Mikakati kuokoa wazazi hii

19Nov 2017
Gaudensia Mngumi
Nipashe Jumapili
Mikakati kuokoa wazazi hii
  • Kuanzisha vituo maalumu nchi nzima, kufuatiliwa hadi kipindi cha 40

MACHI 8, 2017, saa 5:10 asubuhi , mama kijana akiwa na miaka 30, Enina Beria, anavuta pumzi yake ya mwisho duniani, akiwa katika hospitali ya Mkoani iliyoko Kibaha mkoa wa Pwani.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya.

Alikaa Mkoani kwa saa 10 akitokea Mlandizi baada ya kushindwa kujifungua kulikotokana na kupasuka mfuko wa uzazi na kupoteza damu nyingi.

Alijifungua na mtoto wake ni mzima, wakunga na madaktari wameshindwa kumukoa Enenia. Mwanae aliyepewa jina la Tulizo, hatamfahamu mama yake maisha yote, lakini atapata upendo wa baba, kaka zake wawili watakaomkuza na kumsaidia aishi.

Ni simulizi ya kweli inayowahusu wanawake wengi wanaojitoa sadaka kubeba mimba ili kuzaa watoto. Familia na taifa huomboleza vifo vyao ambavyo vingeepukika kama kungekuwa na huduma za kutosha za afya. Leo vifo hivyo vimebakia kuwa kitisho zaidi, kwani wanawake wanapofikiria kupata watoto huona kama ni kujitoa mhanga na kuweka maisha rehani.

Idadi ya wanaopoteza maisha kutokana na matatizo yanayohusisha uzazi imeongezeka kutoka wanawake 426 mwaka 2010 hadi 556 mwaka 2015 kwa kila vizazi hao 100,000,kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya (pichani).

Anasema hata kama angekufa mwanamke mmoja ni jambo linaloumiza na halikubaliki.Anaeleza hayo katika mohojiano na wanahabari wakati wa mkutano na wadau wa maendeleo kutoka Benki ya Dunia na Shirika la Afya Duniani (WHO) wiki hii jijini Dar es Salaam kuzungumzia mikakati ya kudhibiti vifo hivyo.

Katika mahojiano hayo, Katibu Mkuu anasema serikali na wadau hao, wanaangalia mkakati wa taifa wa kupunguza vifo vya mama na mtoto ambao unalenga kuvishusha hadi vifo 220 katika kila vizazi hai 100,000.

“Utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu umebaini kuwa kuanzia mwaka 2010 na 2016 idadi ya vifo vya wanawake wanaokufa kutokana na sababu za uzazi imeongezeka kutoka 426 hadi 556 katika kila vizazi hai 100,000.Nisema hata kama angekufa mmoja katika 100,000 haikubaliki.”

CHANZO CHA VIFO
Anasema sababu kubwa za vifo hivyo ni uzazi pingamizi, kukosekana kwa huduma zinazostahili, ukosefu wa damu wakati wa ujauzito na ule wa kujifungua maambukizi mbalimbali kama VVU , shinikizo la juu la damu na pia zipo sababu nyingine ambazo hazijulikani.

“Sasa tumejiwekea malengo ndani ya malengo endelevu ya kupunguza vifo hivyo hadi 220 ifikapo mwaka 2020 lakini kama tutaweza kuteremka zaidi tutafanya hivyo.” Anasema Dk. Ulisubisya.

MIKAKATI
Kwanza anasema ni kuwasaidia wanawake kupata huduma muhimu kabla ya na wakati wa ujauzito pamoja na wanapojifungua.

Lakini pia kabla ya ujauzito. Watapatiwa huduma ili kushika ujauzito pale wanapohitaji kufanya hivyo. Pia kuhakikisha huduma za uzazi wa mpango zinapatikana kuweka vituo vya huduma ya afya ya uzazi vinavyowavutia vijana ili wazitafute na kuzitumia.

