MEJA JENERALI ISAMUHYO: Tumeanza kubadilisha teknolojia mashambani

03Jan 2018
Flora Wingia
Nipashe
MEJA JENERALI ISAMUHYO: Tumeanza kubadilisha teknolojia mashambani

JICHO bado linatizama Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kuona malengo yake mbalimbali yanavyotekelezwa na hasa katika kuinua uwezo na vipaji vya vijana wa taifa hili.

Kilimo cha Vitunguu si Ilula pekee hata Ruvu JKT kinafanyika. Vijana wa JKT wakipalilia vitunguu. PICHA: MTANDAO.

Mengi yameshazungumzwa na Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Michael Wambura Isamuhyo, katika mfululizo wa makala kama alivyonukuliwa kwenye mahojiano katika kipindi cha Dakika 45 kilichorushwa na kituo cha ITV Novemba 13, mwaka huu.

Mtangazaji alikuwa Sam Mahela. Hii ni sehemu ya mwisho ya mahojiano hayo.

 

SWALI: Pengine Meja jenerali, Jeshi la Kujenga Taifa lina miaka mingapi sasa hivi linafufua kambi zake zilizofungwa kwa miaka iliyopita.

Hii ina maana gani kwa taifa, ni gharama zaidi za kuziendesha au ni faida zaidi kiuchumi, ajira na uzalishaji mali?

 

JIBU: Moja ya mambo ambayo yanasababisha kuwapo na dalili za rushwa, watu wanadhani kwamba rushwa inatumika kwa ajili ya kuwaingiza vijana katika national service, ni uhaba wa kazi. Nafasi zinakuwa chache na kadhalika.

Lakini pia manufaa ya national service katika maeneo mbalimbali, kama jinsi nilivyoeleza kwamba wananchi wanaozunguka kambi hizi wananufaika kwa masuala mbalimbali.

Huduma kwa maana ya hospitali, huduma ya usafiri, lakini pia vijana wanakwenda kufanya mafunzo katika kuanzisha masuala ya ufugaji, kilimo bora na hata ujenzi wa nyumba na kadhalika.

Kwa hiyo, ufunguzi wa haya makambi una faida nyingi. Lakini ufunguzi huu unaendana na maagizo ya serikali, na nia njema ya serikali kuhakikisha kwamba kila mkoa katika nchi yetu kunakuwa na kambi za JKT.

Ni bahati mbaya, sasa hivi tuna mikoa karibu 25. Lakini kati ya hizo ni mikoa minane tu haina kambi za national service. Kwa hiyo ufunguzi wa hizi kambi tano una manufaa makubwa kiuchumi pamoja na kijamii.

Kijamii kama nilivyokwisha kueleza kwamba unapokuwa na kambi ya jeshi, kumbuka kunakuwa na wanajeshi, kunakuwa na vijana wanapata posho, hela za chakula zinatumwa pale, wanajeshi wanapata mshahara. Unaona hawawezi kwenda sehemu nyingine, hawawezi kutoka nje ya mkoa.

Lakini pia national service panapokuwa na kambi, kunakuwa na miradi mbalimbali kama ufugaji, kilimo na kadhalika.

Kwa hiyo mkoa unainuka kiuchumi. Lakini pia kama nilivyosema kiuchumi, ndio kama tulivyosema kuanzisha viwanda mbalimbali vidogo ambavyo vinaweza kusaidia hata wananchi wenyewe kupata soko.

Kwa mfano tunapozungumzia kiwanda cha kukamua alizeti, sisi JKT mazao yale hayatoshelezi kuendesha hivyo viwanda. Kwa hiyo inabidi tuchukue kwa wananchi ambao nao wanapata soko.

Niseme kwa ufupi tu kwamba nitumie nafasi hii kumshukuru sana, Rais wetu Rais John Pombe Magufuli kwa jinsi ambavyo amefanya kazi kubwa kwa muda mfupi kuweza kurejesha vikosi vitano.

kulikuwa na gharama nyingi kuviendesha lakini amevirejesha tuliona akikabidhi gari jipya kila kambi, alifungua ofisi mpya nzuri, majengo mapya mazuri, mabweni ya vijana na kadhalika.

