Kukaribia miaka 24 tangu mauaji ya Rwanda, dunia haijajifunza chochote

03Jan 2018
Ani Jozen
Nipashe
Kukaribia miaka 24 tangu mauaji ya Rwanda, dunia haijajifunza chochote

BAADHI ya watu wanaofuatilia mtitiriko wa kesi na taarifa nyinginezo kuhusu mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994 walishangaa hivi karibuni.

RAIS RWANDA, PAUL KAGAME.

Walishangaa kusoma mahojiano maalum kati ya Linda Melvern, mwandishi wa habari za uchunguzi wa Uingereza ambaye mwaka 1994 alikuwa akitafiti kuandika kitabu cha historia ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa.

Ni wakati huo mauaji ya Rwanda yalipoanza akaona kuwa ni tukio kubwa sana katika kile alichokuwa akikifuatilia, akaacha upana wa historia ile (hata kama kuna sehemu aliyochapisha) akaingia katika mkakati mpya.

Hadi leo anaendelea kufuatilia suala hilo na kuandika vitabu.

Licha ya kuwa gazeti lililochapisha mahojiano hayo, moja ya magazeti makubwa nchini halikusema habari hiyo ilichapishwa wapi kwanza, inaelekea ilikuwa katika mtandao baada ya kuchapishwa nchini Rwanda.

Mwanamama huyo mchunguzi na mwenye uchungu na kilichotokea mwaka 1994 amepata nishani za juu nchini humo kwa urafiki wake wa kina na watu wa Rwanda.

Anasikitishwa na udhaifu wa jumuiya ya kimataifa kuhusiana na suala hilo, jinsi kesi zilivyoendeshwa katika Mahakama Maalum ya Kimataifa ya Rwanda (ICTR) hadi ilipofungwa, chombo kingine kikachukua nyaraka zake. Yote hayo anayachunguza na aliyajadili.

Moja ya mambo aliyoyagundua katika utafiti na uchunguzi kwa zaidi ya miaka 20 ambayo aliyagusia katika mahojiano (na chombo cha habari nchini Rwanda) ni jinsi mauaji yale yalivyopangwa na kulipiwa, na hata jinsi silaha zilivyokusanywa.

Kwa mfano itakumbukwa kuwa silaha iliyotumiwa zaidi katika kuua watu wa kabila la wa-Tutsi (na wa-Hutu wanaopenda amani, mazungumzo na kundi la waasi) ni mapanga.

Hayakuwa ni ya kawaida yanayotumika nyumbani ila yalinunuliwa (baada ya kutengenezwa kwa 'order' rasmi kama bidhaa) nchini Misri. Aliyefanya mpango wote huo alikuwa Dk. Boutros Boutros Ghali, anayejulikana sana.

Profesa Boutros-Ghali aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje nchini Misri na baadaye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), na wakati huo (wa mauaji ya Rwanda) akawa ni Katibu Mkuu wa La Francophonie, yaani sekretariati ya kuunganisha nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa duniani.

Ina maana kuwa ni silaha za mauaji zilizonunuliwa kibiashara na kuingia kibiashara kwa kutumia NGO, kwani La Francophonie ni kama NGO, au zinaitwa 'QUANGO,' Quasi-Governmental Organizations (mashirika huru ya kiserikali).

Akijibu swali la mwandishi na mchunguzi huyo alisema eti 'silaha nyingine elfu kadhaa zisingebadili lolote' nchini Rwanda.

Mchunguzi anatoa lawama kali kuhusu vikao vya Baraza la Usalama kuhusu suala hilo vilivyoendeshwa, akisema kuwa dhamira ya UN ni uwazi na ukweli kuzuia matukio kama lile la Rwanda na mengine mengi, ndiyo maana ya kianzio cha tangazo la kuundwa kwake, 'We, the peoples...'

Anasema katika hali halisi dhamira hiyo haifuatwi na hivyo UN inakuwa umoja wa serikali zao, siyo watu wenyewe, changamoto ya kihisia kuhusu dhamira ya katiba au kanuni za diplomasia ambazo hakuna mwenye jibu la swali hilo.

Kimsingi ni kuwa mradi waliokuwa wanajadiliana ni wa udhalilishi wa serikali, mauaji yalifaulu.

Kuonyesha jinsi waliokuwa na nafasi ya kuzuia tukio hilo walikaa pembeni wakaruhusu mkondo wa uovu uchukue nafasi yake, Melvern anakumbushia jinsi mwandishi wa Uingereza Richard Dowden alivyofika Kigali mwanzo wa mwaka 1994 akakutana na ofisa mwandamizi Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) Phillip Gaillard.

