IJUE LESENI YA KUENDESHA GARI BARABARANI- 1

29Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
IJUE LESENI YA KUENDESHA GARI BARABARANI- 1

BARABARA ni njia zote kubwa na ndogo, zinazotumiwa na jamii zikiwemo za lami, madaraja, njia za mitaani na sehemu za kuegeshea magari; isipokuwa barabara zilizomo ndani ya kambi za jeshi na nyumba za watu binafsi.

Lengo kuu la matumizi ya barabara likiwa ni urahisishaji wa shughuli za uchukuzi katika kutoa huduma muhimu kwa jamii kama kusafiri, kusafirisha watu na wanyama; kwa urahisi, kwa raha na kwa usalama toka sehemu moja kwenda nyingine, kwa makundi yote yanayotumia barabara na kwa wakati mmoja.

 

Katika Barabara, yapo Makundi sita yanayotumia barabara ambayo ni; Waendesha Magari, Watembea kwa miguu, Wapanda baiskeli, Wapanda pikipiki, Wasukuma mikokoteni na Waswaga wanyama.

 

CHOMBO CHA MOTO

 

Chombo cha moto kinachoendeshwa barabarani huwa kina mifumo saba, inayohitaji ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha chombo hicho ni kizima na hakina tatizo lolote kiwapo barabarani.

 

Mifumo hiyo ni mfumo wa umeme, tairi, maji, break, mafuta, ndani ya gari, na nje ya gari. Mifumo hii yote hufanya kazi kwa kushirikiana katika kuhakikisha kuwa gari linasafiri salama barabarani.

 

 

Kwa mfano:- Chombo kikiharibika mfumo wa umeme kinaweza kuleta matatizo hata katika mifumo mingine ya chombo na kusababisha hatari kwa watumiaji wengine wa barabara.

 

 

Katika jitihada za kuhakikisha watumiaji wa barabara wanakuwa salama, dereva ni mtu muhimu sana kuwa na weredi wa kutosha ili kukabiliana na ajali.

 

Aidha, udereva uchukuliwe kama taaluma na si kujua kuendesha gari tu kama wengine wanavyodhani.

 

Zipo aina mbalimbali za vyombo vya moto ambavyo ni; magari, pikipiki, bajaji, trekta, mitambo ya mashambani nk, ambavyo huhitaji kuhitimu na kupewa leseni kabla ya kuanza kuviendesha barabarani.

 

Pengine ajali nyingi za barabarani zinatokea si kwa kukusudia, lakini kwa kuwa yawezekana madereva wengi hawaelewi kama udereva ni taaluma na una misingi yake, ambayo ni pamoja na kupata leseni ya kuendesha.

 

LESENI YA UDEREVA

Leseni ya udereva ni hati ya kisheria inayomruhusu dereva kuendesha chombo katika daraja lililoonyeshwa katika leseni hiyo.

 

 

Leseni ya ndani ya nchi ni hati ambayo iko katika mfumo wa smart card, ambayo imetengenezwa maalum kwa ajili ya kuinua kiwango cha udereva nchini, kurahisisha upatikanaji wa takwimu za madereva nchini, kuwezesha mamlaka za udhibiti wa usalama barabarani, nk.

 

Leseni hiyo huwa na taarifa mbalimbali zinazomhusu dereva kama vile; picha ya mwenye leseni, namba ya leseni, majina matatu ya mwenye leseni, tarehe inayoonyesha imetolewa wapi na lini na tarehe ya kumaliza muda wa leseni.

 

Pamoja na taarifa hizi ambazo zinaonekana kwenye leseni kuna taarifa nyingine muhimu zinazomhusu dereva ambazo zinahifadhiwa kwa njia ya elektroniki.

 

ITAENDELEA WIKI IJAYO

 

 

Habari Kubwa