Kumea mashamba ya mpunga Usangu kunavyokausha maji ya Mto Ruaha

28Dec 2017
George Tarimo
Nipashe
Kumea mashamba ya mpunga Usangu kunavyokausha maji ya Mto Ruaha
  • Imegeuka tatizo sugu lenye miaka 20
  • Hifadhi, umeme wa maji ziko njia panda

HIFADHI ya Taifa ya Ruaha ndiyo kubwa kuliko zote katika Afrika Mashariki, ikiwa na eneo lenye kilometa za mraba 20,226.

Ndani yake kuna vivutio mbalimbali vya wanyama wengi wakubwa na wadogo, ndege na samaki.

 

Pia, Mto Ruaha Mkuu unaanzia katika vyanzo vya maji kwenye mito midogo iliyopo katika mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya na milima ya Uporoto na Kipengere, kisha unakatisha katikati ya Hifadhi ya Taifa Ruaha.

 

Sasa inakuwa tegemezi na wanyama waishio ndani yake hata hivyo moja ya changamoto kubwa inayoikumba hifadhi hiyo ni kukauka kwa maji kwenye mto Ruaha Mkuu.

 

Hifadhi hiyo ni sehemu ya mfumo mkubwa wa ikolojia yenye ukubwa wa zaidi ya kilometa za mraba 45,000 inayojumuisha mapori ya akiba ya Rungwa, Kizigo na Muhesi ambazo zote zipo ndani ya bonde la Ruaha Mkuu, ambako mbali na utalii, pia kuna shughuli za kilimo na uvuvi.

 

Bonde hilo linachangia asilimia 80 ya uzalishaji umeme unaozalishwa kwa maji nchini kutoka mabwawa ya Kidatu na Mtera, pia linategemewa na mamilioni ya Watanzania kwa ajili ya uzalishaji maji.

 

Katika ziara yake na kushuhudia hali halisi, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, anatamka: “Kitendo hiki hakikubaliki. Inabidi maji yatiririke kama zamani, ili wanyama wetu wapate maji.”

 

“Sasa kukosekana maji, kutasababisha wanyama hawa waweze kuhama na kwenda hifadhi nyingine za jirani, pengine hata kuuawa na majangili na huko pembezoni wataenda kuwasumbua wananchi wetu.

 

“Leo hii nimetembelea hapa, nimejionea sasa hiki kipindi ni cha mvua na kipindi ambacho sio cha mvua, hali itakuwaje?” anahoji Samia.

 

Mwezi Aprili mwaka huu, Samia alizindua kikosi kazi cha kutembelea mikoa yote unakopita Mto Ruaha Mkuu, ili kuwaondoa wanaoendesha kilimo kwenye mto huo na hadi sasa kikosi hicho kinaendelea na kazi.

 

Mtiririko wa maji kwenye Mto Ruaha Mkuu, ni tegemeo la wanyama katika hifadhi hiyo na mabwawa ya kuzalisha umeme ya Mtera na Kidatu, pia wanyama na viumbe wengine katika hifadhi hiyo.

 

MUIKOLOJIA

 

Muikolojia wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Halima Kiwango, anasema eneo la ardhi oevu la Usangu, ndio chanzo kikuu cha maji kwenye Mto Ruaha Mkuu.

 

Anasema kuwa Mto Ruaha Mkuu katika hifadhi ya taifa ya Ruaha ulianza kukauka mwaka 1993, katika kipindi kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba na muda wa kukauka mto umekuwa ukiongezeka wakati mwingine hadi miezi mitano mfululizo.

 

Anasema takribani miaka 20 iliyopita, eneo hilo liliharibiwa na kuongezeka shughuli za kibinadamu, hususan kilimo cha umwagiliaji wa mashamba ya mpunga na uvamizi wa mifugo.

 

Halima anasema Usangu ni bakuli linalokinga maji wakati wa mvua na kuyatiririsha kwenye Mto Ruaha Mkuu, ilikauka kabisa katika kipindi cha kiangazi mwaka 2000 na 2002, hivyo kuathiri mtiririko wa maji na lilipata uhai tena baada ya kuondolewa mifugo katika eneo la Usangu, mwaka 2006.

 

Halima anasema tafiti mbalimbali zilifanyika kukadiria kiasi cha maji kinachotakiwa katika vipindi mbalimbali vya mwaka, kuuwezesha mfumo wa ikolojia ya mto na hifadhi kwa ujumla kutoathirika.

 

Takwimu zinaonyesha tangu mwaka 2007 hadi 2017, kiasi cha maji katika Mto Ruaha kimepungua kwa asilimia kati ya 10 na 76 kwa kipindi cha masika na asilimia kati ya 50 hadi 100, katika kipindi cha kiangazi.

 

MHIFADHI MKUU RUAHA

 

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha, Dk.Chritopher Timbuka, anasema kukauka mto huo kumewaweka hatarini viumbe hai wa majini, baadhi wakifa kwa magonjwa ya kuambukizana, wengine kukosa maji.

