KIWEWE CHA KUSAKA NGUVU ZA KIUME

16Jul 2017
Christina Mwakangale
Nipashe Jumapili
KIWEWE CHA KUSAKA NGUVU ZA KIUME
  • TFDA yaonya ulaji ‘Viagra’ feki wanaume wajihadhari kupasua mioyo Vyakula vya mizizi na baharini vyatajwa kuwa ni supa

ZAMA hizi za malalamiko ya ukosefu wa nguvu za kiume zimeibua wajasiriamali wanaofanya biashara ya kuuza dawa za asili na kuboresha uwezo wa kujamiiana nyingine zisizo rasmi japo kuna wengine wanaosambaza zilizotafitiwa na kusajiliwa.

Wakati nikifikiria kuandika makala hii nilikutana na vibao vya matangazo madogo kwenye mitaa tofauti jijini Dar es Salaam, hususan Buguruni, Vingunguti, Magomeni, Manzese, Ubungo, Kimara na Tabata yakitangaza namna wateja wanavyoweza kupata tiba ya nguvu hizo kwa kutumia dawa za asili.

Katika matangazo hayo mara nyingi wanaotangaza hawataji wala kuelekeza lilipo duka, nyumba au mtaa zinakouzwa, bali utaziona namba zimewekwa kwa ajili ya kupata mawasiliano na mganga.

WADHIBITI UBORA
Hata hivyo Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), mara nyingi inasisitiza kuwa dawa pekee zinazofaa ni zile zilizothibitishwa kitaalamu kuwa zina tiba ya upungufu huo na siyo vinginevyo na kuonya kuwa kama zipo zilizothibitishwa si nyingi na kwamba hazizidi tano kwa orodha.

Nyingi hazijathibitishwa na hivyo kuwa na uwezekano wa kutotimiza matarajio ya watumiaji au kuwaweka hatarini na kusababisha madhara mbalimbali yakiwamo ya kupasuka kwa mishipa ya damu kwenye moyo.

Afisa Uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza, anaiambia Nipashe kuwa ni kweli kuna dawa nyingi zinazotangazwa na watu mbalimbali kuwa zinatibu tatizo la nguvu za kiume, lakini zilizo rasmi ni pamoja na Viagra, Erecto, Cialis na Suagra.

Anasema dawa hizo ndizo wanazozitambua kuwa zinaweza kutumiwa na watu waliopungukiwa au kuishiwa kabisa nguvu za kiume kwa sababu zimepitishwa baada ya kukidhi vigezo vya kitaalamu. Hata hivyo, Simwanza anasema dawa hizo siyo za kutumiwa kiholela bali wenye shida nazo ni lazima wafuate maelekezo ya madaktari ili kujiepusha na madhara.

“Kuna dawa nyingi ambazo sisi tunazitambua na tumezipitisha zitumike…lakini mtu asizitumie hadi pale atakapopewa ushauri wa daktari. Hizi zina nguvu na zinaweza kufanya mishipa ya moyo kupasuka ama kuathiri mfumo wa damu kwa watu wanaozitumia bila kufuata maelekezo ya wataalamu,” anasema Simwanza.

Alipoulizwa kuhusu dawa za asili za kuongeza nguvu za kiume zikiwamo kizizi cha mkuyati na zile zinazofahamika kama vumbi la Kongo, zikihusisha orodha ya dawa mbalimbali za aina hiyo kutoka Kongo kama kasongo na mundende, Simwanza anasema TFDA hawawezi kuzizungumzia hizo na badala yake waulizwe wataalamu wa kitengo cha Tiba Asili na Tiba Mbadala cha Wizara ya Afya au katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Dawa nyingine maarufu za kiasili ambazo huuzwa katika maeneo mbalimbali Dar es Salaam hutambulishwa kwa majina ya mkongoraa, sheki na oljanilolo zinazopatikana kwa Wamasai

KUTUMIA VYAKULA
Hivi karibuni Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Paul Mhame (pichani), anasema mahitaji ni makubwa ya bidhaa kwa baadhi ya watumiaji wanaamini kwamba zitawasaidia na furaha kwenye mahusiano.

