DENGUE DAR; Masaki, Tandale zimo katika maeneo 19 maambukizi tishio

23May 2019
Mary Geofrey
DAR
Nipashe
DENGUE DAR; Masaki, Tandale zimo katika maeneo 19 maambukizi tishio
  • Mikocheni, Sinza ‘hakufai’; Ilala kinara

HIVI sasa katika maeneo mbalimbali nchini, watu wana ufahamu wa namna fulani kuhusu ugonjwa wa dengue.

Hii ina maana kama si kusikia, basi wameshuhudia, kuuguza au kuugua.   

 

Kitaalamu inaelezwa kuwa, ni ugonjwa wa kitropiki unaosababishwa na virusi maarufu kama dengue. Pia, inajulikana kama ‘homa ya kuvunja mifupa’ kwa sababu inamfanya mgonjwa kuwa na maumivu makali, hadi kuhisi ‘mifupa yao inavunjika.’

Tangu mtu aambukizwe, dalili zake huanza wastani wa kati ya siku tatu hadi 14, baada ya kuambukizwa. Baadhi ya dalili ni homa kali, kuumwa kichwa, kuota vipele kwenye ngozi na maumivu kwenye misuli na maungo.

Kwa baadhi watu na mara nyingi si wengi, homa ya dengue inaweza kubadilika kwa kuhatarisha maisha. Dalili kubwa inatajwa ni kuvuja damu, kutoka mishipa ya damu.

Kwa kawaida matibabu yake yanachukua kati ya siku tatu hadi saba mgonjwa kupona. Hakuna dawa ya chanjo inayomudu kuwakinga dhidi ya virusi vya dengue.

Wakati  serikali ikiendelea na mkakati wa kudhibiti mazalia ya mbu wanaoeneza homa ya dengue na kusambaza vifaa tiba vya kupima homa hiyo katika hospitali mbalimbali nchini, watu wamebuni mbinu mbadala ya kujikinga na mbu hao.

Wakazi wa jiji la Dar es Salaam, wamekuwa wakitumia mafuta ya nazi na kuamini kuwa mbu hao hawawezi kutua kwenye mwili wa binadamu.

Ugonjwa huo ambao umeshamiri katika jiji la Dar es Salaam, pia mikoa ya Tanga, Pwani na Kilimanjaro iliyoanza kupata mgonjwa mmoja mmoja, ulianza kubainika Januari mwaka huu. Tayari takribani watu 2,000 wamebainika kuugua.

Baadhi ya wananchi wa jiji la Dar es Salaam, wamebuni kinga hiyo na kudai inazuia mbu wenye virusi vya homa ya dengue kutua miguuni, hivyo kuepuka kung’atwa na kupata maambukizi hayo.

Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa. Mohamed Kambi, anakanusha uhakika wa utaalamu huo mbadala, kudhibiti mbu waenezao homa ya dengue.

Anasema taarifa hizo ni za upotoshaji, hivyo wananchi wanapaswa kufuata taratibu za kujikinga na homa hiyo, ambazo zimetolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

“Ugonjwa huu hauna chanjo wala tiba ya moja kwa moja mpaka sasa na niwatahadharishe wanaoendelea kutoa taarifa za upotoshaji kuhusu tiba ya ugonjwa huu kupitia mitandao ya kijamii,” anasema Profesa. Kambi.

Hatua muhimu

Profesa Kambi anawaasa wananchi kuendelea kuchukua hatua za kujikinga kuumwa na mbu, ikiwa ni pamoja na kutumia dawa za kufukuza mbu.

Anasema mbinu nyingine ni kuvaa nguo ndefu za kujikinga dhidi ya kuumwa na mbu na kutumia vyandarua vyenye viuatilifu, pia kuweka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba wanazoishi.

“Watu wanasema mafuta ya nazi yanazuia mbu wenye virusi vya dengue, lakini bado hatujadhibitisha kuhusu hilo. Hivyo, ni muhimu wananchi wakafuata taratibu zilizotolewa na Wizara ya Afya,” anasisistiza Profesa Kambi.