Njia nyingine ni kuwa na vituo na huduma za kusaidia wajawazito karibu na wananchi ili ikiwezekana kila mjamzito ahudhurie kliniki angalau mara nne kabla hajajifungua.

Aidha, anasema kwa upande mwingine imebainika kuwa wajawazito na jamii inaamini zaidi huduma za wakunga wa jadi kwenye uzazi na kusababisha kucheleweshwa kupata huduma bora wakati wa kujifungua.

“Tunataka kuwatumia wataalamu wale wa jadi kuwafundisha kuwa mjamzito anapokaribia kujifungua wampeleke kwenye kituo cha afya akahudumiwe na wataalamu wenye ujuzi wa kutambua viashiria hatarishi mapema na kumpeleka mbele ambako atapata huduma bora na kwa haraka zaidi iwapo atapata matatizo.”

Katibu Mkuu anasema , japo huduma bora za afya zinapatikana zaidi mijini kuliko vijijini, serikali inaona kuwa kuanzia sasa I inashirikiana na wadau kama WB kuweka vituo vya kushughulikia wajawazito vijijini ili kuepuka kusafiri umbali mrefu kuja mijini kufuata huduma hizo.

“Vituo vitakuwa na wataalamu wa afya, vifaa na huduma ili kuwasaidia katika maeneo yao na wale watakaokuwa na shida kubwa zaidi watapewa rufani za kwenda hospitali za wilaya, mikoa, kanda na wenye shida kubwa zaidi watafikishwa kwenye hospitali za kitaifa.”

Aidha, anasema wanakuja na mpango wa kutoa huduma kwa wanawake baada ya kujifungua ili kuendelea kuwaangalia ndani ya kipindi cha wiki sita (siku 42).Hii ni kwa sababu katika kipindi hicho cha siku 40 kunatokea maambukizi mengine na kusababisha wanawake kufariki baada ya kujifungua, anasema.

Aidha, wanawake waliopata matatizo ya mimba kuharibika watapatiwa huduma ili kukabiliana na changamoto zinazotokana na mimba kuharibika kwa kuwa hilo nalo husababisha vifo vya uzazi hapa nchini.

“Aidha tunataka kuweka utaratibu ambao watoto waliozaliwa wanapewa huduma bora za chanjo na tiba. Kwa mfano kuna mkakati unaoangalia magonjwa kama naimoni na kuhara ili yaweze kushughulikiwa kwa pamoja.”

ANGALIZO WATOA HUDUMA
Kuhusu vifo vinavyoweza kusababishwa na watoa huduma, anawashauri wanawake wanaoona kuwa hawakuhudumiwa inavyostahili kuafuata taratibu zilizowekwa kulalamika.

“Wauguzi wana utaratibu, madaktari, watu wa maabara wana kanuni zao, aidha watumishi wa radiolojia nao wanazo kanuni , hivyo zinapokuwa vimevunjwa yapo mabaraza ya kushughulikia malalamiko na uvunjaji kanuni bila upendeleo.

“Lengo letu siyo kusubiri mpaka watu wafanye makosa. Sisi tunafuatilia utendaji kazi kila mara kwa mfano mama au mtoto anapofariki wakati wa kujifungua tunapenda ufuatiliaji ufanyike siku inayofuata ikizidi iwe ndani ya wiki moja na sisi tunapata ripoti kupitia mtandao wetu wa kukusanya taarifa wa Wizara kila siku ili kufuatilia utendaji wa kila mmoja.

Inasema inawezekana kusiwe na ufanisi wa asilimia 100 lakini baada kuimarisha ufuatiliaji simu zitatumika kufuatilia utendaji kazi.

“Hata hivyo hatutaki watendaji wasifanye midhaha na maisha ya watu kwa vile hakuna chenye thamani kuliko maisha.Fundi chuma akiharibu chuma atakichomelea na kukiunda upya lakini mwanadamu akifa hakuna cha kufanya. Kwa hiyo serikali inaweka mazingira yanayowezesha kila mwananchi kupata huduma bora.”

Habari Kubwa