Kuingilia kijeshi Gambia na ustawishaji wa demokrasia Afrika

11Jan 2017
Ani Jozen
Nipashe
Kuingilia kijeshi Gambia na ustawishaji wa demokrasia Afrika

KUEKEA mkesha wa Krismasi na mwaka mpya, kulikuwa na kila dalili kuwa kiongozi wa Gambia aliyeshindwa katika Uchaguzi Mkuu kujaribu kukiuka azma yake ya kukiri matokeo hasi kwake angeweza kujikuta akishikishwa adabu na majirani zake wa Afrika Magharibi.

Rais Yahya Jammeh kwanza alikiri kuwa upinzani ulikuwa umeshinda uchaguzi, lakini kwa kuwa amekuwa Amiri Jeshi Mkuu kwa miaka 22, anaamini kuwa majeshi ya nchi hiyo yako nyuma yake na hayataki wapinzani watwae madaraka.

Ndicho kinatokea Afrika; kwanza watu wapige kura, lakini pia jeshi liulizwe.

Ni hali ambayo watawala wa Afrika wanataka waendelee nayo milele ila upo uwezekano kuingilia kati endapo ni nchi ndogo kama Gambia.

Uingiliaji kijeshi katika nchi za Afrika umechukua sura kadhaa tangu uhuru, na huu wa kulazimisha kukubaliwa kwa matokeo ya uchaguzi wa kidemokrasia ni ya hivi karibuni zaidi.

Miaka iliyopita nchi zilikuwa zinaingilia kati kulingana na maslahi yao endapo nchi inaparaganyika, kwa mfano Ethiopia ikisukumwa na kufadhiliwa na Marekani iliingilia Somalia kuondoa utawala wa Mahakama za Kiislamu walipokaribia kupata ushindi nchi nzima.

Nchini Congo kudorora kwa utawala wa Mobutu Seseseko kulitoa nafasi ya Rwanda na Uganda kuingilia kati, vita pana ikaja baadaye.

Kabla ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu nchini humo, Rais Jammeh alitangaza mpango wa kujitoa katika Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC) kwa madai yale yale ya kulengwa viongozi wa Afrika na si wengine duniani.

Ni kama sasa akisema anaandamwa kwa vile ni Mwafrika, hilo tu. Na Mwendesha Mashtaka wa ICC ni raia wa Gambia, Fatou Bensouda, na hatamwonea haya.

Ila mazingira hayo hayajafikiwa, na hapajakuwepo bado na umwagaji damu kama Burundi ambako kukataa kuheshimu ukomo wa mihula kuliingiza nchi katika machafuko.

Kulikuwa na uasi wa jeshi wa baadhi ya vikosi lakini ukashindwa, wakaanza kupitapita wafuasi wa Rais Pierre Nkurunziza kudai eti ni Watutsi wanataka waanze kutawala tena, na si mapungufu demokrasia na kukithiri kwa rushwa nchini humo.

Hakuna mpango wa kuingilia kijeshi kwa nchi za Afrika Mashariki kwa suala kama la Burundi, tofauti na Somalia.

Suala kuhusu uvamizi wa kijeshi linakuja kwa kuwa kuna tofauti kati ya tatizo la kuvurugwa kwa mtiririko wa kawaida wa uchaguzi mkuu, kutangaza matokeo na kila mhusika atii, na kuangalia ukubwa wa nchi ili kuingilia.

Hata hivyo nchi kama Ivory Coast ambayo ni kubwa na yenye nguvu tofauti na Gambia pia iliingiliwa kijeshi, vikosi vya Ufaransa vikiongoza, wakati Rais Laurent Gbagbo alipokataa matokeo ya Uchaguzi Mkuu, akidai mpinzani wake Alassane Ouatarra ni raia wa Burkina Faso.

Ndiyo Hizbu ya nchini Cote d’Ivoire, mtu anatupiwa u-Hizbu anapokuwa mpinzani, asimsumbue mzawa.

Ndipo inazuka kanuni kuwa nchi yenye nguvu ikivuruga Uchaguzi Mkuu inabidi kuwe na hali tete ya machafuko ndipo nchi zijikusanye kuingilia kati, kama kuna taifa kubwa la kikanda kuongoza operesheni hiyo lijikusanye kuingilia kati, au taifa kubwa la Magharibi liko tayari kuongoza operesheni hiyo.