Anasema ukweli ni kwamba ulaji wa vyakula vya kisasa na kuvipuuza vya asili ni sababu mojawapo ya kuongezeka kwa idadi ya wanaume wanaozitafuta nguvu za kiume hususan mijini.

"Ukiona mahitaji ni makubwa kuna wahitaji, tena katika hili ni kinamama ndio wanaohitaji na kuwasukuma kinababa kutafuta dawa hizo, huwezi kuwafananisha na wanaume wa miaka ya 1960 na wa sasa anayekula viazi au chips, chakula anachokula wa leo si cha asili, matokeo yake dawa zinatumika la sivyo ndoa zitavunjika,” anaonya.

Dokta Mhame anaeleza kwamba aina za vyakula zipo nyingi ikiwamo vile vitokanavyo na mizizi kama viazi, mihogo, viazi vikuu na vitamu, vingine vya porini pamoja na matunda .

Uyoga unatajwa kuwa katika miaka ya nyuma ulikuwa unaliwa na kwamba ulikuwa unaota maeneo mengi , lakini pia pombe za kienyeji zilichanganywa na mimea ya kuongeza na kuimarisha afya kabla ya kunywewa.

“Hivi sasa vinywaji vinavyotumiwa hasa mjini ni vile vilivyofungashwa katika vifungashio vya kisasa kutoka kiwandani na kuwekewa dawa ili visiharibike, pamoja na mabadiliko ya kisayansi na teknolojia kwenye uzindikaji,lakini tunaweza kula na kunywa vinywaji ambavyo ni vya asili kwenye mazingira haya,” anahimiza.

Zipo mbegu za asili kama kweme, njugu, mboga za maboga na vyakula vya mseto vya kienyeji vyenye mboga, maziwa, wanga na michanganyiko mingine mingi ya protini ambavyo vinaweza kuimarisha afya ya mwanaume.

Mboga za asili kama mlenda, nyanya, vitunguu vya asili na jamii nyingine za minafu zilikuwa muhimu kwenye kupata lishe yenye tiba.

USASA MWINGI
Anasema tatizo lililopo nyakati hizi ni usasa kwa baadhi ya wasomi ambao hawana muunganiko wa moja kwa moja kati ya mazingira, chakula na mtindo wa kuishi.

Anasema zamani mbegu kwa ajili ya mazao tofauti zilitunzwa ndani na zilitumiwa kwenye msimu mwingine wa kilimo wakati hivi sasa baada ya kuvuna mkulima anakula hadi mbegu, akitegemea kwenda kununua nyingine dukani.

“Zamani wazee wetu walisafiri na mbegu kila walipokuwa wanahama au walihifadhi ndani, watakula mazao yote lakini mbegu imo ndani, hii ilikuwa ni kulinda asili na aina ya chakula cha asili.”

“Mbegu ya asili ya mpunga uliolimwa mwaka 1960 hivi sasa haipo, kinachopandwa ni aina mpya.” Kwa upande wa mbegu changamoto ni nyingi kama vile mabadiliko ya hali ya hewa , mazao ya asili kubunguliwa na viuatilifu, ukame na athari nyingine kwenye kilimo ambazo zinahitaji maboresho ya mbegu na kilimo cha kisasa kufanyika mara kwa mara.

Anasema hivi sasa wanaokumbwa na changamoto hiyo akimuelezea rafiki au mtu yeyote kuhusu kupungukiwa na nguvu za kiume atashauri akanunue dawa, kumbe angekula chakula kama vile aina mbalimbali za samaki wa baharini, matunda, mbona vyakula vya mizizi angeweza kutatua tatizo hilo.

Habari Kubwa