 

Mwezi Septemba mwaka huu, viboko 42 walikufa kwenye Hifadhi ya Ruaha, huku tahadhari ikiendelea kuchukuliwa kudhibiti ugonjwa uliowaua kwa kuchukuliwa sampuli ya viboko waliokufa.

 

“Hapa kwetu tuna samaki ambao wanategemea maji kwa kiasi kikubwa wanaweza kuathirika, wengine kufa kutokana na kukosekana kwa maji au maji yanayobakia kwenye madimbwi na mabwawa kuwa ya moto sana, kiasi cha samaki kupoteza kiasi kikubwa cha oksijeni kilichopo kwenye maji na hatimaye kufa,” anasema Dk.Timbuka.

 

MATUMIZI DUNI

 

Dk.Christopher Timbuka anasema changamoto inayoukabili Mto Ruaha Mkuu, ni matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali maji kwa ajili ya kilimo, ufugaji na makazi yanayofanywa kwenye ardhi oevu ya Ihefu na vyanzo vingine vya maji vinavyotiririsha maji katika mto huo.

 

 

Dk.Timbuka anatahadharisha kutoweka hifadhi hiyo, iwapo hakutakuwapo namna endelevu ya kulinda hifadhi.

 

Anasema zimekuwapo jitihada mbalimbali za kunusuru hali hiyo, lakini kauli za baadhi ya wanasiasa zinazohamasisha shughuli za kibinadamu kufanyika kwenye vyanzo vya maji zimekuwa zikikwamisha jitihada za Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) kumaliza tatizo hilo.

 

“Kwa kipindi cha miaka 14 sasa, changamoto kubwa inayokabili mto huo ni maji kukauka, wanyama kuhama, samaki kuathirika na wengine kufa kwa sababu ya maji kuwa na moto.

 

“Wanyama wanapoenda nje ya hifadhi, kuna madhara kwa jamii ikiwamo msuguano baina ya jamii na Tanapa, kuharibu mazao, madhara kwa binadamu, mifugo na hata mimea kuathirika,” anasema Dk. Timbuka na kufafanua:

 

“Kwa sababu kingo za mito zinaharibiwa hasa kwenye yale maeneo ambayo wanyama wanapita kunywa maji, mmomonyoko wa udongo na kusababisha kina cha maji kujaa udongo na maji yanapokuja kina cha maji kinakuwa kifupi.”

 

NINI KINAFANYIKA? 

Dk. Timbuka ana ushauri kwa kauli ifuatayo:”Hakuna njia mbadala kuweza kunusuru ikolojia ya mto huu, isipokuwa kwa kupunguza au kuzifanya kwa uendelevu shughuli za kilimo.

 

“Hii ni kwa sababu kwenye kilimo, watu wengine wanachukua maji wakati wa kiangazi halafu hawayatumii. Sasa yale maji yakirudishwa kwenye mto yatasaidia kwa kiasi kikubwa.

 

“Kama watatumia kwa njia endelevu na baadaye wakayarudisha kwenye mto, naamini maji yatatiririka kwa mwaka mzima,”anasema Dk.Timbuka.

 

Anapinga utaratibu wa watu kuchukua maji mtoni kwa njia ya mifereji au pampu.

 

Kuhusu viboko waliokufa, Dk.Timbuka anasema hivi karibuni sampuli zao zilipelekwa katika Kituo cha Utafiti wa Mifusi Iringa (Veterinary Investigation Centre) na sasa zimepelekwa makao makuu jijini Dar es Salaam, kwa uchunguzi zaidi, baada ya kubainika ni kimeta.

 

OFISA MAJI

 

Ofisa wa Maji Bodi ya Maji ya Bonde la Mto Rufiji, Idris Msuya, anasema kukauka Mto Ruaha Mkuu ni kwa muda mrefu sasa na kipindi cha mto kukauka kumeongezeka katika eneo iliko Hifadhi Ruaha.

 

Ofisa huyo anasema tafiti nyingi zimefanyika na kubaini watafiti hasa eneo oevu la Ihefu, wilayani Mbarali, Mbeya.

 

“Maji mengi yanachepushwa lakini hakuna miundombinu kama sehemu za kuchukulia maji (Intake) na mifereji iliyopo haijasakafiwa na watu wanaendelea kutumia maji mengi hata sehemu ambazo hazihitaji maji mengi,” anasema Idris.

 

Anasifu jumuiya za watumia maji kusaidia utunzaji wa vyanzo vya maji na hata hivi karibuni wameweka mipaka kwenye vyanzo vya maji na kuondoa vizuizi vya maji.

 

Akizungumzia watumia maji haramu (bila kibali), Idris anasema wamekuwa wakizuka kila siku na sehemu kubwa wapo katika maeneo yasiyofikika wakati wa mvua.

