Kama hajawa John Cena asiwe John Cena

16Apr 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Kama hajawa John Cena asiwe John Cena

Ni 'hadithi' ya kuchekeshana tu, lakini kwa sababu msimuliaji alisisitiza kuwa ni kisa cha kweli, tulikubaliana naye, lakini bado pamoja na ukweli wake inachekesha. Hadithi yenyewe ilkuwa hivi:

Kwenye nyumba moja mtaani, dogo wa miaka sita alijifanya John Cena, yule mcheza mieleka wa WWE, na ili kuonyesha u-John Cena wake, akamkamata dogo mwingine wa miaka minne na kumnyanyua kisha 'akamgigiza' chini, pwaaa!

Kilichofuata ni mtoto yule 'aliyepigizwa' kuzimia kwa sekunde kadhaa kwa sababu 'alipigizwa' kwenye ardhi kavu yenye mchanga kidogo.

Bahati nzuri, kwenye vipindi vyote vya televisheni vinavyoonyesha michezo ya mieleka ya WWE, huwa kunatolewa onyo kuwa watu wasijaribu mchezo huo, ni hatari.

Hata hii inaonyesha kama vile baadhi ya wazazi hawajakuwa makini katika kuwaeleza watoto wao nini maana ya adhari inayotolewa juu ya mchezo huo ambao kwa asilimia kubwa unapendwa zaidi na watoto.

Kwamba vile viti vya chuma au mbao za mabenchi zinazochukuliwa na wachezaji na kuwatwanga nao wenzao huenda si vitu halisi na iwapo utawaiga kwa kutumia vitu halisi basi 'utaua'!

Ila kwa watoto wanawaona kina John Cena wakitwangana na vitu hivyo bila ya kufa au 'kuumia sana', si rahisi kukubali ukweli kuwa mchezo huo ni wa hatari, "utakuwaje wa hatari wakati kija John Cena wenyewe hawaumii?", watakuuliza.

Katika hali kama hiyo, ndipo usimamizi wa wazazi katika kuwaongoza watoto wao kuangalia mchezo huo unapotakiwa kwa vule mzazi ana nafasi ya kumweleza mtoto kila hatua ya mchezo inavyokwenda na kumtahadharisha juu ya hatari yake.

Zipo pia tamthilia kadhaa zinazopendwa na watoto ambazo kwa kuziangalia mzazi anaweza kuona kuwa zinaweza kuleta madhara kwa mtoto akiachiwa kuziangalia bila ya usimamizi wa watu wazima wa kumpa maelezo na taadhari.

Ni kwa sababu hizo umuhimu wa mzazi kuwa karibu na mtoto wakati wa kuangalia michezo isiyo na usalama unapotakiwa hasa kwa kuzingatia kuwa watoto siku zote ni watu wa kuiga mambo mapya yanayowavutia na hasa yale yenye ya kishujaa.

Wanasaikolojia na taasisi kadhaa za ustawi wa jamii Marekani umegundua tatizo la makundi ya vijana wanaoshambuliana kwa silaha ni matokeo ya watoto kutopewa ungalizi wa wazazi wao walipokuwa wakitazama sinema za kivita.

Pia kuwaachia watoto kutumia toi za silaha, zenye muonekano wa silaha halisi kunatajwa kama sababu nyingine ya madhara yanayoikumba Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya hivi sasa.

Ni dhahiri kuwa haya yote yanahitaji wazazi kusimamia kwa ukaribu michezo na 'sinema' wanazopenda watoto wao kuliko kuwaachia 'wacheze' na kina John Cine bila ya uangalizi wa karibu.

Habari Kubwa