Kwa hiyo kwa kufanya hivyo, ametatua tatizo kwa kiasi fulani vijana wetu kupata nafasi.

Kwa hiyo idadi ya wanaoingia JKT sasa itaongezeka kwa hiyo vijana kiasi wengi watapata nafasi ya kujiunga na national service.

 

JKT NA MIGOGORO YA ARDHI

SWALI: Pengine pamoja na maelezo yako muhimu na umetueleza, lakini pia kunakuwapo na malalamiko kuhusu uwepo wa jeshi pale na wananchi pembeni, kwamba jeshi limeingilia maeneo yao.

Wengine hawana uelewa wanadhani kuwa mmeingilia maeneo yao. Je, migogoro inapokuwapo mnatatuaje kama JKT?

JIBU:Kwanza nishukuru kwa swali zuri sana. Migogoro ya ardhi inasababishwa na kile kipindi ambacho Jeshi la Kujenga Taifa linachukua vijana.

Kwa hiyo, ilionekana kwamba mashamba mengi yamekuwa mapori.

Na ukiangalia tangu mwaka 1994 hadi 2013 karibia miaka 20, kambi zilikaa bila kuwa na vijana.

Kwa hiyo baada ya hayo mashamba kuachwa, wananchi wakaanza kuomba kwamba watalima kwa muda, lakini wengine ambao siyo waaminifu wakaamua kukaa kwa muda mrefu na kujenga.

Lakini tatizo nililokuwa ninaliona ilikuwa ni namna makambi haya yalikuwa yanapatikana.

Ilikuwa ni agizo la serikali, unakwenda mamlaka za mkoa za serikali, unawaomba kwamba tunahitaji eneo la national service wanalitafuta, mnapewa inakuwa ni mwisho.

Wakati huo ardhi ilikuwa kubwa na wananchi walikuwa wala hawana shida na ardhi. Kwa hiyo, baada ya kuonekana tatizo hilo lipo, nadhani unaelewa ardhi wameweka utaratibu kwamba maeneo yote ya serikali ni lazima yapimwe unapewa hati milki na itakuwa inalipiwa kwa pesa ndogo.

SWALI: Pengine ushirikiano wenu kati ya Jeshi la Kujenga Taifa na majeshi mengine ukoje? tusaidie kwa faida ya Watanzania.

JIBU: Kwa kweli hilo ni suala ambalo tunashukuru viongozi wetu wa ngazi ya juu wameweka mfumo mzuri sana. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama wanashirikiana katika ngazi ya juu mpaka ngazi ya chini.

Na ndio maana kama nilivyosema mwanzo kuna kamati ya ulinzi na usalama utakuta vyombo vyote vinakutana pale kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya ulinzi na usalama katika maeneo yao.

Lakini tunasaidiana katika masuala mbalimbali pale inapotokea hitajio kwamba vyombo vyote vishirikishwe. Nadhani wananchi wote wanafahamu kwamba inapotokezea suala muhimu vyombo vyote vinashirikiana vizuri sana. Kwa hiyo mashirikiano ni mazuri.

SWALI: Meja Jenerali, tusaidie, sasa hivi tunaona teknolojia imebadilika, nini ambacho unafanya kama mkuu wa JKT kuhakikisha kwamba watu wako nao waendane na teknolojia ambayo ipo pengine katika kazi zenu, namna ambavyo mnafanya kazi, kuwapeleka wengine shule zaidi ili teknolojia inavyozidi kupanuka nanyi muendane na hiyo hali.

JIBU: Nitoe ufafanuzi kwamba ndani ya JKT kuna makundi mawili; kuna wale ambao ni viongozi ambao wote ni waajiriwa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.

Kwa hiyo wanaletwa huku wa ajili ya kuwalea vijana. Lakini kuna kundi la vijana wenyewe sasa ambalo ndio hasa national service, hawa ni kundi lingine.

Kujibu swali lako kwa upande wa hawa viongozi wanaoletwa huku, mafunzo yao yote wanachukua kupitia utaratibu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Na ndio maana Mkuu wa Majeshi ni kiongozi wao.