Mwakilishi mkuu huyo alieleza kuwa mauaji ya kimbari dhidi ya waTutsi yamepangwa kufanyika na mwandishi huyo akasema haoni ushahidi wowote, akaondoka nchini humo baada ya siku tatu.

Mauaji yalipoanza Aprili 6 usiku wa manane ilichukua wiki tatu ndipo Oxfam ikatoa taarifa kuwa yapo mauaji.

Habari hiyo ilipotoka Aprili 28 ilipuuzwa na vyombo vya habari vya kimataifa (kwa maana ya vile vya nchi za Magharibi), kiasi kwamba gazeti linalosifika kwa habari za kimaendeleo nchini Uingereza, The Guardian, liliitoa habari hiyo kama muhtasari, wenye 'paragraph' moja katika ukurasa wa 15 wa toleo lake la siku hiyo.

Ni wakati waandishi wa habari kutoka nchi tofauti duniani walipofika katika sherehe ya kuapishwa kwa Rais Nelson Mandela nchini Afrika Kusini ambako hali hiyo sasa iliwekwa wazi, ikazungumzwa kwa kina kati ya waliokuwapo, mwisho wa Aprili, ambako habari zilianza kusikika, juhudi za kukanusha kilichotokea zikaanza.

Mchunguzi huyo ametumia muda mwingi kutafiti na kupambana na mtiririko wa habari na machapisho yenye lengo la upotoshaji, kwa mfano 'documentary,' taarifa ya kichunguzi na kitafiti iliyotolewa na shirika la utangazaji la Uingereza, BBC.

'Documentary' hiyo ilidai kuwa wa-Hutu walikufa zaidi katika machafuko hayo nchini Rwanda kuliko wa-Tutsi, ambao ni uwongo wa kutunga.

Mojawapo ya vielelezo vya upotoshaji huo, lakini kielelezo hicho hakikurudiwa katika mahojiano hayo, ni dai la muda mrefu kuwa ndege ya aliyekuwa Rais Juvenal Habyarimana iliangushwa na waasi RPF (chama cha Rais Paul Kagame), ikasababisha mauaji.

Suala hilo liliwahi kujadiliwa kwa kina na mchunguzi na mtafiti mwingine, Profesa Gerard Prunier ambaye alifanya utafiti ndani ya mwaka mmoja wa mauaji hayo akagundua kuwa mauaji yalianza nusu saa baada ya ndege iliyomchukua Rais Habyarimana kuangushwa karibu na Ikulu.

Swali lake lilikuwa kwamba endapo ndege hiyo ingekuwa imeangushwa na waasi, kama propaganda za utawala wa wauaji ulivyokuwa ukidai, na dhana hiyo ikaenea kama sumu kote Afrika Mashariki na kwingineko, ingekuwaje vikosi vya mgambo tayari vimejipanga ndani ya nusu saa? Si ingekuwa mtafutano kuanza wa kuweka mazingira ya uwepo wa serikali?

Kimsingi ndege hiyo ilikuwa iangushwe ili kujua kuwa mamlaka ya nchi yametoka mikononi mwa rais na makamu wake, Agathe Uwilingiyimana ambaye aliuawa mapema kabisa baada ya wakataji mapanga kuanza kazi, pamoja na walinzi 10 nyumbani kwake, askari wa UN wakitokea Ubelgiji.

Alipokufa Rais Habyarimana kamati ya maandalizi ya mauaji ndiyo iliyotwaa madaraka halisi, ikateua wakuu wa majeshi na nafasi nyingine, na kiongozi wake alikuwa Kanali Theoneste Bagosora, shemeji wa Habyarimana ambaye alipinga kwa nguvu zote mazungumzo ya amani ya Arusha, akiwa waziri wa Ulinzi. Akaapa kuleta 'kiyama.'

Kwa vile bado tuna 'matongotongo' ya kusherehekea uhuru (Desemba 9) labda tungekumbushana kuwa suala la uhuru kuleta Afrika njema zaidi kuliko ukoloni (ulivyokuwa au ungeendelea) bado linaleta mjadala wa kina, ingawa si kila wakati.

Machafuko na mauaji ya kimbari kama ya Rwanda yamewezekana kwa sababu Afrika iko huru na hakuna nchi ya kuingilia wanachopanga, wakati haijafikia ngazi ambako dhana ya utu wa binadamu, thamani ya uhai wa binadamu kuingia katika fikra na kutawala kinachotokea katika siasa nchini.

Mwandishi Melvern anaulaumu Umoja wa Mataifa - ila aseme ni kwa kutokuiokoa Rwanda na mizimu yake.

Ndiyo iliyoandaa umwagaji damu; gazeti la wauaji, Kangura, ni jina la mzimu, upo pia huku kwetu, Kangero.

 

 

 

 

 

Habari Kubwa