Anasema, wanapaswa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo kwa kuzuia kunga'atwa na mbu kwa kutumia chandarua chenye dawa.

Pia, anataja mbinu nyingine ni wananchi kujipaka mafuta ya kufukuza mbu mikononi na miguuni, wakiwa wamevaa nguo ndefu zinazofunika mwili kama mikono, miguu na mgongo.

Dk. Kambi anasema, Manispaa zote za jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine, zinapaswa kutekeleza mpango wa upulizaji viuatilifu katika madimbwi yanayotuamisha maji katika kudhibiti ugonjwa huo.

Inavyokabiliwa

Profesa Kambi anapongeza hatua zinazochukuliwa na Mkoa wa Dar es Salaam katika kuudhibiti ugonjwa huo, inayojumuisha kunyunyizia dawa vya kuua wadudu kwa ajili ya kuangamiza mazalia ya mbu, linaloendelea sambamba na kutoa elimu watu kujikinga.

Anawataka wananchi waongeze kasi kutumia kamati za kitaalamu na sekta zote kudhibiti ugonjwa, pia kuwachukulia wanaokiuka taratibu na sheria za usafi wa mazingira, zinazosababisha mazalia ya mbu au kutochukua tahadhari.

Profesa Kambi anawataka viongozi wa mikoa kuanzia za juu hadi chini kama vile tarafa, kata, vijiji, mitaa na vitongoji, kuchukua hatua kupambana na ugonjwa, ulioanza kusababisha athari katika ukanda wa Pwani.

“Tunasisitiza kuwa ugonjwa huu unazuilika. Tushirikiane kudhibiti mbu, kwa sababu kufanya hivyo pamoja na kudhibiti ugonjwa huu, tutadhibiti pia magonjwa mengine yanayoenezwa na mbu,” anasema Profesa Kambi.

Anarejea somo la kuangamiza mazalia ya mbu wa dengue, ni kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama au kunyunyuzia dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo na kuondoa vitu vyote vinavyoweka mazalia ya mbu.

Mganga Mkuu wa Serikali, anayataja baadhi yake kuwa ni vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa ovyo na vichaka jirani na makazi ya watu.

Anasema, kuna haja ya kuhakikisha maua yanayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama, huku yawe yanafunika mashimo ya majitaka kwa mfuniko imara na kusafisha paa la nyumba zinazoruhusu maji kutuama.

Hali ikoje?

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hadi wiki iliyopita, zinasema kila siku kuna watu 75 kila siku kuwa na virusi vya homa ya ndengue hali inayopelekea idadi ya wagonjwa kuendelea kuongezeka na kufika 1,901.

Kati ya wagonjwa hao, 1,809 ni wakazi wa jiji la Dar es Salaam, 89 kutoka Tanga mmoja kutoka Singida, mmoja Kilimanjaro na mmoja kutoka mkoani Pwani.

“Katika kipindi cha siku tisa ambazo wizara ilikuwa ikikusanya muenendo wa hali ya ugonjwa huu nchini, kuna ongezeko la wagonjwa 674 sawa wastani wa wagonjwa 75 kwa kila siku, ikiwa ni tofauti ya wastani wa wagonjwa 32 waliopatikana kila siku kwa mwezi uliopita,” anasema Profesa Kambi.

Kwa mujibu wa Profesa Kambi, ongezeko hilo linatokana na uelewa, kuhusu ugonjwa huo kwa wananchi.

Serikali nayo imeendeleza huduma za uchunguzi zinazoendelea kupanuka kwenye vituo vya afya katika Mkoa wa Dar es Salaam na Tanga.

Aidha, anasema idadi ya vituo vinavyopima ugonjwa huo imeongezeka hadi kufikia 19, tofauti na vituo saba vilivyokuwapo awali, ili kutoa fursa kwa wananchi kupata huduma.

