavyo na uzazi.

“Sheria zetu zinakataza kutoa mimba, isipokuwa zinaruhusu ikiwa labda kuna sababu za kiafya, hasa ikiwa ujauzito unaweza kuleta athari kwa afya ya mama au mtoto aliye tumboni.

“Pale mimba imetoka au ametoa, anachosaidiwa ni kusafishwa kizazi. Sasa kwanini watu wanatoa mimba mimi naona kwa sababu hawataki kuzaa,” anasema waziri.

“Ni kosa la jinai kutoa mimba kulingana na sheria zetu, hatujabadilisha sheria, mimi siwezi kuhamasisha ifanyiwe marekebisho.

“Kikubwa kwetu (Wizara) ni kuhakikisha tunahamasisha jamii kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango, mtu aamue mwenyewe azae lini na nani, wapi badala ya kutoa mimba.

“Kama ‘abortion’ imetokea, tuna mwongozo wa huduma baada ya mimba kuharibika wa mwaka 2015 (comprehesive post abortion care), unatumika katika vituo vya kutoa huduma za afya.

“Mama anapatiwa huduma anazostahili, hatuulizi sababu ya mimba kutoka, hatuulizi kwanini amechoropoa, hiyo ni ‘non of our business’ ( si wajibu wetu), akifikishwa hospitalini tunamchukulia kama mgonjwa.

“Siwezi kuwa ‘champion’ (kinara wa kuruhusu utoaji mimba, japo najua zipo nchi zimeruhusu. Kama mtu amebakwa, hatuna namna tena, tutakachozingatia sisi ni kuelimisha njia za kisasa za uzazi wa mpango,” anasisitiza.

Watafiti watamka

Ripoti iliyochapishwwa mnamo Machi 31, 2016 katika mtandao wa Chuo Kikuu cha Guttmacher, Marekani, inakadiriwa kila mwaka wanawake milioni moja nchini wanapata mimba zisizotarajiwa, asilimia 39 zinatolewa.

Ni zao la utafiti uliofanywa na Chama cha Madaktari Bingwa wa Uzazi na Magonjwa ya Wanawake Tanzania (AGOTA), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na wenzao wa Guttmacher.

Pia, inataja utoaji mimba usio salama ni ya pili kuchangia vifo vya kinamama na wasichana.

Takwimu za WHO

Shirika la Afya Duniani (WHO), linakadiria kila mwaka kuna mimba zipatazo milioni 25 hutolewa katika njia zisizo salama, kulingana na ripoti yake ya 2010/2014.

  • Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa barua pepe: [email protected]  na simu: Simu; (+255) 0758 218 013

 

 

Habari Kubwa