Lakini katika kuwafunza vijana, pia tunajaribu kubadilisha, tunapata maelekezo jinsi ya kuwalea kutoka chuo chetu cha viongozi.

Tumeanza pia kubadilisha teknolojia mashambani, kwa mfano tunaanza kutumia teknolojia ya madawa ya kuua magugu, mpunga kwa mfano sasa hivi tunakodisha combine harvesters (mashine za kuvuna).

Na kama nilivyosema badala ya kuuza mazao haya ya mashambani, mfano ukivuna mahindi badala ya kupura kwa kutumia mikono sasa hivi wanatumia mashine na kadhalika.

Kwa hiyo, tunajitahidi kuhakikisha kwamba tunakwenda sambamba na teknolojia ya sasa.

SWALI: Meja Jenerali tangu uteuliwe na Mheshimiwa Rais Februari Mosi, 2016, kama Mkuu wa JKT, natumaini kwamba ulikuta baadhi ya changamoto katika jeshi hili. Ni zipi hizo changamoto kwa ufupi na hadi sasa tumefika 2017 umezitatua vipi?

JIBU: Changamoto hazikosekani, lakini ziko chache na katika hizo kuna moja ambayo niliiona kuwa ni changamoto kubwa. Na bahati nzuri katika maelezo yangu yote na maswali mengi uliyoniuliza yalikuwa yanajikita hapo hapo.

Kwamba ulitokea usaili mwezi wa tano mwaka 2016, vijana waliojitokeza walikuwa ni wengi sana na kwa kweli tulikuwa hatuna sehemu ya kuwapeleka wote. Hiyo ndiyo changamoto kubwa.

Lakini kitu ambacho tulifurahi ni kwamba Rais wetu alipopata hizo habari ndio maana akaagiza kwamba makambi yote yaliyokuwa yameachwa yarudishwe.

Kwa hiyo kupata makambi matano ni moja ya hatua ya kutatua zile changamoto ambazo tulikuwa nazo. Vinginevyo changamoto zingine ni za kawaida ambazo ziko ndani ya uwezo wa JKT.

SWALI: Mwisho kabisa tunapokwenda kuhitimisha, wote tunakutazama wewe Meja Jenerali, nini Watanzania watarajie kwako kwa miaka mitano ijayo. Jeshi la Kujenga Taifa, tutarajiye litakuwa ni jeshi la namna gani?

JIBU:Kwa kweli wananchi kitu ambacho ningeweza kuwaeleza ni kwamba jeshi la kujenga taifa ni jeshi lao. Na ni jeshi ambalo lipo kwa ajili ya kuwalea vijana ili baadaye wawe vijana wazuri mijini na vijijini.

Lakini pia wawe ni wananchi bora wa baadaye katika nafasi mbalimbali kama wazazi, kama wakulima, wafanyabiashara na wale wanaopata nafasi waweze kuwa wafanyakazi.

Ninachoomba ni kwamba makambi haya yaliyoko katika maeneo mbalimbali katika nchi yetu ukiacha ile mikoa ambayo hatujaanzisha, kwa hiyo kwa yale maeneo ambayo kuna makambi ya JKT waone ni makazi yao.

Wajitahidi sana kushirikiana nayo kama kuna matatizo yote basi wayatatue katika namna ambayo hayataleta uvunjifu wa amani.

Uwepo wa makambi ya JKT uonekane kwao ni faraja badala ya kuwa mzigo. Niwahakikishie kwamba inapotokezea ni bahati mbaya askari mmoja wa kwetu, kwa sababu zake amefanya mambo ambayo yanawakera wananchi hatua zitachukuliwa.

Kwa hiyo naomba tu ushirikiano na kama ambavyo Rais wetu ameonyesha njia kuliendeleza hili jeshi na hata akafikia kwa muda mfupi kuanzisha makambi matano mapya, kwa hiyo mjue kwamba wale vijana wanaokosa nafasi wataendelea kuchukuliwa hatua kwa hatua.

 

 

Habari Kubwa