 

“Wilaya ya Mbarali ipo eneo tambarare na mvua zikiwa nyingi eneo lote linakuwa limeenea maji. Huwezi kuwafikia watu hao na wao wanatumia mlango huo, lakini maeneo ambayo yanafikika tumejitahidi na kupunguza mifereji haramu, ikiwamo kufunga mifereji na kuwalipisha faini,” anasema Idris.

 

Anaogeza:“Maji yakishatumika kwenye mashamba makubwa ya mpunga ya Kapunga na Mbarali, yanatakiwa kurudi mtoni.

 

“Wananchi wamevamia maeneo yanayopita maji kwenda mtoni na kufungua mashamba makubwa hata kuliko mashamba yaliyopo na matokeo yake maji yaliyotumika hayarudi mtoni.”

 

Idris anasema kikosi kazi cha Makamu wa Rais – Samia, kiligundua eneo kubwa sawa na mashamba matatu ya Kapunga, Mbarali na Madibila yanayomwagiliwa nje ya maeneo yenye kibali.

 

Anasema bwawa la Mtera linalopeleka maji Kidatu bado linafanya kazi na iwapo mwaka huu mvua zikinyesha, bwawa hilo litaendesha mitambo yake katika kiwango cha kawaida. Maji yanayotumika sasa ni makusanyo au miaka iliyopita.

 

Wadau mbalimbali wa mazingira walijitokeza kupambana kwa ajili ya kurejesha mtiririko wa maji ni Spanest, WWF, Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, pamoja na Tanapa.

 

MRADI WA PAMOJA

 

Godwel Ole Meing’ataki, Mratibu wa Mradi wa Kuhifadhi na Kuendeleza Maeneo yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (Spanest), anasema moja ya vivutio kwenye Hifadhi ya Ruaha ni Mto Ruaha Mkuu.

 

Ni mradi ulio chini ya Tanapa na kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), lakini kwa sasa mto huo umekauka kabisa kiasi cha wanyama wengi kupata shida.

 

Pia, inaelezwa wanyama wakubwa kama tembo, wanaweza kuhama kwenda pembezoni kwa lengo kutafuta maji na wakienda nje ya Hifadhi wanaweza kuleta madhara kwa kuharibu mali za wananchi.

 

Ole Meing’ataki, anasema jitihada nyingi zimefanyika kuhamasisha wadau, kuelimisha na kushirikiana pamoja, lakini hawajafanikiwa na inachukuliwa hatua mpya kwa vitendo.

 

“Kwa ninavyofahamu mimi changamoto ya mto ruaha sio kuhamasisha tu, bali tuangalie kiini cha huu mto kukauka ambao ni matumizi holela ya maji katika bonde la Usangu,” anasema Meing’ataki.

 

Baadhi ya wanyama walioonekana kuhangaika kutokana na kupungua maji, ni viboko, tembo na swala.

 

Mkazi wa eneo hilo, Rachel Mbosa, anahoji:“Mimi binafsi nawaomba wanasiasa waache kutoa kauli zinazokinzana na maagizo ya serikali, kwa sababu kauli hizo zinawafanya wananchi kuendelea kushambulia maeneo oevu na vyanzo vingine vinavyotiririsha maji katika mto Ruaha Mkuu, ambao ni chanzo cha peke yake cha maji na cha uhakika kwa wanyama wa hifadhi ya Ruaha.”

 

Kwa mujibu wa Meing’ataki, Spanet imefanya mengi ya kuendeleza hifadhi hiyo katika mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya na maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Ruaha.

 

Anasema tayari wameshachukua sampuli ya damu ya viboko itakayopelekwa kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kwa mujibu wa Dk. Timbuka, vimelea vya kimeta vinasababishwa na mambo kadhaa, ikiwamo matumizi ya maji machafu ambayo kwa sasa yanatumiwa na viboko wa Ruaha.

 

“Mwaka jana amethibitisha viboko watano na twiga watatu, lakini mwaka huu kwa mwezi Septemba wanamaeneo matatu ambayo yana jumla ya viboko 42 ambao wamekufa, japokuwa hatujamaliza kuchukua sampuli lakini dalili za awali zinaonesha ni kimeta,” anasema Dk.Timbuka.

 

KAZI YA NEMC

 

Kikosi kazi kilipoelekea wilayani Kilolo, Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC,) kiliwatoza faini ya Shilingi milioni 20 wawekezaji wawili wa kilimo na ufugaji wilayani humo, kwa makosa ya kuendesha shughuli zao bila kufanya tathmini ya uharibifu wa mazingira.

 

Mwanasheria wa NEMC, David Kongola, alitoa baadhi ya adhabu hizo, alipotembelea mashamba ya wawekezaji na kubaini kasoro kubwa za mazingira na kuhatarisha usalama wa vyanzo vya maji na

 

“Sasa adhabu yao hawa, sisi tunawatoza Shilingi milioni 10, kwa kila mmoja kwa kufanya hii shughuli bila ya kuwa na cheti cha EIA (Tathmini ya Mazingira),” anasema Kongola.

 

 

 

Habari Kubwa