Kwasababu machafuko yalikuwa hayajaanza nchini Gambia kutokana na kukataa matokeo ya Uchaguzi Mkuu, suala la kuingilia kati lilikuwa bado mapema, lakini wazo hilo lilikuja haraka kwani inaonekena haitakuwa kazi ngumu. Kwa maana hiyo suala la maadili lipo, na pia dalili za ‘kujitutumua.’

Licha ya mapungufu yake katika mizani ya uharaka wa kuingilia kati, bado kuna chembe ya kujiamulia wenyewe hata ingekuwa ni suala la kukataa matokeo ya uchaguzi – kama serikali ilivyosisitiza kwa suala la kufutwa kwa matokeo uchaguzi wa rais Zanzibar.

Ni suala hili ambalo linafanya kungoja hadi kuwe na machafuko ndipo kuwe na suala la uingiliaji kijeshi au watu wengi wapoteze maisha ndipo suala la ICC lifikiriwe.

Kufanya vinginevyo ni sawa na kutokujali kuwa nchi hiyo ni huru; haijauhatarishia amani ukanda.

Inaelekea kuwa Rais Jammeh ‘amegangamala’ katika kukataa kutambua matokeo ya Uchaguzi Mkuu, hali inayomaanisha kuandaliwa kwa uvamizi.

Haitazamiwi kuwa operesheni hiyo itachukua muda mrefu au labda kuzaa matunda hasi kama yale ya Libya, alipopunduliwa Gaddafi, zimwi likatanda.

Endapo kunakuwa na uingiliaji kijeshi halafu sehemu ya wafuasi wa Jammeh wanaacha kushabikia demokrasia ya vyama vingi na badala yake wanaanza kujumuika kutaka ‘sheria za Mungu’ ndiyo zifuatwe na siyo za binadamu, kuingilia kunakuwa sumu.

Ni mazingira ambako badala ya nchi kujisukuma iwezavyo, hata kwa ‘udikteta uchwara’ hadi ifikie demokrasia kwa hatua zake yenyewe, inasukumwa kukamilisha hatua za demokrasia na badala yake inafumuka.

Ndivyo Iraq ilivyofumuliwa na kupoteza dira kama nchi, pale Marekani na washirika wake walipovamia kuondoa ‘silaha za maangamizi’ za kubuni, kumbe suala lilikuwa kuondoa ushawishi wa Russia, China; mafuta.

Kwasababu Rais Jammeh alikuza sana uhusiano wake na mifungamano mikali ya kidini na hata kujiita sheikh, akiwa pia amehiji mara kadhaa, kuna hatari ya kujinasibisha na wafuasi wa makundi kama hayo kama alivyofanya Rais Saddam Hussein nchini Iraq wakati Marekani ilipovamia.

Na mwendelezo wa vita nchini humo ukachukua sura ya kidini badala ya vita ya demokrasia, hali ambayo pia ilijiri nchini Libya.

Rais Gaddafi muda wote alijaribu kushika mizania kati ya dini na itikadi ya kimapinduzi ya ki-Magharibi, hivyo akiwa hana njia nyingine dhidi ya uvamizi wa Magharibi, alijishikamanisha na dini.

Waswahili wanasema ‘amdharau mwiba mguu huota tende’ na hilo linaelekea ni tatizo kwa upande wa Gambia, kuwa nchi za jirani zina ‘mchecheto’ wa kuvamia na kuondoa serikali ya Jammeh madarakani baada ya kushindwa uchaguzi.

Kinachotawala katika hisia za wapanga mikakati wa nchi za Magharibi na wenzao wa nchi za Afrika waliosomea na wenye hisia kiitikadi zinazoendana na zile za Magharibi ni kuwa hapa kuna mtu mmoja ambaye anang’ang’ania madarakani baada ya kushindwa katika kura.

Kumbe kuna mifumo ya jadi iliyojikita katika dola ambako siyo rahisi makundi hasi kuwa tayari kubadilishana nafasi madarakani, kama inavyoonekana nchini Marekani hivi sasa, yaani uadui wa wazi kati ya wafuasi wa Republican na wale wa Democrat, kwani tofauti zao mwaka huu ni za kina zaidi kuliko kawaida.

Tofauti za kijamii na kisiasa Afrika hazivumishwi katika nchi za Magharibi na badala yake wanaonekana tu ‘madikteta uchwara,’ na matokeo yake ni maafa. Na si Afrika tu ila hata nchi za Mashariki ya Kati; na si chache.

Habari Kubwa