Majembe ma5 Afrika yaliyopo sokoni Ulaya

17Jul 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Majembe ma5 Afrika yaliyopo sokoni Ulaya

WACHEZAJI wa Afrika wamekuwa wahusika muhimu katika dirisha la usajili Ulaya hadi kufikia sasa, lakini ikiwa umebaki takriban mwezi mmoja na nusu kabla ya soko kufungwa, kunatarajiwa idadi kubwa kwa nyota wa bara hili wanaokipiga majuu kwenda kwingineko kutafuta nyasi zilizo bora zaidi.

Pierre-Emerick Aubameyang.

Mohamed Salah, Asamoah Gyan na Carlos Kameni, tayari wameshalamba dili mpya katika majira haya ya joto, lakini ni jina gani tena la kipaji kikubwa kutoka Afrika linatarajiwa kuelekea kwingineko kabla ya biashara kufungwa?

1. Pierre-Emerick Aubameyang
Mustakabali wa baadaye wa kipaji hiki kikubwa bado haueleweki, huku akipewa nafasi ya kutimkia Klabu ya Tianjin Quanjian ya China.

Lakini wakati klabu hiyo ya China ikiwa tayari kumwaga mpunga wa kutosha ili kumnasa, itakuwa ni aibu kwa kipaji cha hali ya juu kama hicho kwenda kucheza soka nchini humo kutokana na kiwango chake cha juu alichokionyesha barani Ulaya.

Kadhalika, inawezekana kuona straika huyo raia wa Gabon akitua Real Madrid, klabu ambayo alimuahidi babu yake kwamba ipo siku ataichezea.

Pia klabu tatu za Premier League Chelsea, Liverpool na Arsenal zimekuwa zikihusishwa na kuhitaji saini yake, na ubora wake alioonyesha kwa kufunga mabao 31 msimu uliopita, utamfanya kung'ara England, na hiyo inaonyesha ni kwa namna gani anaweza kufiti katika ligi hiyo.

2. Naby Keita
Kiungo huyu mahiri, alikuwa mmoja wa wategemewa wakubwa kwa RasenBallsport Leipzig msimu uliopita katika Bundesliga, kwa kuiwezesha kukata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya hapo mwakani.

Msimu huu atahitajika kuisaidia tena kutoa changamoto ya kuwania ubingwa, hivyo ni wazi RB Leipzig haitakuwa tayari kumuuza Keita.

Nyota huyo wa kimataifa wa Guinea, ameonyesha ubora wa hali ya juu - kwa kuweza kuvuna wastani wa 2.6 katika ukabaji na 2.6 uporaji pasi msimu uliopita kwenye Bundesliga.

Liverpool imekuwa ikihusishwa na kuhitaji saini ya Keita majira haya ya joto, lakini Leipzig imesisitiza kuwa kiungo huyo hauzwi, ila fedha zinaongea katika biashara hii!

3. Kelechi Iheanacho
Straika huyu wa Nigeria, anaonekana kuwa katika nafasi ya kuondoka majira haya ya joto. Ameshindwa kumshawishi Pep Guardiola kwa msimu uliopita- licha ya kufunga bao la ushindi dhidi ya Manchester United mapema msimu uliopita.

Kutua kwa Gabriel Jesus, kulimpa kizuizi kikubwa cha kufaulu kapata nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Bado ni kinda sana, Aiyegbeni Yakubu, Julius Aghahowa na Peter Rufai, walithibitisha hilo wakati walipoulizwa na ESPN, Iheanacho anahitaji kucheza mechi nyingi zaidi? Hata hivyo licha ya kwamba kwa kuwa chini ya Guardiola atafaidika kwa mbinu nyingi, kuhamia klabu nyingine ya Premier League kutathibitisha ubora wake zaidi na kuweza kujiendeleza.

Tottenham Hotspur, Arsenal na Everton zimekuwa zikihusishwa na straika huyo wa Super Eagles, ingawa klabu hizo tayari zimeshazama mfukoni na kusajili katika nafasi yake ya ushambuliajia, ila West Ham United inaweza kumnasa.

4. Serge Aurier
Uamuzi wa Paris Saint-Germain kumnunua Dani Alves kutoka Juventus umepokelewa vizuri katika jiji hilo la Ufaransa, ambapo kumekuwa na utamaduni mkubwa wa uhitaji wa vipaji kutoka Brazil.

Kwa hakika, nyota huyo wa zamani wa Barcelona hakuwa na sababu ya kutua Ligue 1, kwenda kucheza sehemu ambayo tayari kuna ushindani wa namba kati ya Thomas Meunier na Aurier wanaopigana vikumbo katika nafasi hiyo ya beki wa kulia.

Hivyo kutua kwake kunatarajiwa kuona nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast, Aurier akichapa mwendo.

Juve -ambayo tayari imeshapoteza uelekeo katika beki yake ya kulia, tayari imemtolea macho, wakati Manchester City iliyomsajili Kyle Walker pia inaiacha Spurs sokoni ikisaka mbadala wa nafasi hiyo.

5. Riyad Mahrez
Mwaka mmoja uliopita, mustakabali wa baadaye wa Mahrez, ulikuwa kati ya mada nzito katika dirisha la usajili. Lakini msimu wa 2016-17 kiasi fulani Mualgeria huyo hana soko kihivyo, na sasa zimebaki tu tetesi za kuhitajika.

Tetesi za nyota huyo wa zamani wa Le Havre kuhitajika Barcelona, tayari zimekufa, na sasa Mahrez amebaki akihusishwa zaidi na Arsenal.

Lakini hata hivyo, Arsenal inaonekana kama kutotoa msukumo mkubwa na sasa ameonekana kuhitajika zaidi AS Roma.

Habari Kubwa