“Ugonjwa huu unapimwa kwenye vituo vyetu vya serikali na tunaendelea kuimarisha upatikanaji wa vipimo vya ugonjwa huu bure. Niwatake watoa huduma za afya wote na wananchi, watambue kuwa si kila homa ni dengue,’ anasema Profesa Kambi na kuongeza:“Chunguza au chunguzwa maradhi mengine na wataalamu kwenye vituo vyetu vya huduma ya kwanza, kabla ya kupima.”

Kunakopatikana huduma

Anataja vituo vya serikali kunakopatikana huduma hizo jijini Dar es Salaam, ni Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Maabara Kuu Muhimbili, Hospitali za rufani za Manispaa Amana, Temeke na Mwananyamala.

Pia, kuna Hospitali Kuu ya Jeshi la Lugalo, Hospitali za Sinza, Mnazi Mmoja na Mbagala, pia zahanati za Vijibweni, Kigamboni na FFU Ukonga.

Mbali na Dar es Salaam, Profesa Kambi, anataja kwingine kwenye huduma hizo Hospitali za Rufani za Bombo mjini Tanga, Morogoro na Tumbi, Kibaha.

Zingine anazitaja ni Hospitali ya Utete Rufiji, Mkuranga, Mafia, na Manyara. Profesa Kambi anafafanua: “Natambua vipo pia vituo binafsi vinavyotoa huduma za upimaji. Katika mikoa mingine, ufuatiliaji unaendelea na hatujapata wagonjwa wenye dalili.”

Wizara inavyojipanga

Katika kukabiliana na changamoto ya matibabu, Profesa Kambi anasema serikali imeagiza vipimo vingine vya kupima wagonjwa 30,000, vinavyotarajia kuingia nchini hivi karibuni na vitasambazwa kwenye vituo vya umma mkoani Dar es Salaam na kwingineko.

“Niwatahadharishe wanaoendelea kutoa taarifa za upotoshaji kuhusu tiba ya ugonjwa huu, kupitia mitandao ya kijamii,” anatahadharisha.

Profesa Kambi anasema, wizara kwa kushirikiana na mikoa na halmashauri, imechukua hatua, ikiwamo kuandaa mpango wa dharura kukabiliana na ugonjwa huo, inayojumuisha uandaaji mwongozo wa matibabu ya ugonjwa, kuimarisha ufuatiliaji na utoaji elimu.

Dar vitani

Mganga Mkuu Profesa Kambi anasema, wizara imetuma timu za wataalamu kuungana na timu za Mkoa wa Dar es Salaam, kuudhibiti ugonjwa huo.

Maganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Yudas Ndugile, anataja maeneo yenye wagonjwa wengi katika jiji hilo na idadi yake katika mabano ni: Ilala (253); Sinza (223); Vingunguti (86); Kariakoo (79); Mbezi (78); Kimara (65); Masaki (56); Msasani (50); Wazo (49); Kinondoni (45); Mikocheni (40).

Maeneo mengine ni Tabata (41) Gerezani (40), Mbezi Beach (37), Tandale (38), Kijitonyama (34), Ukonga (26), Mwenge (28) na Tegeta (270.

“Hivi ndio vituo ambavyo zimetoa wagonjwa zaidi ya 25 lakini zipo kata nyingine nyingi ambazo zina wagonjwa wa homa ya Dengue katika wilaya zote za jiji hili,” anasema Dk. Ndugile.

Anasema mkoa huo unendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu kujikinga na maambukizi ya homa hiyo inayosababishwa na mbu aina ya ‘Aides Mweusi’ mwenye madoa meupe ya kung’aa.

Dk. Ndugile anasema, dalili za ugonjwa huo ni homa ya ghafla, maumivu ya kichwa hususani machoni, maumivu ya viungo na uchovu.

“Dalili hizi huanza kujitokeza kati siku ya tatu hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya homa ya gengue. Hivyo ni muhimu wananchi kuchukua tahadhari.

Habari Kubwa